22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

KINANA AMPA TANO JPM KUKOSOA AWAMU ZILIZOPITA

Na Waandishi Wetu

-MUHEZA/DAR

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewataka wananchi kuacha kulalamikia utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli kwa sasa anasahihisha makosa ya awamu zilizopita   chini ya CCM.

Kauli hiyo aliitoa jana wilayani Muheza mkoani Tanga kwenye mkutano.

Alisema hivi sasa kuna baadhi ya watu wakiwamo wana CCM wamekuwa wakilalamikia hatua ya Rais Dk. John Magufuli kuwa mkali na namna anavyosahihisha mambo yaliyopo serikalini.

Alisema hatua hiyo inayofanywa na Rais Magufuli anaiunga mkono kwa sababu  anachofanya ni kusahihisha na hakuna dhambi kufanya hivyo.

“Wapo watu wanalalamika kuwa Rais amekuwa mkali na anakosoa serikali zilizopita kwa vile  akifanya hivyo kuna dhambi gani?

Serikali zilizopita zilikuwa ni za CCM na iliyopo madarakani ni CCM hivyo sioni ajabu kama Rais Magufuli anafanya mabadiliko kwa vile  ni nzuri ya kusafisha na kuleta mabadiliko hivyo si dhambi,” alisema Kinana.

Katibu Mkuu huyo wa CCM ambaye kwa siku kadhaa alikuwa hajaonekana hadharani, alisema kwa sasa wananchi wanahitaji maendeleo   mambo yao yaweze kwenda haraka badala ya kucheleweshwa kwa uamuzi ambao unahitaji uharaka kwa masilahi yao.

“Najua mlichoka kusubiri mambo yanayohitaji uamuzi wa haraka kuchukua muda kufanya uamuzi lakini Rais huyu yeye katika masuala yenye masilahi huwa anachukua uamuzi wa haraka kwa ajili ya masilahi ya wananchi waliojiona wanyonge,” alisema.

Akizungumzia uamuzi wa Serikali kuyafutia hati mashamba yasiyoendelezwa, alisema hatua hiyo ni mkombozi kwa wananchi waliokuwa wakilima mashamba hayo.

“Mheshimiwa Rais wapo watu walikuwa wakimiliki mashamba ambayo wameshindwa kuyaendeleza na kugeuka mapori na wanapokwenda kulima wanafukuzwa na hata mazao yao kuharibiwa,” alisema Kinana.

Alisema baada ya Rais Dk. Magufuli kuona kero hiyo ndipo alipoamua kuyachukua, sasa wanapiga kelele kuwa wanaonewa na kusema rais anavunja utaratibu wakati walikuwa wameyatelekeza bila kuyaendeleza.

“Rais ameamua kuchukua ardhi yake, oooh mnasema anavunja utaratibu, sasa ni utaratibu upi uliovunjwa wakati mmeshindwa kuyaendeleza,” alisema.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Rais Dk. John Magufuli alisema hatajali mtu wala mali yake katika kutetea haki na masilahi ya Watanzania wanyonge, ndiyo maana analazimika kufanya uamuzi mgumu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Alisema   awali rasilimali za nchi hii zilikuwa zinamilikiwa na watu wachache ambao walisababisha mpaka kukihodhi chama na serikali   lakini sasa atahakikisha watu hao hawapo tena.

Rais alisema katika utawala wake hataruhusu watu au wawekezaji wanaomilikia maeneo makubwa ya ardhi na kushindwa kuyaendeleza bali atahakikisha anayatwaa na kuyagawa kwa wananchi.

Alisema katika utawala wake tayari ameshafuta hati za mashamba matano makubwa ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza na kuacha mapori.

“Tumefanywa wajinga …  watu wanachukua maeneo yetu halafu wanakwenda kukopa mikopo katika  benki za nje huku sisi wanatuachia mapori matupu ambayo wameshindwa kuyaendeleza,” alisema.

Akizungumzia shamba la katani linalomilikiwa na mwekezaji Chavda lililopo wilayani Korogwe alisema notisi ya siku 90 aliyopewa imekwisha na anachosubiri ni kupelekewa taarifa mezani kwake.

  Awapoka ardh iJKT

Akiwa Mkata wilayani Handeni, Rais Dk. Magufuli, alitangaza uamuzi wa kukinyang’anya ardhi Kikosi cha Jeshi cha 835 KJ Kabuku kwa kukitaka kurudisha ekari 50 kwa Serikali ya Kijiji baada ya kushindwa kuiendeleza kwa miaka saba.

“Naomba leo (jana) mkitoka hapa nendeni kwenye Serikali ya Kijiji na mrudishe eneo mlilolichukuwa kwa sababu  hamna uwezo wa kuliendeleza na mlirudishe   wananchi waweze kulifanyia kazi,” alisema.

Alisema wananchi hao walipewa eneo hilo kwa ajili ya kujenga kiwanda lakini hadi sasa halijaendelezwa.

Aliwataka kujenga kwenye maeneo yao ya jeshi kwa sababu  bado yana nafasi kubwa.

“Tumieni maeneo yenu   kujenga kiwanda, mna maeneo makubwa ambayo mnalima mahindi na machungwa.

“Kwa nini msiyatumie hayo badala ya kuendelea kuchukua maeneo ya wananchi?” alisema Rais Dk. Magufuli.

Uchunguzi mil. 500/-

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli ametoa siku 15 kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kuunda tume   kufanya uchunguzi wa Sh milioni 500 zilizopelekwa wilayani Handeni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya.

Alisema fedha hizo zinaonekana zina shaka badala ya kufanya kazi ya ujenzi zimeenda kuwafaidisha watu wachache ambao aliahidi kuwashughulikia.

“Nakuagiza mkuu wa wilaya ufuatilie hilo asiponyoke mtu yeyote.  Katika hilo na kila aliyehusika ajipeleke mwenyewe gerezani lakini nitahakikisha ninawashughulikia kwa sababu  fedha za wananchi hazipotei bure,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles