24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA SHEIKH KHALIFA YANUSURIKA KULIPULIWA

NA ASHA BANI

FAMILI ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, imekumbwa na hofu baada ya kushindwa kwa jaribio la kutaka kulipua nyumba yake, lililofanywa na watu wasiojulikana.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Lalago eneo la Magomeni Makanya jijini Dar es Salaam, ambapo watu hao walifanya jaribio hilo kwa kutumia bomo la petroli.

Taarifa za tukio hilo lililozua taharuki zilianza kuzagaa jana asubuhi kuwa nyumba ya sheikh huyo imerushiwa mabomu na watu wasiojulikana na hivyo kusababisha madhara ikiwa ni pamoja na gari lake kuunguzwa.

Baada ya taarifa hiyo Jeshi la Polisi lilifika nyumbani hapo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuzungusha utepe wa kuashiria hali ya hatari katika eneo hilo.

Baadhi ya majirani wa sheikh huyo walilieleza MTANZANIA kuwa usiku wa kuamkia jana walisikia mlio mkubwa mithili ya bomu lililolipuka katika nyumba hiyo.

“Mimi nilisikia mlio mdogo na wala sikuhisi kama unaweza kuwa  ni bomu, hadi nilipoamka asubuhi na kupata taarifa kuwa kuna watu walitaka kulipua nyumba ya sheikh,” alisema Aisha Shabani.

Mkazi mwingine wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Kassim, alisema hakusikia mlio wowote hadi alipoona Jeshi la Polisi asubuhi wakiwa wamezingira nyumba hiyo, huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa katika mtaa huo .

MTANZANIA ilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Muliro Jumanne Muliro ambaye alisema mapema jana asubuhi askari wake walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuchunguza na kwamba uchunguzi huo bado unaendelea.

Alisema kuhusu kama ni bomu au laa ni hisia za watu na hisia za kiongozi huyo wa dini kuwaza namna hiyo, lakini jibu sahihi litajulikana baada ya kukamilika kwa uchunguzi na taarifa itatolewa.

Alipoulizwa  kuhusu taarifa kuwa eneo hilo limeshambuliwa kwa bomu alisema walichokiona wao ni gari aina ya Toyota Mark II lenye namba T 180 BGQ likiwa limeungua sehemu ya nyuma na si vinginevyo.

 

 

“Uchunguzi wa awali unaonesha ni buti la gari ndilo ambalo limeungua, lakini bado tunafuatilia kufahamu limeungua na nini.

“Hata hivyo si jambo la ajabu au geni kuungua kwa gari kwani hata wewe gari lako linaweza kuungua muda wowote hata huko barabarani magari yanaungua si ajabu.

“Gari ni la binadamu na yeye sheikh ni binadamu pia hivyo si ajabu kuungua kwa gari hilo,” alisema Kamanda Muliro na kuongeza.

“Hizo za kwamba ni bomu ni hisia zake huwa hatuchukulii au kupelekwa na kuamini jambo kwa hisia, niliingia ndani tumemuhoji na kuachana naye humo humo ila upelelezi unaendelea,” alisema.

Sheikh anena

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake jana Sheikh Khalifa, alisema tukio hilo lilitokea saa nane usiku akiwa anaandika masuala yake ya kikazi, ambapo alishituliwa na kishindo cha kitu kizito kikiwa kimeanguka.

Alisema baada ya kishindo hicho alijaribu kuangalia kwa kutumia kamera maalumu za ulinzi (CCTV) na hakuona chochote.

“Baada ya dakika tano mke wangu nilimsikia anamuamsha kijana ambaye tuanaishi naye hapa, akimwambia kuna moto unawaka nje, tulipojaribu kutoka tulishindwa kwenda getini kutokana na mota mkubwa uliokuwa umetanda” alisema.

Alisema baada ya kelele majirani walisogea na kuanza kuzima moto huo na wao kufanikiwa kutoka kushirikiana na majirani kuuzima moto huo.

“Tulikuta dumu kubwa la lita 20 ambalo lilifunikwa nguo na dogo kama la lita tano hivi yanayoonekana yalikuwa na petroli, lile kubwa lilikuwa tayari limewaka moto mkubwa ambao ulianza kuunguza gari (Toyota Mark II)” alisema.

Aliongeza kuwa watu hao walijaribu kuwasha moto huo wakiwa umbali wa karibu mita 40 kwa kutumia tambi ambazo zilizima na kushindwa kufika eneo lililokusudiwa na ndipo wakaamua kusogea getini na kuwasha moto huo.

Alisema waliona gari lililokuwa likitumiwa na watu hao kwa kutumia kamera japo hawakufanikiwa kulitambua kutokana na ukuta wa nyumba hiyo kuzuia.

Hisia zilizopo 

Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wake, baadhi ya watu wanahusisha tukio hilo na matukio mbalimbali ambayo yamemkabili sheikh huyo, ikiwa ni pamoja na tukio la kumhusisha na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Mwezi uliopita Sheikh Khalifa aliitwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kuhojiwa kwa siku tatu mfululizo kutokana na madai kuwa alitoa kauli za kichochezi alipozungumza na vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Sheikh Khalifa, alihojiwa kuhusu matamshi yake ya kuunga mkono kauli ya Lowassa, alipoitaka Serikali kuharakisha upelelezi wa kesi ya ugaidi inayowakabili masheikh wa Uamsho, ili kama hawana hatia waachiwe huru.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari sheikh Khalifa alisema. “Tunaiomba Serikali iweke wazi kwanini hairuhusiwi kwa sheikh au mtu yeyote aliyewekwa ndani gerezani kuonwa na zaidi ya mtu mmoja au siku 14 zipite ,yaani akija mkewe au ndugu yake kumwona hayo mambo hayapo kabisa,” alisema.

Pia wapo baadhi ya watu wanaohusisha tukio hilo na mgogoro wa Msikiti wa Ndugumbi, ambapo sheikh huyo anadaiwa kuwa karibu na uongozi wa bodi ya wadhamini ya msikiti huo ambao unapingwa na kikundi cha baadhi ya waumini msikitini hapo.

Hata hivyo watu wengine wanadai dhana hiyo haina nguvu kutokana na kwamba sheikh huyo si kiongozi katika msikiti na wala hapendelei kufanya ibada katika msikiti huo ambao siku za hivi karibuni umekuwa na mzozo wa kugombea madaraka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles