24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

MDEE: BILA DEMOKRASIA UCHUMI UTAENDELEA KUYUMBA

Na MARGRETH MWANGAMBAKU- TUDARCO

WAZIRI Kivuli wa Wizara ya Fedha na Mipango, Halima Mdee, amesema bila uwepo wa demokrasia na utawala wa kisheria nchini, uchumi utaendelea kuyumba.

Kutokana na hilo, ameitaka Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi au Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Msemaji wa Serikali, watoe majibu kwanini chakula kinapatikana kwa gharama kubwa.

Kauli hiyo ya Mdee imekuja siku moja baada ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, kueleza kuwa hali ya uchumi nchini iko sawa na uchumi umekua na kufikia asilimia saba, tangu Rais Dk. John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015.

Dk. Abbasi alikuwa akijibu tamko la Chadema kupitia Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, aliyesema uchumi unayumba na kuitaka Serikali kuwa na mpango wa muda mfupi wa kufufua uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema alichosema Dk. Abbas hakieleweki kwa sababu hakujibu hoja.

“Tunaitaka Serikali itambue kuwa, wakati wa maneno maneno umepitwa na wakati na waelewe bila uwepo wa demokrasia na utawala wa kisheria, uchumi utaendelea kuyumba.

“Wakati huu kama ulikuwa unakunywa bia mbili, unakunywa moja au usinywe kabisa, lakini linapokuja suala la chakula, lazima ule.

“Tunaitaka Serikali ijibu hoja zetu ambazo zimetokana na taarifa ya BoT, kuwa uchumi wetu unayumba au unaporomoka ukilinganisha na miaka iliyopita.

“Dk. Abbasi alipotosha takwimu hasa aliposema uchumi wa dunia ulikua kwa asilimia 3.5 mwaka 2015 na kunukuu taarifa ya Gavana wa BoT.

“Dk. Abbasi alilitumia tamko la sera ya fedha ya mwaka 2016/17 lililotolewa na BoT Februari mwaka huu ambalo lilitathmini mwenendo wa utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi cha nusu mwaka wa kwanza wa fedha.

“Ukweli ni kwamba, uchumi wa dunia ulikua kwa wastani wa asilimia 3.1 mwaka 2016, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.2 mwaka 2015.

“Sasa basi, msemaji wa Serikali alitoa wapi takwimu za ukuaji wa asilimia 3.5 za mwaka 2015,”alihoji Mdee.

Kwa mujibu wa Mdee, msemaji huyo wa Serikali alipotosha umma kwa makusudi aliposema Tanzania ni ya kwanza Afrika Mashariki kwa kuvutia wawekezaji kwani taarifa ya uwekezaji Afrika iliyotolewa na Quantum Global Research Lab ya Uingereza ya Mei mwaka huu, inaonyesha Tanzania si ya kwanza bali ni ya pili baada ya Kenya.

“Kwa upande wa kilimo, alisema katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli malengo ni kukua kwa asilimia sita, lakini kimeporomoka na kufikia asilimia moja.

“Kwa tafasiri nyingine, Serikali si rafiki kwa wakulima, wavuvi na wafugaji. Tukisema Serikali hii si rafiki na inawachukia wafugaji, wakulima na wavuvi, wanasema sisi ni wachochezi.

“Tuko katika nchi ambayo Serikali inashindana na wananchi, wafanyabishara na wafanyakazi kukopa katika mabenki na kwa vyovyote vile, Serikali itakuwa na kipaumbele, yaani tuko katika hali mbaya kiuchumi,” alisema Mdee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles