28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

KOREA KASKAZINI: TUITAZAMISHA MELI YA MAREKANI

SEOUL, KOREA KUSINI


KOREA KASKAZINI jana imesema itaonesha uwezo wake mkubwa wa kijeshi kwa kuizamisha meli ya kubebea ndege za kivita ya Marekani iliyo njiani kuelekea rasi ya Korea.

Kauli hiyo imekuja baada ya meli mbili za japani kuungana na ya Marekani kwa mazoezi ya kivita magharibi mwa Bahari ya Pasifiki.

Rais wa Marekani, Donald Trump aliamuru meli hiyo USS Carl Vinson kuelekea katika rasi hiyo kufuatia majaribio ya makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini na tishio la shambulio dhidi ya Marekani na washirika wake wa Asia.

Marekani haijataja eneo hasa ambalo meli hiyo imefika, lakini Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence alisema itawasili ndani ya siku chache bila kufafanua.

“Majeshi yetu ya mapinduzi yamejiandaa kuizamisha meli inayotumia nguvu za nyuklia ya Marekani kwa pigo moja,” Rodong Sinmun, gazeti la chama tawala cha Wafanyakazi nchini humo lilisema.

Gazeti hilo liliifananisha meli hiyo na ‘mnyama mchafu’ na kwamba pigo hilo litaonesha mfano halisi wa uwezo wa kijeshi wa Korea Kaskazini.

Katika kinachoonekana ongezeko la mgogoro baina ya pande hizo mbili, Korea Kaskazini imemkamata mtu mwenye asili ya Marekani na Korea na kufanya idadi ya Wamarekani wanaoshikiliwa mjini Pyongyang kufikia watatu.

Mtu huyo aliyejulikana kwa jina moja la Kim, amekuwa nchini humo kwa mwezi moja kwa shughuli za hisani, shirika la habari la Yonhap limesema.

Alikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Pyongyang wakati akijiandaa kuondoka humo.

Taifa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 85 ya kuwekwa msingi wa jeshi lake la watu wa Korea kesho.

Huko nyuma maadhimisho muhimu kama hayo yamekuwa yakiendana na majaribio ya silaha.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles