24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KINGOLWIRA: SHULE YA MSINGI ILIYOGEUZWA GESTI, UWANJA WA WACHAWI

Na Ashura Kazinja, Morogoro

SHULE ya Msingi Kingolwira ni miongoni mwa shule mbili za serikali katika Kata ya Kingolwira Mtaa wa Mwembe Msafa Manispaa ya Morogoro. Shule hii ina jumla ya wanafunzi 1,461 ambapo kati yao wasichana ni  737 na wavulana 724.

Kingolwira ilianzishwa rasmi mwaka 1952 ikiwa katika Wilaya ya Morogoro Vijijini, lakini baada ya habari za mipango miji mwaka 1993 kuongeza maeneo, shule hiyo ikaingia katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mwaka 1995.

Awali shule hii ilikuwa na walimu 30 lakini baada ya mmoja wao kukutwa na kashfa ya vyeti feki sasa wamebaki 29.

Akiizungumzia shule hiyo, Mwalimu Mkuu, Jimmy Katabaruki anasema inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ufinyu wa madarasa ambayo yapo 13 wakati uhitaji ni madarasa 33.

Hii ni kwa sababu kata hii ina shule mbili za msingi ambapo nyingine ni Shule ya Msingi Mwenge huku kata ikiwa na mitaa nane.
Anaeleza kuwa zoezi la elimu bure limechangia idadi ya wanafunzi kuongezeka maradufu ukilinganisha na awali ambapo walikuwa wachache kutokana na kuandikishwa kwa fedha.

Anasema elimu bure imesaidia hata wazazi ambao hawakuwa na mwamko wa kusomesha kulazimika kuwapeleka shule watoto wao kwa kuogopa sheria na taratibu zilipo sasa.

“Mbaya zaidi asili ya watu wa huku hawapendi shule, lakini kutokana na elimu kuwa bure, wanafunzi wamekuwa wengi. Kwa mwaka tunaweza kusajili wanafunzi hata 500 kwa kuwa wazazi wanaogopa kukaa na watoto kukwepa kukabiliwa na mkono wa sheria,” anasema mkuu wa shule.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni kukosekana kwa uzio wa shule, hali inayosababisha wakazi wanaoishi kuzunguka eneo la shule kuvamia na kujenga makazi, hivyo wameamua kupanda miti badala ya uzio ili kupunguza ukubwa wa tatizo.

Anasema ufahamu wa wazazi na walezi  juu ya umuhimu wa shule kwa watoto ulikuwa duni, hivyo

kushindwa kuwasimamia  kuhudhuria masomo.

Anasema idadi kubwa ya wanafunzi ni watoro hali inayowafanya wasimudu kusoma na kuandika.

“Kutengana kwa wazazi nako kumechangia watoto wengi kujiingiza kwenye tabia mbaya, hii ni kwa sababu wanakosa uangalizi mzuri wa wazazi  na walezi kushindwa kuwachukulia hatua wanamume wanao  watorosha mabinti pindi wanapo wabaini,” anasema.
Anasema kuwa mbali na changamoto hizo, pia shule hiyo inaandamwa na mambo ya kishirikina.

“Walinzi huwa wanashuhudia vitendo hivyo nyakati za usiku ingawa Serikali haiamini mambo hayo.

“Baadhi ya wazazi nao wamekuwa wakifanya makusudi kutumia ushirikina kuwaharibu watoto wao akili ili wasisome na hivyo kuwa rahisi kwao kukwepa  mkono wa Serikali.

“Wanafunzi tunaowategemea darasani kwamba ndio wenye akili za kuwaongoza wenzao huwa wanakumbwa na mapepo na hivyo kushindwa kabisa kuhudhuria shuleni,” anasema mkuu huyo wa shule.

Anaongeza: “Hivi ninavyoongea kuna baadhi ya wanafunzi tunataka tuwakabidhi kwa wazazi wao kwanza ili wakawatibie na wakipata nafuu watarudi.

“Kwa sababu wanafunzi hawa wanapopandisha mashetani huanza kupiga wenzao na kukimbia ovyo na hivyo kuwafanya wanafunzi wengine kusoma kwa hofu.”

Mwalimu Katabaruki anasema kuwa kuna baadhi ya wazazi kwa sababu zao binafsi hawataki kabisa watoto wao kuombewa pindi wanapoanguka shuleni.

“Kwa sababu hiyo, huwa wakianguka tunaogopa kuwafanyia maombi hivyo huwa tuwaita wazazi wao kuja kuwachukua.
“Hapa shule kuna mti wa siku nyingi mno ambao wenyeji wanautumia kucheza ngoma na una vitu vyao, tulitaka kuukata wakakataa, sasa mti kama huo katika eneo la shule hauwezi kukwepa kutokea mauza uza,” anasema.

Mwalimu Katabaruki anasema mbali na hayo shule hiyo pia imegeuzwa nyumba ya kulala wageni.

Anasema hii ni kwa sababu shule haina umeme, hivyo nyakati za usiku eneo linakuwa giza na kutoa mpenyo kwa watu kutumia madarasa kufanya matendo maovu, hasa ukizingatia kuwa baadhi ya madarasa hayana milango.

“wameifanya hii shule ni nyumba ya kulala wageni (guest), wanatuharibia madawati kwa kuyageuza vitanda, wakati mwingine ukija asubuhi unakuta madawati yamevunjwa,” anasema Mwalimu Katabaruki.

Anasema kuwa vyoo navyo ni tatizo shuleni hapo kwani vilivyopo havifai kutumiwa ni idadi kubwa ya watoto kwa kuwa vimetengenezwa kwa mtindo wa kisasa.

Anasema vyoo hivyo vilivyojengwa kwa udhamini wa watu wa Japan ni vya kuflash hivyo huhitaji maji mengi kwa ajili ya kuflashi na kuvifanyia usafi wa mara kwa mara.

“Jambo hili ni tatizo kwetu kwani shule haina maji hivyo tunashindwa kuvitumia,” anasema.

Naye Mdhibiti wa Ubora wa Shule Wilaya, Mbuke Dittu anasema wamemshauri mwalimu mkuu, kamati ya shule na mkurugenzi kujenga uzio shuleni hapo ili kuweka mazingira salama na rafiki kwa wanafunzi kusoma vizuri na kuzuia watu kuingia kiholela.

Kwa upande wake mzazi wa mwanafunzi anayesoma shuleni hapo, Kosta Mloka anasema mti uliopo shuleni hapo unatumika hasa kipindi cha kiangazi kuendeshea shughuli za kimila na desturi hasa kwa wasichana waliofikia hatua ya kubalehe na kuitwa mama.

Anasema watu huwa wanakusanyika nyakati za jioni na kwamba watu wengi huwa wanashiriki ngoma hizo kwa kuwa ni sehemu ya kudumisha mila zao.

Naye Susan Jumbe anasema vitendo vya kishirikina vimezidi katika eneo hilo si jambo la kushangaza watoto kukumbwa na mapepo na wengine kufanywa wehu.

“Ni kweli kabisa vitendo vya kishirikina hapa vipo, kuna baadhi ya watoto wetu wanasoma kwa shida mno, maana akiwa nyumbani mzima lakini akifika shule unaambiwa mwanao kaanguka mapepo, na wengine mpaka wanapiga wenzao hali ambayo ni hatari,” anasema Susan.

Diwani wa Kata  ya Kingolwira, Bidyanguza Steven anasema kuna umuhimu wa shule hiyo kuwa na walinzi wa kutosha ili kuwadhibiti watu wanaiogeuza kuwa nyumba ya kulala wageni na kufikia hatua ya kuvunja madawati.

“Hii pia itawadhibiti wahalifu hawa ambao hata milango ikifungwa na kufuli huwa wanavunja na hivyo kusababisha uharibifu na upotevu wa mali za shule,” anashauri.

Akizungumzia kuhusu mambo ya ushirikina anasema kuwa ni mengi kwani wakati mwingine inapofika usiku miti huota yenyewe katika kiwanja cha shule na inapofika alfajiri hupotea yenyewe.

Kuhusu mahudhurio shuleni, Mjumbe Kamati ya shule hiyo Banzi Lucas anawaomba wazazi kuhudhuria vikao ili kuweza kujua maendeleo ya watoto wao.

Ofisa elimu Kata ya Kingolwira, Regina Massawe anasema suala hilo kwa sasa limepungua baada ya kuweka mlinzi tofauti na awali ambapo vitendo hivyo vilikithiri zaidi.
Hata hivyo ili kujua adha wanazokumbana nazo wanafunzi na walimu shuleni, ni vema Serikali sasa kuanza kuzitembelea shule mara kwa mara hasa zile zilizopo katika maeneo ya barabara kuu ili kuweza kubaini changamoto hizo.
Tunashuhudia kuwa maofisa wengi wa elimu hawana desturi ya kuzungukia shule zao hali inayochangia kutofahamu adha wanazokabiliana nazo.

Kama watajenga utamaduni huo itakuwa rahisi kutatua matatizo haraka iwezekanavyo na si mpaka madhara yanapotokea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles