23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

KUTANA NA MAMA LISHE ASIYEKATA TAMAA

Alianza kubeba chakula kwenye ndoo, akahamia chini ya Mwarobaini


Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

NIA ya dhati ya kusaka maendeleo ndiyo iliyomsukuma Zena Abein kuanza kufanya biashara ya kuuza chakula kujipatia kipato cha kumsaidia yeye na familia yake.

Zena ni mwenyeji wa Mkoa wa Pwani, alizaliwa katika Hospitali ya Rufaa Tumbi na kulelewa na wazazi wake katika eneo la Mwendapole huko Kibaha.

Anasema yeye na mumewe waliamua kuja kuishi Dar es Salaam kutafuta maisha na kwamba walikwenda kupanga chumba eneo la Mwananyamala.

“Tumejaliwa mtoto mmoja, maisha yalikuwa magumu, mume wangu ndiye ambaye alikuwa akitoka kwenda kutafuta fedha ili tuishi,” anasema.

Anasema kila siku alikuwa akitafakari jinsi gani ambavyo angeweza kusaidiana na mzazi mwenziye kutafuta fedha kuendesha maisha yao lakini hakupata jibu kwa muda mrefu.

“Pale tunapoishi nilikuwa naona watoto wa mama mwenye nyumba wangu wakiamka mapema asubuhi wanaandaa chakula na kuondoka nacho kila siku, walikuwa wanakwenda kukiuza huko eneo la Sayansi, Kijitonyama.

“Ikabidi niwaulize wenzangu wanawezaje kufanya biashara kwa mtindo wa namna hiyo, wakanieleza, mama mwenye nyumba akaniambia ni vema na mimi nitafute eneo la biashara nianze kuuza kama wanavyofanya watoto wake,” anasema.

Zena anasema alilipokea wazo hilo na akaamua kulifanyia kazi, alianza kutafuta eneo la biashara akalipata Sinza Madukani.

“Mwaka 2000 ndipo nilianza rasmi kufanya biashara hii nikiwa na mtaji wa Sh 20,000,” anasema.

 

Alimudu vipi

“Niliamka mapema asubuhi na kumuandaa mume wangu ili aende kazini, alipoondoka ndipo na mimi nilianza kupika vyakula vyangu kisha naweka kwenye ndoo na kutafuta usafiri hadi Sinza Madukani.

“Niliposhuka kituoni nilienda kukaa chini ya mti wa Mwarobaini na kuanza kuita wateja, kulikuwa na madereva taxi ambao walipoonja chakula changu waliona ni kitamu na wakaanza kuwaita wenzao nao waje kula.

“Nilipika wali wa nazi siku hiyo, basi walikuwa wakiitana na kuambiana njooni muonje wali wa Pwani basi siku hiyo niliuza chote kikaisha, nilimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli,” anasimulia.

Anaongeza; “Tangu siku hiyo ndipo likaanzishwa jina ‘Mwarobaini Hoteli, kwa sababu nilikuwa sina mahala pa kuuzia na nilipofika nilikuwa nakaa chini ya mti huo wa Mwarobaini na kuuza chakula changu,” anasema.

Zena anasema idadi ya wateja wake ilizidi kuongezeka kila siku ambapo alipata watu wa saluni, wauza maduka na madereva wa taxi ambao walifika kununua chakula.

“Na hao ndiyo wateja wangu wakuu hadi leo, kila siku nilikuwa nahakikisha saa saba nimefika hapa kuwauzia chakula,” anasema.

 

Changamoto ya usafiri

Anasema alikumbana nayo kila mara kwani alilazimika kusafirisha chakula kutoka Mwananyamala hadi Sinza Madukani.

Anasema baadhi ya madereva na makondakta walimzuia kuingia kwenye gari zao na wakati mwingine walimtaka kulipa nauli zaidi.

“Wakati ule nilipoanza nauli ilikuwa Sh 300, unajua tena usafiri wetu ndani ya jiji hili, wakati mwingine nilikuwa napata shida kusafiri, kuna makondakta walikuwa wananikataa, wengine walikuwa wananitoza Sh 500,” anasema.

 

Wateja waongezeka

Anasema hata hivyo hakukata tamaa, aliendelea kusonga mbele kutafuta fedha na kwamba idadi ya wateja wake iliongezeka na kwa siku anaweza kupata wateja 80 hadi 100.

Anasema alilazimika kutafuta eneo maalumu la kufanya biashara yake na aliajiri wasaidizi wawili.

“Sasa sipiki tena nyumbani, naamka mapema na kutekeleza majukumu yangu ya kifamilia, kisha nakuja ofisini kwangu, nimeajiri wafanyakazi wawili wa kunisaidia,” anasema.

Anaongeza; “Leo hii mtaji wangu umeongezeka na kufikia zaidi ya 85,000, nimeweza kuajiri wafanyakazi wawili ambao kila siku nawalipa Sh 5,000 kila mmoja na napata faida ya kati ya Sh 10,000 hadi 12,000 kila siku,” anasema.

 

Anaiogopa mikopo

Zena anasema mikopo ni mizuri lakini anaiogopa mno kwani changamoto kubwa hujitokeza pindi mtu anaposhindwa kurejesha marejesho.

“Kwa hiyo sijawahi kukopa kwa ajili ya kukuza biashara yangu, maana unaweza kukopa ukashindwa kurejesha wanakuja kubeba masufuria na kujikuta ukipata hasara, ndiyo maana mikopo naiogopa, naridhika na kidogo ninachokipata, kinanitosha,” anasema.

Anasema katika biashara yake hiyo, changamoto kubwa anayokumbana nayo ni baadhi ya wateja kuwa wakorofi.

“Wapo ambao wakila hawataki kulipa, unakuta mtu anakuzungusha hadi mgombane ndiyo akulipe, kwa hiyo tunaenda nao hivyo hivyo,” anasema.

 

Mafanikio

Zena anasema kwa kuwa alipoanza kufanya biashara hiyo ndiyo walikuwa wakianza maisha na mumewe hivyo ilimuwezesha kununua vitu vya ndani.

“Nimeweza pia kununua kiwanja huko Kibaha na tayari tumeanza ujenzi wa nyumba yetu ya kuishi,” anajivunia.

Anasema kwa sasa ana mpango wa kupanua biashara yake hiyo iwapo Mungu atamjalia atatafuta ‘fremu’ ili aiboreshe zaidi.

“Nitatafuta ‘fremu’ niboreshe kwa sababu hapa ninapofanyia biashara kwa sasa naona wateja wangu wanakaa kwa tabu,” anasema.

 

Wategemezi

Anasema kwa biashara yake hiyo anamudu kumsaidia mumewe majukumu ya kusomesha mtoto wao ambaye yupo shule ya msingi hivi sasa.

“Lakini pia namsaidia mama yangu mdogo ambaye alitulea baada ya mama yetu kufariki na nawasaidia pia wadogo zangu ambao wananitegemea,” anasema.

 

Wito kwa wanawake

Anawashauri wanawake wenzake kuamka na kuchapa kazi kwani maisha ya sasa yamebadilika na si kama yale ya zamani.

“Wanawake wasikae majumbani kusubiri wanamume wakafanye kazi walete fedha za matumizi, maisha yamebadilika mno hivyo ni lazima wote mtoke mkatafute, mwenzako akija na Sh 2,000 na wewe 1,000 tayari mnakuwa na 3,000 zitakazowasaidia katika maisha yenu,” anasema.

 

Rai kwa Serikali

Anaiomba Serikali isikie kilio cha wananchi wake kwani maisha yanazidi kuwa magumu kadri siku zinavyosonga mbele.

“Yaani tangu wakati wa uchaguzi hadi leo, maisha ni magumu na kila siku yanazidi kuwa magumu, watu hatuna fedha mtaani, tunafanya biashara lakini wateja wamepungua mno.

“Hakuna wateja wa kutosha kwa kweli, hapa nilikuwa napika kilo 15 za wali lakini nimelazimika kupunguza hadi kilo 10, nilikuwa napika makande na ndizi lakini vyakula hivyo nimeamua kuacha kuvipika kwa sababu hakuna wateja,” anasema.

Anaongeza; “Watu hawana fedha… zamani mtu mmoja alikuwa anakula sahani moja ya wali peke yake lakini leo hii wakija wanakula wawili sahani moja.

“Nimesema awali madereva taxi ni miongoni mwa wateja wangu wakuu lakini nao wanalalamika wateja hakuna, biashara ni mbaya kusema ukweli, hao Yono wanakuja kuwakamata kila siku mchana na usiku.

“Hata hao wafanyabiashara wa maduka nao wanalalamika hawana fedha, wanalipia fremu fedha nyingi lakini biashara hakuna, kwa hiyo mambo yanazidi kuwa magumu kila siku,” anasema Zena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles