26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

… kupambana na Rais Kenyatta mwakani

Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, akiwa katika mahojiano maalumu na wahariri wa magazeti ya Kampuni ya New Habari ( 2006) Ltd, Dar es Salaam hivi karibuni.
Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, akiwa katika mahojiano maalumu na wahariri wa magazeti ya Kampuni ya New Habari ( 2006) Ltd, Dar es Salaam hivi karibuni.

*Ajivunia kuisambaratisha Tume ya Uchaguzi

Na Ratifa Baranyikwa,

WAZIRI Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, amesema endapo wananchi watamtaka agombee urais katika uchaguzi wa mwakani, atafanya hivyo.

Odinga ambaye endapo atagombea uchaguzi huo itakuwa ni mara ya tatu, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Wahariri wa New Habari (2006) Ltd, wiki hii Dar es Salaam.

“Wengine wanasema Raila sasa astaafu, Raila sasa Mzee na mimi nasema kama wananchi wananitaka mimi nitakuwepo debe,” alisema.

UCHAGUZI 2017/UFISADI TUME YA UCHAGUZI

Katika mahojiano hayo, Odinga pia alizungumzia juu ya hatua yao ya kuishtaki Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya nchini humo (IEBC) kwa wananchi.

Raila ambaye alianza kwa kueleza mlolongo wa matukio ambayo yanafanywa na viongozi wa Serikali ili kuhakikisha wanabaki madarakani, aliitaja Tume ya Uchaguzi kuwa miongoni mwa vyombo wanavyotumia kujihalalishia ushindi.

Alisema wanazo rekodi zinazoonyesha kwamba katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Serikali iliyoko madarakani haikushinda kiti cha urais.

Odinga alisema hilo linathibitishwa na idadi ya watu waliopiga kura kuchagua wabunge, maseneta, wawakilishi wa wanawake, magavana, madiwani n.k, ambao walikuwa milioni 10.

Hata hivyo, Odinga alieleza mshangao wake kuhusu wapiga kura milioni 12 waliomchagua rais.

Huku akicheka, Odinga alishangaa walikotoka watu milioni mbili waliokwenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua rais tu.

“Ndio maana tukasema tujadili Tume ya uchaguzi wakakataa walipokataa tuka force kwenda street kupinga.”

Alisema kwa sababu walikataa mazungumzo, Katiba ya Kenya kifungu cha 35 kinawapa haki ya kukusanya saini za wananchi milioni 1.6 kuipinga Tume.

Odinga alisema walipokusanya saini hizo na kuzituma IEBC, ikasema saini zaidi ya laki saba zilikuwa batili kwa sababu wengine walichora faru.

“Tukawahoji mlijuaje kama hiyo ndovu si sahihi yake?” alisema Odinga huku akicheka na kuongeza:

“Tukawaambia kama kuna upungufu mngetupatia fursa sisi kujaza ili ifike milioni moja, wakasema tulipungua kama laki moja na kitu ifike milioni   wakakataa sasa tukaamua kwenda kwa wananchi tukasema kila Jumatatu tunakuja.

“Walipoona inaenea kila mahali wakaogopa tukaanza mazugumzo, tukaunda kamati ya wabunge wetu saba na wao saba hivi sasa tumekubaliana ile tume yote inakwenda nyumbani sasa wanaandaliwa kiinua mgongo waondoke, tulisema IEBC must go.”

Aidha, Odinga alisema hivi sasa wamekubaliana daftari la wapiga kura lisafishwe kwa kuondoa wapiga kura bandia na marehemu.

“Tuweke tume mpya, tumekubaliana tutaweka kamati maalumu ya kuteua makamishna wapya itakuwa ndani ya siku 30 ili waanze kufanya kazi yao ya kusajili.

“Tunataka usajili wapiga kura uanze Desemba mwaka huu hadi Januari na baadaye watengeneze registration mpya mwezi wa pili iwe tayari imehakikiwa, uchaguzi utakuwa Agosti 8, mwakani kama kila kitu kitu kitatengenezwa vizuri tutakuwa na sababu gani ya kushindwa?” alihoji Odinga.

AIZUNGUMZIA JUBILEE

Odinga alisema hatua hiyo ya kuisafisha  IEBC ni pigo kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Katika hilo alizungumzia pia muungano unaondwa na Jubilee unaotarajiwa kuzinduliwa mwezi Septemba mwaka huu kuwa vyama 12 vinavyotaka kuungana hata kama vingekuwa 100 havimtishi.

“Vyama ambavyo viko pale ni viwili au vitatu tu ndio vyenye wabunge… wengi wao hawakupata hata udiwani, vingi ni kama jina tu…na sisi tunasema hiyo ni kama yule mnyama anayenuka, fungo ni fungo tu hata ukiita jina gani,” alisema.

Alisema CORD watafanya muungano wa pamoja na viongozi wanaotaka mabadiliko na wana hakika watakuwa na muungano mkubwa hivyo haoni sababu ya kutopata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.

APINGA KIWANGO CHA KAMPENI

Odinga pia alipinga ukomo wa kiwango cha fedha uliowekwa kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa mwakani akisema unatoa mwanya wa kupenyeza fedha chafu.

“Kwa Rais wameweka Ksh bilioni 5, kwa Tanzania ni kama bilioni 100, Gavana kama Tsh bilioni 10 na kwa Diwani kama Tshs milioni  200, sasa mishahara ya huyu haifiki hata hiyo kwa miaka mitano sasa ata-correct hiyo pesa kutoka wapi? Hiyo wanataka tufanye kama tutakatishe fedha ya raia ambayo umeiba,” alisema.

Katika hilo, Odinga aliishutumu Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuiba fedha ya mkopo kutoka nchi za Ulaya ili waweze kuzitumia kununua wananchi katika uchaguzi wa mwakani.

“Wao walikwenda katika soko la fedha la Ulaya kukopa pesa, wakakopa Dola bilioni 2.8 lakini ile waliyoleta iko Dola bilioni 1 ambayo hawakuleta yaani wamekopa huko nje na wakaiba huko huko.

“Ile ambayo walileta ni deni sasa Mkenya ni mtu mwenye deni kubwa sana duniani, kila Mkenya ana deni kama Ksh 85 yaani kila Mkenya akiwemo mtoto ambaye hajazaliwa Ksh 85 inamgonja. Hii pesa ingejenga barabara, ingetengeneza miradi ya maji au shule ni afadhali unalipa lakini haikukufanyia kazi yoyote.

“Hiyo ni pesa wako nayo wameweka wanataka kutumia kununua wananchi, so that’s why we say we don’t support this kind of expenditure limits must be reasonable to curb corruption,” alisema.

Odinga pia alihoji kiasi cha Ksh milioni 50 sawa na bilioni 1 za Tanzania kinachotumiwa kila mwezi na Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto kwa ajili ya harambee.

“Makamu wa Rais kila wiki hutoa pesa, kila mwezi anatumia kama Ksh mil 50, hiyo ni bilioni 1, pesa ya Tanzania hiyo ni hela yake mwenyewe, kila mwezi harambee. “Sasa anasema kama Raila si mchoyo na yeye atoe pesa kwa harambee,” alisema.

VIONGOZI WANAOHAMA

Kuhusu kuhama kwa Ababu Namwamba kutoka muungano wa CORD, Odinga alirudia tena kauli yake kwamba kiongozi huyo amenunuliwa.

“Mambo ya viongozi kununuliwa, kupigwa bei, hayakuanza jana yalianza wakati wa Moi wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi.”

Odinga alisema Moi alikuwa akiwanunua wabunge wakati ule kwa sababu Katiba ilimpa mamlaka makubwa ya kuamua wapi na kwa nani apeleke maendeleo.

“Siku hizi Katiba tumebadilisha, Rais hawezi kuleta maendeleo kwa mtu yeyote, Katiba imeweka level mbili za kiserikali, ya kitaifa na county, sasa pesa inagawanywa Serikali ya kitaifa na county na pesa inatolewa na Bunge…hivyo wewe kama mbunge shiriki katika bajeti kuhakikisha pesa inakwenda kwenye wilaya yako na si kwenda kupiga magoti chini kwa rais eti mimi nataka maendeleo, hakuna maendeleo ya pesa ya kupewa hiyo ni maendeleo ya tumbo,” alisema Odinga.

Alisema kwa sababu hiyo ndio maana hata Namwamba amefukuzwa nyumbani kwao.

UKABILA

Katika mahojiano hayo, Odinga pia alizungumzia dhana ya ukabila nchini Kenya ambayo baadhi wamekuwa wakiamini kuwa ni kikwazo cha demokrasia nchini humo.

Katika hilo alisema dhana hiyo imekuzwa na wasomi wachache wenye masilahi binafsi.

“Mimi ni Pan africanist, mimi nataka kuona Waafrika wanaungana na sisi pan africanist tuna believe the ability of African people can develop Africa, ile mutu ambaye analeta migawanyiko ya watu kwa misingi ya ukabila niseme ni mpumbavu.

“Maana yake Afrika ina shida nyingi zaidi, wale wanaoleta ukabila ni wasomi ‘the elite’ ndio wanaosema hivyo for their selfish interest,” alisema.

Huku akitoa takwimu na mifano kuonyesha kwamba ukabila unaozungumzwa ni propaganda, Odinga alisema:

“Idadi ya Wakikuyu wote ni asilimia 17, Luo 15, Kalenjini 13, Akamba 11 na watu wa maeneo ya Pwani 10,  so you cannot win election Kenya in basis of ukabila,” alisema.

Akijitolea mfano yeye mwenyewe ambaye amepata kuwa mbunge wa Jimbo la Lang’ata kwa zaidi ya miaka 20, alisema kama ukabila unaozungumzwa ungekuwepo asingekuwa mbunge wa jimbo hilo.

Si hilo tu, Odinga alikwenda mbali na kusema kama kungekuwa na ukabila asingemfanyia kampeni Mwai Kibaki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

“Mimi ningekuwa nina shida na Wakikuyu nisingesema Kibaki tosha, nilijua Kibaki ni Mkikuyu lakini Kibaki ni Mkenya, Wakikuyu ni Wakenya na wakaniita wakati huo ‘Mtongoleajamba’, eti mimi shupavu, shujaa kama Mkikuyu hana shida na mimi kama ana shida na mimi ni elite they know it,” alisema.

Alisema hata mtoto wake ameoa Mkikuyu na ana marafiki wengi Wakikuyu na kwamba anaungwa mkono na kushinda uchaguzi katika maeneo ya Pwani, Kaskazini, Nyanza, Mashariki, Magharibi, Lift Valley na Nairobi.

Kuthibitisha hilo alisema wao Cord wanadhibiti majimbo 24 kati ya 47, hivyo haoni dhana ya ukabila inayoelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles