31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

MAHAKAMA: KIGOGO IPTL ATATIBIWA LUGALO, AMANA

NA KULWA MZEE- DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema mshtakiwa Harbinder Singh Sethi atatibiwa  Hospitali ya Amana au Hospitali ya Rufaa ya  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  Lugalo.

Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai.

Wakili Swai alikiri kuwapo amri ya mahakama ya kuamuru mshtakiwa kupatiwa matibabu.

“Mheshimiwa hakimu, hakuna ushahidi  mshtakiwa alipokamatwa alikuwa anakwenda Afrika Kusini kutibiwa.

“Suala la mshtakiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu bado si sahihi, kwa sababu utaratibu wa mgonjwa kupelekwa nje unafahamika….haendi kwa sababu ya amri ya mahakama,”alidai Swai.

Alipinga Sethi kutibiwa nje ya nchi kwa sababu madaktari wa hapa nchini, hawajasema wameshindwa na hakuna uthibitisho wa kushindwa.

Hata hivyo, Swai alidai hakuna utaratibu wa mgonjwa kupelekwa Muhimbili moja kwa moja, utaratibu mgonjwa anatakiwa kuanzia Hospitali ya Amana ama Lugalo wao ndiyo watafanya utaratibu wa kumpa rufaa kwenda kutibiwa Hospitali ya Muhimbili.

Alidai Magereza ambako Sethi anatibiwa, ndiyo wametakiwa kuthibitisha na kufanya utaratibu apelekwe Hospitali ya Amana .

Kuhusu ombi la Wakili wa Sethi,Alex Balomi kuomba kesi itajwe ndani ya siku saba kwa ajili ya kuangalia kama amepelekwa hospitali, Swai aliomba ipangwe ndani ya siku 14.

“Kesi kutajwa ndani ya siku saba ni kumsumbua mgonjwa, muda huo autumie kwenda hospitali na siyo mahakamani, naomba ipangwe ndani ya siku 14 kama utaratibu ulivyo,”alidai Swai..

 

Alidai ndani ya muda huo, atakuwa amefikishwa Hospitali ya Amana ama Lugalo kupatiwa matibabu na utaratibu wa magereza umekamilika na wao watasimamia.

Wakili Balomi, alidai hadi sasa mteja wake hajapelekwa hospitali na kuomba mahakama isimamie amri yake ya mshtakiwa kupatiwa matibabu.

Hakimu Shaidi katika uamuzi wake, alisema hajasema mshtakiwa apelekwe kutibiwa nje ya nchi, atibiwe nchini.

Pia aliwapa siku 14 Takukuru kama walivyoomba awali  ili kuangalia kama atakuwa amefikishwa hospitali zilizotajwa kupatiwa matibabu. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti17, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Washtakiwa hao katika shtaka la kwanza, wanadaiwa Rugemarila  ambaye ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa    kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19 , 2014 Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya  kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la pili la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao kati ya Oktoba 18,2011 na Machi 19,2014 Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma na watumishi wa umma  walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Kwa upande shtaka la tatu, Sethi  anadaiwa   Oktoba 10,2011 katika mtaa wa Ohio Ilala,Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 a ya usajili wa makampuni  na kuonesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki, wakati akijua ni uongo.

Seth katika shtaka la nne anadaiwa kutoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 ya usajili wa kampuni kwa ofisa msajiri wa kampuni, Seka Kasera kwa njia ya kuonesha kwamba yeye ni Mtanzania na Mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka la tano, washtakiwa wote, wanadaiwa kuwa kati ya  Novemba 28/29, 2011 na Januari 23,2014 makao makuu Benki ya Stanbic kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi St. Joseph  kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani 22,198,544.60 na Tsh 309, 461,300,158.27.

Katika shtaka sita la kusababisha hasara,  washtakiwa hao wanadaiwa kuwa   Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati Kinondoni kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Katika la saba, kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300.27 wakati wakijua fedha hizo zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka la nane, wanadaiwa Novemba 29,2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania Wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua BOT Dola za Marekani 22,198,544.60 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la tisa, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh 309,461,300,158.27 kutoka BOT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Shtaka ya kumi,  inadaiwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemarila  alitakatisha fedha, Sh 73,573, 500,000 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Kwa upande wa shtaka la 11, inadaiwa kuwa Januari 23,2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemarila alitakatisha fedha Dola za Marekani 22,000,000 kutoka kwa Seth wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Shtaka la 12, Seth anadaiwa Januari 28,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Wilaya ya Kinondoni alihamisha Rand 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika benki ya Standard Bank Land Rover Sandton Johannesburg, wakati akijua katika kipindi anahamisha fedha hizo zimetokana na zao la kujihusha na genge la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles