26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Kwa weledi huu, Simba itafika anga za Al Ahly, Mazembe, Zamalek

 SOSTHENES NYONI 

WIKI mbili zilizopita, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, alimwanika Barbara Gonzalez, kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya wa klabu hiyo.

Barbara amechukua nafasi ya Senzo Mbatha aliyejiuzulu na kulamba ajira mpya akiwa mshauri wa mfumo wa mabadiliko katika klabu ya Yanga. 

Akimtambulisha Barbara, Mo Dewji alisema: “Hatujakurupuka kufanya maamuzi na wala sio maamuzi yangu, ni ya kikao kwani tulikaa jana (Ijumaa) na kuamua kumpitisha Barbara, anakuwa CEO wa kwanza mwanamke. Ni mchapakazi na anaipenda Simba, hivyo tunaamini kila kitu kitakwenda sawa.” 

Lakini baada ya Barbara kutangazwa kushika wadhifa huo, wapo waliotilia shaka uwezo wake wa kuongoza klabu kubwa ya Simba. 

Lakini pia wapo waliounga mkono uteuzi wake na hasa baada ya kufatilia wasifu wake na kubaini ana uzoefu wa kutosha wa kufanya kazi katika taasisi za kimataifa. 

Wanaompinga Barbara wanadai kuwa bosi huyo mpya wa Simba hana uzoefu na mambo ya soka, hivyo hakustahili kabisa kupewa nafasi hiyo. 

Tukiachana na mengine yanayozungumzwa juu ya Barbara, nimeona nilizungumzie hili la uzoefu wa mwanadada huyo katika masuala ya soka. 

Mitazamo hii tofauti ndiyo ililolishawishi MTANZANIA kumsaka Barbara na kufanya nae mahojiano ya kina yaliyoegemea kwenye uzoefu wake kwenye soka na je anaonaje kupata fursa ya kuiongoza klabu kubwa ya Simba. 

Barbara anasema amekuwa karibu na soka kwa muda mrefu, ikiwamo kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na lile la Afrika (CAF). 

Anasema kuwa, kuionyesha jinsi alivyo mpenzi wa soka, alishawahi kukutana na mshambuliaji nyota wa zamani wa Arsenal, Barcelona na Ufaransa, Thiery Henry na mastaa kibao wanaotamba Ulaya. 

“Watu wengi hawafahamu kuwa mi si mgeni katika masuala ya soka kwa sababu mara zote nimekuwa nyuma, sikuwa najiweka mbele kwa kila nililofanya. 

“Si FIFA na CAF pekee, nimekuwa karibu na taasisi nyingi za kimataifa na hata klabu kubwa za soka za Ulaya kama Arsenal, Liverpool, Everton, FC Porto na Juventus ya Italia. Kama unakumbuka Mo aliwahi kukutana na viongozi wa Juventus, Arsenal, Porto, Liverpool na Everton…ni mimi niliyemuunganisha nao. 

“Hivyo, mimi si mgeni na mambo ya soka, nimefanya mengi, tatizo sikuwa naweka wazi kila kitu na huwa sipendi kujianika nimefanya nini. Hata Simba nimeshiriki mambo mengi. 

“Nilishiriki katika mchakato wa mabadiliko ya kimfumo Simba tangu mwaka 2016. Nilikutana na wanasheria jijini London (England) kubadilishana nao uzoefu katika masuala haya ya mabadiliko ya kimfumo wa uendeshaji wa klabu za soka na nilijifunza mengi kwani wenzetu walishaanza mambo hayo miaka mingi,” alisema Barbara. 

Lakini hata kama Barbara asingekuwa mwanafamilia wa soka, kwa elimu yake, angeweza kushindwa kutekeleza majukumu yake ndani ya klabu kama Simba ambayo nyuma yake kuna watu kibao wanao ufahamu mpira na tamaduni zake. 

Ukimweka kandi Mo ambaye anakiri kutokuwa mtaalum wa soka zaidi ya mapenzi aliyonayo kwa mchezo huo na Simba, wapo watu wengine wanamchango mkubwa katika kuifikisha klabu hiyo hapa ilipo. 

Jina la Crescentius Magori si geni katika medani ya soka kama ilivyo kwa Zacharia Hanspoppe. 

Kwa mtu msomi kama Barbara mwenye uzoefu mkubwa katika taasisi za kimataifa, ni wazi Simba inaelekea kule ambako wanazi wengi wa klabu hiyo wanatamani kuona ikifika. 

Lakini pia, nani asiyemfahamu Mulamu Ng’hambi? Salim Abdallah ‘Try Again’ je msomi Mwina Kaduguda ambaye anaufahamu nje ndani mpira wa Tanzania na mazingira yake? 

Barbara pia anazungukwa na vichwa vingine vinavyolifahamu vilivyo soka kama Kassim Dewji ‘KD’, Hamis Kisiwa, Mohammed Nassor na Musleh Rawah. Atafeli vipi mwanadada huyo iwapo atapewa ushirikiano wa kutosha? 

Mtu gani wa mpira asiyemfahamu KD? Kisiwa, Musleh na Nassor? Kwanini watu wawe na wasiwasi na Barbara kwamba anaweza kufeli Simba wakati anazungukwa na vichwa kama hivyo? Labda tu iwapo watakuwa na agenda yao ya siri ya kumuhujumu. 

Lakini kwa ufahamu wangu, Barbara hawezi kufeli Simba iwapo atawakaribisha vigogo hao wa Msimbazi na wao kumpa ushirikiano wa kutosha kwa maslahi ya klabu yao na soka la Tanzania kwa ujumla. 

Na kwa kuwa Mo Dewji alikiri kuwa wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi Simba walibariki uteuzi wa Barbara kuwa CEO mpya Msimbazi, ni wazi kuwa vigogo hao hapo juu wanaounda bodi hiyo, watampa ushirikiano wa kutosha mwanadada huyo. 

 Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Asha Baraka ‘Iron Lady’, anasema hawakukurupuka kumkkabidhi jukumu hilo Barbara. 

“Kuna watu wanadhani tumekurupuka katika uteuzi wa Barbara au ilikuwa ni bahari mbaya, nikuhakikishie Barbara ni mwanamke wa chuma, ana uwezo wa kuifanyia makubwa Simba. Kwa wasiofahamu, tulimpa jaribio la kuandaa shughuli nzima ya Simba Day na alifanikiwa kama sote tulivyojionea. 

“Kwa watu waelewe kuwa Barbara yupo siku nyingi Simba, zaidi ya mwaka sasa anafanya kazi za Simba. Watu wanashtuka sasa hivi, sijui kwa kuwa ni mwanamke! Mwanamke pia ana uwezo wa kufanya kazi nzuri na kubwa tu. 

“Sidhani kama wanachama wa Simba wana haja ya kuwa na hofu ya uteuzi wa Barbara uliofanywa na bodi, tupo wajumbe wa bodi walioteuliwa na Mo na tupo tuliochaguliwa na wanachama ambao tunalinda maslahi ya klabu. Hatujaona sehemu ambayo tumekosea, pale tutakapoona kuna jambo halipo sahihi, hatuwezi kukubali. 

“Lakini pia ieleweke, Mo ameifanyia makubwa sana Simba na anaipenda sana Simba, kama kuna mwanachama ambaye kuna jambo haelewi, ni vema aulize, nasi tupo tutaliweka wazi, hakuna haja ya kuanza kurumbana wenyewe kwa wenyewe na kutoa mwanya kwa wapinzani wetu kutuvuruga. 

“Naamini iwapo Barbara atapata ushirikiano wa kutoska kutoka kwa viongozi, mashabiki na wanachama, atatufikisha mbali,” anasema Asha ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (Aset), wamiliki wa bendi ya muziki ya African Stars ‘Twanga Pepeta’. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles