24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Kinondoni yalenga kusaidia wanawake zaidi kiuchumi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe amesema wamejipanga kuendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwataka maofisa maendeleo ya jamii kusimamia uundwaji vikundi vya wanawake na kuvijengea uwezo.

Amesema manispaa hiyo inazo fedha za kutosha kuwakopesha wanawake na wanachosubiri ni maelekezo ya Serikali ya namna bora ya kutoa mikopo hiyo.

Ameyasema hayo Machi 13,2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake ambayo kiwilaya iliadhimishwa katika viwanja vya CCM Mwinyjuma vilivyopo Mwananyamala.

Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Stella Msofe (katikati) akimsikikiza mjasiriamali Grace Msimbe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake ambayo kiwilaya iliadhimishwa katika viwanja vya CCM Mwinjuma Mwananyamala.

“Manispaa fedha zipo tunasubiri tu maelekezo ya viongozi wakuu namna gani bora ya kuzikopesha kwahiyo tuendelee kuunda vikundi na maofisa maendeleo ya jamii mvisimamie viwe vyenye tija.

“Tusiache vikaundwa halafu mwisho wa siku tunawaambia hawana sifa, tunawakatisha tamaa…tuwajengee uwezo,” amesema Msofe.

Kuhusu Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake 2024 ambayo inasema; Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii amesema watahakikisha wanaithibitisha kwa vitendo.

Katibu Tawala huyo pia amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Naye Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amewataka wanawake kuendelea kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha maendeleo ya wilaya hiyo na Tanzania nzima.

“Wanawake hamna sababu ya kurudi nyuma, palipo na mwanamke pana matokeo chanya na maendeleo makubwa. Nimefanya kazi na mkurugenzi mmoja tu mwanamume lakini wote walikuwa wanawake, lile ambalo tunakubaliana ndilo linalofanyika na wanalofuatilia linaonekana,” amesema Mnyonge.

Akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa wilaya hiyo, Mwekahazina wa Chama cha Wajane Wilaya ya Kinondoni, Husna Kanoga, amesema wamehamasika kuunda vikundi vya kiuchumi na kijamii 185 na tayari wanawake 332 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji miradi.

Amesema pia wameunda jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi ambalo mpaka sasa lina vikundi 127.

Hata hivyo amesema mikopo inayotolewa bado haitoshelezi kwa kuwa mahitaji ni makubwa na baadhi ya wakopaji kutorejesha kwa wakati.

Mojawapo ya kikundi cha Vijimambo kutoka Kata ya Kigogo kimenufaika kwa kupata mkopo wa Sh milioni 10 hatua iliyokiwezesha kuvuka kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Mwakilishi wa kikundi hicho Grace Msimbe, amesema walianza kukopa Sh milioni 3.5 kisha Sh milioni 6 na sasa wana mkopo wa Sh milioni 10 ambao wako kwenye hatua za mwisho za kumalizia kulipa.

“Tulikuwa hatuna mashine lakini kupitia mkopo wa manispaa tumeweza kununua na kuboresha bidhaa zetu za virutubisho vya vyakula na tiba lishe na pia tumeweza kutoa ajira kwa watu wengine,” amesema Msimbe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles