27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Sh bilioni 16 za watumishi hewa zaokolewa

Angela Kairuki
Angela Kairuki

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeokoa Sh bilioni 16 ambazo ingelipa mishahara ya watumishi hewa 16,127 kwa Agosti, mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, Dar es Salaam jana.

Alisema kuokolewa kwa fedha hizo ni matokeo ya kazi ya uhakiki wa watumishi katika taasisi mbalimbali za Serikali ambayo hadi sasa imefanikiwa kwa kuridhisha.

Waziri Angela alisema kazi ya uhakiki inaendelea na kwamba wizara yake ilikwishatoa agizo kwa waajiri wote kuwasilisha taarifa za mwisho za uhakiki ili kuwabaini na kuwaondoa watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mshahara kabla ya malipo ya mishahara ya mwezi Juni mwaka huu.

Alisema muda huo umekwishamalizika hivyo alitoa siku sita kwa taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa za watumishi wake kutekeleza agizo hilo kabla ya Agosti 26, ili aweze kuwasilisha ripoti kwa Rais John Magufuli.

“Kati ya waajiri 409, ni 264 waliowasilisha taarifa za watumishi wanaowaongoza huku 201 zikiwa zimekwishathibitishwa kuwa na watumishi hewa 16,127. Hawa Serikali ingewalipa shilingi bilioni 16 katika malipo ya mishahara kwa mwezi Agosti pekee.

“Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, 63 wamethibitisha kutokuwa na watumishi hewa na waajiri 145, hawa bado hawajawasilisha taarifa zao wizarani. Ninawapa siku sita kuanzia leo (jana) kuleta ripoti zao kwangu. Kwa maana kwamba kabla ya Agosti 26 niwe nazo.

“Baada ya muda huo taarifa zote zitawasilishwa kwa Rais Magufuli kwa hatua zaidi,” alisema Kairuki.

Aidha, waziri huyo alieleza kuwa tayari maofisa utumishi watatu wamesimamisha kazi na watumishi hewa 606 wamekwishafikishwa katika vyombo  vya dola.

Alisema wizara yake inaendelea na kazi ya uhakiki wa kushtukiza wa watumishi hewa kwa taasisi 70 ili kuoanisha na ripoti za waajiri, kazi ambayo ilianza Agosti 15, mwaka huu.

“Taarifa zinazowasilishwa wizarani ni pamoja na jina la taasisi, fungu, hundi namba ya mtumishi, jina kamili la mtumishi, cheo cha mtumishi na jina la tawi la benki ambalo mtumishi anapitishiwa mshahara.

“Pia akaunti namba ya benki ya mtumishi, tarehe ambayo mtumishi aliondolewa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi, mshahara na mengineyo,” alisema.

Alizitaja baadhi ya taasisi ambazo hazijawasilisha taarifa za watumishi wake kuwa ni pamoja na Baraza la Elimu na Mafunzo ya Ufundi (NACTE), Baraza la Mazingira (NEMC), Bodi ya Korosho, Chuo cha Diplomasia, Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) na Halmashauri ya Jiji la Mwanza na wengineo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles