26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

LAANA YA ARGENTINA INAVYOMTESA MARIO GOTZE

NA BADI MCHOMOLO


HAKUNA kitu kibaya kama wachezaji wa soka wanaotikisa dunia kwenye klabu zao kushindwa kutwaa taji la Kombe la Dunia katika maisha yao. Mastaa wengi waliopita waliweza kutikisa dunia kwa kutwaa maji mbalimbali ndani ya klabu pamoja na Kombe la Dunia wakiwa na Mataifa yao.

Wachezaji ambao wanatikisa kwa sasa duniani ni pamoja na Lionel Messi wa Argentina, Cristiano Ronaldo wa Ureno pamoja na Neymar wa Brazil. Wachezaji hao wote hawajafanikiwa kutwaa Kombe la Dunia katika maisha yao mbali na kuzisaidia klabu zao na kuzipa mataji mbalimbali.

Mwaka 2014, nyota wa Argentina na bingwa mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Lionel Messi, aliweza kupambana na kufanikiwa kuipeleka timu yake katika fainali ya Kombe la Dunia nchini Brazil na walikutana na Ujerumani katika fainali hizo.

Wengi waliamini kuwa Messi angeweza kuwapa Argentina taji hilo kutokana na uwezo wake, lakini alishindwa kufanya hivyo kwa kuwa wapinzani wao Ujerumani walikuwa bora na walicheza kwa umoja.

Messi alikuwa bora zaidi ya mchezaji mmoja mmoja wa Ujerumani, lakini ubora wake haukuweza kushirikiana vizuri na wachezaji wenzake wa timu hiyo na kuweza kutwaa taji hilo.

Dakika 90 za fainali hizo zilikamilika bila ya timu yoyote kuona lango la mwenzake, lakini dakika za ziada ziliweza kuwapa ubingwa Ujerumani ambapo mwaka huu wanakwenda nchini Urusi wakiwa mambingwa watetezi.

Bao hilo la pekee liliwekwa wavuni na kinda wao wa kipindi hicho Mario Gotze akiwa na umri wa miaka 21. Mchezaji huyo alitokea benchi kabla ya kuongezwa kwa dakika 30 mara baada ya kumalizika kwa dakika 90.

Mchezaji huyo aliingia katika dakika ya 87, akichukua nafasi ya Miroslav Klose, aliyekuwa anacheza nafasi ya ushambuliaji. Mchezaji huyo kwa sasa ni mmoja kati ya viongozi wa timu hiyo ya Taifa ya Ujerumani tangu alipoamua kuachana na soka mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo.

Chuki na laana za mashabiki wa soka nchini Argentina zilianza ikiwa zimesalia dakika nane kati ya zili za nyongeza ili kutimia 120, Gotze aliweza kuandika bao ambalo lilidumu dakika zote nane hadi mchezo unamalizika na Ujerumani wanatwaa ubingwa.

Ilikuwa historia kubwa kwa kinda huyo kuchukua ubingwa dhidi ya staa wa soka wa dunia Messi, Argentina hawakuamini kama kweli mchezaji huyo ameweza kuzima ndoto za staa wao na staa wa dunia kwa ujumla, hivyo kuanzia hapo Argentina hawakuweza kumsahau mchezaji huyo na hawatoweza kumsahau katika maisha yao yote.

Laana sio lazima itolewe na wazazi hapana! Mtu yeyote anaweza kutoa laana au radhi endapo unaweza kumfanyia kitu kibaya ambacho kitakuwa kinamuumiza katika sehemu kubwa ya maisha yao.

Laana au radhi ya Argentina waliielekeza kwa Gotze na sio Ujerumani, leo hii mchezaji huyo ameachwa kwenye kikosi cha Ujerumani kwenye michuano ya Kombe la Dunia Urusi bila ya kujali ndio mchezaji ambaye aliwapa ubingwa mwaka 2014, lakini ameachwa na kocha wao yule yule Joachim Low.

Vita ya panzi ni furaha ya Kunguru, kuachwa kwa mchezaji huyo kunawafanya Argentina wawe na furaha kubwa baada ya kupandikizwa chuki ya miaka minne ilipo moyoni mwao, hivyo Argentina wana furaha kuona adui yao hayupo kikosini.

Gotze ameachwa kwenye kikosi cha Ujerumani kutokana na kiwango chake kushuka akiwa na klabu yake ya sasa ya Borussia Dortmund.

Msimu huu mchezaji huyo amepata nafasi chache katika klabu yake kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu. Mara ya kwanza kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo msimu huu ni Agosti 19 mwaka jana baada ya kukaa nje kwa miezi saba.

Kutokana na hali hiyo ya kukosa nafasi ndani ya klabu yake kukamfanya kocha wa Ujerumani kuachana na mchezaji huyo kuelekea urusi. Inaweza kuwa moja ya laana ya Argentina kwa kile alichowafanyia mwaka 2014, lakini hali hiyo ni kawaida katika sehemu ya maisha ya wachezaji wa soka duniani kupitia vipindi vigumu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles