Na Ratifa Baranyikwa,
MWANASIASA maarufu nchini Kenya, Raila Odinga, amesema amemuuliza Rais John Magufuli kuhusu hatua yake ya kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Odinga ambaye anaongoza muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya (CORD), alisema tofauti na maelezo anayoyasikia nje, katika mazungumzo yao Rais Magufuli alimwambia hajapiga marufuku mikutano ya kisiasa ikiwemo ile ya wanasiasa au viongozi wa juu wa kitaifa wa vyama vya siasa wasio na majimbo.
Alisema badala yake alimwambia amepiga marufuku mikutano ya kubeba watu kwenye mabasi kutoka eneo moja kwenda jingine kwa madhumuni ya kufanya vurugu.
Odinga aliyekuwa nchini kwa shughuli binafsi, yeye na familia yake, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii katika Hoteli ya Hyat Dar es Salaam na wahariri wa magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.
Katika mahojiano hayo yaliyoanza kuchapishwa wiki hii na gazeti dada la MTANZANIA JUMAPILI la RAI, Odinga pia alizungumzia mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hatua ya wabunge wa upinzani kususia vikao vyake, lakini pia uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiunga upinzani na kisha kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Odinga anayetambulika kama baba wa demokrasia katika siasa za Afrika Mashariki, alilazimika kufichua siri ya mazungumzo baina yake na Rais Magufuli baada ya wahariri kutaka kujua kama alikutana na rafiki yake huyo na kuzungumzia joto la siasa za hapa nchini.
Katika majibu yake kuhusiana na swali hilo, Waziri Mkuu huyo wa zamani nchini Kenya, alikiri kukutana na Rais Magufuli Jumapili ya Agosti 14 mwaka huu Ikulu, Dar es Salaam na kula naye chakula cha jioni kisha kuzungumza mambo yao ya kirafiki na yale ya kisiasa lakini yasiyohusu urais.
“Jana mimi nimeongea na Rais yeye ameniclaim tofauti okey…amesema hajawanyamazisha wasiongee, anasema wanataka kufanya maandamano katika jimbo zile zingine ambazo hawana watu na kutaka kubeba watu kwa mabasi yeye alisema wakitaka hivyo wafanye kwao na si kubeba watu kutoka eneo hili kwenda eneo lingine, sasa sijui ukweli mimi maana mimi si Mtanzania.
“Anasema hajawakataza kama wakifanya eneo lao wanaweza kufanya lakini kubeba watu kutoka jimbo hili kwenda jimbo hili na mabasi kwenda kuleta vurugu ndio anasema amekataa,” alisema.
Alipoulizwa kama pengine Rais Magufuli amemweleza msimamo wake wa kupiga marufuku siasa za ushindani hadi mwaka 2020 pia ulilenga kuwazuia viongozi wakiwemo wale wa juu wa kitaifa wa vyama vya upinzani wasio na majimbo, Odinga alisema huku akimalizia na kicheko;
“Anasema hajakataa.”
Akisisitiza kile alichoelezwa na Rais Magufuli ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi, Odinga alizungumzia uhuru wa kutoa maoni akisema wapinzani kazi yao ni kupinga na si kushangilia na kwamba hiyo ndiyo demokrasia.
Alisema kutokana na kile alichomweleza Rais Magufuli, hadhani kama alikuwa na madhumuni ya kuwanyamazisha wapinzani.
Awali wakati akijibu swali hilo, Odinga ambaye miezi mitatu iliyopita alikuja nchini na kukutana na Rais Magufuli nyumbani kwake Chato, ziara ambayo ilizua gumzo hapa nchini na Kenya, alianza kwa kusifu kazi iliyofanywa na kiongozi huyo ya kusafisha hekalu lake pindi tu alipoingia madarakani Novemba mwaka jana.
“Kwanza nimshukuru sana Rais Magufuli kwa yale aliyofanya, tangu ashike hatamu ya utawala Tanzania kuna maendeleo mengi ambayo yamefanyika kwa mfano ile vita dhidi ya ufisadi, uzembe na kuleta nidhamu kwa upande wa kutoa huduma kwa wananchi.
“Sasa waliolala usiwaamshe (kicheko), lakini mimi sioni kama kuna shida kubwa, kama upande huo wapinzani wanatafuta relevance sasa kwa hivyo nilikuwa sitaki kujiingiza katika mambo ya ndani ya Tanzania,” alisema.
Wakati haya yakitokea sasa kwa takribani miezi mitano kumekuwa na vita baridi ya kisiasa kati ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Msingi wa vita yenyewe ni madai yanayotolewa na Ukawa, hususani Chadema kwamba Taifa limeporwa haki na demokrasia na Serikali inayotawala.
Kutokana na hilo hivi karibuni Chadema walitangaza kufanya mikutano na maandamano nchi nzima ifikapo Septemba mosi mwaka huu kupitia operesheni waliyoibatiza jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).
Hatua hiyo ya Chadema ilionekana wazi kumkera Rais Magufuli ambaye akiwa katika ziara ya chama chake mkoani Singida takribani wiki mbili zilizopita alikaririwa akisema yeye si mtu wa kujaribiwa na kwamba mwanasiasa atakayeandamana kinyume na maagizo yake atakiona cha mtema kuni.
Rais Magufuli alisema mtu pekee anayeweza kupita kila mahali ni yeye peke yake kwa sababu ni rais huku pia akiruhusu mikutano kwa wabunge wenye majimbo tu.
Juni mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kupiga marufuku mikutano ya siasa za ushindani hadi mwaka 2020, akiwataka watu kufanya kazi.
UKAWA WALIKOSEA KUSUSIA BUNGE
Akielezea mtazamo wake kuhusu uamuzi wa wabunge wa vyama vya upinzani wanaounda Ukawa kususia vikao wa Bunge kwa hoja ya kudai kunyimwa haki na kukandamizwa kidemokrasia, Odinga alisema uamuzi huo ni makosa makubwa kufanywa na wapinzani.
“Nafikiri ni makosa sana kususia Bunge, Bunge ni platform ambayo wapinzani wako nayo ya ku – engage Serikali, hapo ndio wewe unaweza ukasimama ukatoa maoni yako na maoni ya watu ambao unawawakilisha.”
Odinga pia alishangazwa na hoja ya wapinzani kuzira Bunge kama njia ya kumwondoa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.
Katika hilo alisema: “Eti humtaki Naibu Spika, Naibu Spika huchaguliwa na wabunge siyo? Hajachaguliwa yeye mwenyewe, hata kama wewe hutaki sura yake saa ile anayokuwa kwenye kiti… mimi nasema huo uamuzi ulikuwa ni kutoelewa nguvu na umuhimu wa Bunge,” alisisitiza Odinga.
Kauli hiyo ya Odinga imekuja wakati ambako Juni mwaka huu wabunge wa upinzani walitangaza kususia vikao vya bunge, ambapo mara hiyo waliamua kutohudhuria vikao vitakavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia.
Uamuzi huo waliuchukua kutokana na madai kwamba, Dk. Tulia mbali na kupelekwa kwa kazi maalumu ya kuwadhibiti lakini pia wanamtuhumu kwa kuendesha vikao vya Bunge pasipo kujali maoni yao.
LOWASSA MWANAFUNZI, AJE KWANGU
Katika mahojiano hayo, Odinga alipoulizwa alichojifunza katika harakati za kisiasa za Lowassa na hatua yake ya kuhamia upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema mwanasiasa huyo ni mwanafunzi kwake na akamtaka aende kujifunza.
Katika hilo, alisema: “Sio mimi nijifundishe, Lowassa ndiye anayeweza kujifundisha kwenye siasa zangu.
“Ndio anaanza sasa ni mwanafunzi anaweza kuja kwenye shule yangu (anacheka) tayari kujua yale ya kufanya maana yake najua democratization si kama kahawa, ‘instant coffee’ ambayo una brew una kunywa saa hiyo hiyo, it’s a process it takes a long time.”
Katika kuonyesha kuwa yeye ni Mwalimu kwa Lowassa, kiongozi huyo alirejea matukio kadhaa aliyokumbana nayo wakati akipambana kuingia Ikulu kupitia siasa za upinzani, ikiwemo kufungwa jela miaka tisa, kutofautiana na hata kuwa adui wa mtu aliyempigania kwa udi na uvumba hadi kuwa rais wa Kenya.
“Naangalia kule tulikoanza na bwana Moi (Daniel Arap Moi- Rais wa pili wa Kenya 1978 -2002) mwanzoni mwa mwaka 1994, maana yake mimi nakumbuka nimekaa gerezani miaka tisa, yaani mara tatu nimefungwa bila kushtakiwa.
“Mara ya kwanza nimekaa mwaka 1982, nikaachiwa kwa miezi sita, nikashikwa tena kwa zaidi ya mwaka mmoja, nikaachiwa nikashikwa tena, nikarudi tena kwa zaidi ya mwaka mmoja mpaka mara ya mwisho nimeachiwa mwaka 1991 eeeh!”
Alisema baada ya kuachiwa yeye na wenzake wakaanzisha chama cha upinzani cha Ford ambacho kilikuwa kina nguvu kubwa na kwamba kama wapinzani wangeamua kuungana wakati ule basi wangeshinda moja kwa moja katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1992.
“Kama kungekuwa hakuna hii migawanyiko ya wapinzani maana yake sisi tulipata kura asilimia 66, Moi alipata 34 lakini kwa sababu tulikuwa tumegawanyika tukashindwa.
“Mwaka 1997 tukasimama tena kwa hivi tulikuwa watu watano, Moi akapata 36 na sisi tukapata 64, Kibaki alikuwa namba mbili mimi tatu na Kibaki ndio ilikuwa shida ya Moi ndio sababu mwaka 2002 mimi nikasema Kibaki tosha nikaunganisha upinzani yote pamoja kuunga mkono bwana Kibaki.”
Katika hilo, Raila alisimulia jinsi Kibaki alivyopata ajali iliyomuacha mahututi huku yeye akibeba jukumu zito la kumfanyia kampeni.
“Alipata ajali ya gari akawa mahututi mimi ndio nikawa candidate nikamkampenia mpaka tukashinda, nilikuwa candidate dhidi yake huyu Uhuru ambaye Moi alimuweka kama karagosi,” alisema Odinga huku akiangua kicheko.
Katika safari yake hiyo ya kisiasa, Raila pia alisimulia jinsi walivyokuja kutofautiana na Kibaki licha ya kumpigania kwa nguvu zote na kuingia Ikulu.
“Sasa tulikuja kutofautiana juu ya mambo ya Katiba, wao walikuwa wanataka Katiba kama ile ya Tanzania, walitaka Rais awe na nguvu zaidi, yetu kama ile ya Ufaransa, walipokataa ndio tukaenda kwenye kura ya maoni, sisi tukawapinga na tukawashinda.
“Hapo ndio movement yetu ya chungwa ‘orange revolution’ ilipoanzia ambayo imekuja kumwangusha 2007, akakataa kukiri kushindwa alipokataa ndio nchi ikalipuka sasa yeye chama chake kilipata wabunge 43 changu zaidi ya wabunge 100, sasa ukiunganisha na wale watu wangu wote tulikuwa na wabunge zaidi ya 150, yeye alikuwa na 60 na kitu lakini mimi nilikuwa na yeye pamoja na hayo yote.
“Lakini kwa sababu ya ile fujo ilifanyika wakati ule hawa jamaa wakashtakiwa kule ICC sasa kwa sababu yeye mwenyewe jina lake lilitajwa akaamua kusaidia hawa watu kwa sababu walifanya yale ambayo walifanya ya kuiba kura, kwa hiyo sisi tumekuwa na uzoefu wa kutosha, akina Lowassa wanaweza kuja kwa shule,” alisema Raila.