25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

AGIZO LA JPM LAKWAMISHWA

Na Waandishi Wetu, DAR/Mikoani


AGIZO la Rais Dk. John Magufuli kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta nchini kuhakikisha ifikapo Julai 31, mwaka huu wawe wamefunga mashine za kukusanya kodi kwa kutumia mfumo wa kieletroniki (EFD’s), limegongwa mwamba baada ya mashine hizo kuadimika kwa mawakala.

Dk. Magufuli alitoa agizo hilo Julai 19, mwaka huu wakati wa ufunguzi wa barabara ya Kigoma-Biharamulo-Lusahunga  kwa kuwapa siku 14 wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini, kuhakikisha wanaweka na kutumia mashine za EFD na atakayekiuka atafutiwa leseni ya biashara yake.

Alimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuhakikisha wanafuatilia maagizo hayo.

“Wanaolalamika kukosa mafuta waendelee kufanya hivyo, ni mara mia tukose mafuta kuliko kuwa na wafanyabiashara wanaokwepa kodi, hivyo ninatoa siku kumi na nne, wakishindwa wafutiwe leseni,” alisema Rais Magufuli.

 

ARUSHA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha, Apili Mbaruku, alisema baada ya wakala wa kusambaza mashine hizo kupungukiwa, wamelazimika kuingia makubaliano maalumu na wafanyabiashara wenye vituo hivyo, ili kuwawezesha kuendelea na biashara.

Alisema makubaliano ya mkataba huo yamelenga wafanyabiashara waliokuwa wamelipia katika kipindi kilichopangwa na kujikuta wamekwama kupatiwa mashine hizo na wasambazaji.

“Mkataba huu tunasainishana na wenye vituo vya kuuzia mafuta na umewalenga wale waliokuwa tayari wamelipia lakini hawajapatiwa EFD’s. Kwa wale ambao hawakuwa wamenunua hadi kipindi kilichotolewa kinamalizika, hao tumewafungia hadi sasa,” alisema Mbaruku na kuongeza:

“Kwa sasa tunaanda taarifa ya Mkoa wa Arusha tutakayoipeleka makao makuu jijini Dar es Salaam… Hadi jana wateja 13 ndio walikuwa wamesaini makubaliano hayo yanayowawezesha kuendelea kusubiria mashine hizo huku wakiuza.”

MTANZANIA lilifanikiwa kutembelea baadhi ya vituo vilivyopo jijini Arusha, vikiwamo vya Manji’s kilichopo katikati ya jiji, Mount Meru vilivypo katika maeneo tofauti ya Jiji la Arusha na nje ya mji vikiwa tayari vimefungwa mashine za EFD’s.

 

IRINGA

Wamiliki wa vituo vya mafuta mkoani Iringa wamesema wanashangazwa na hatua ya kukosa mashine hizo licha ya kuzilipia kama walivyotakiwa na Serikali.

Wakizungumza na MTANZANIA, wawakilishi wa vituo vya TFA na Lake Oil vilivyopo mjini Iringa, walisema kuwa wao walikwishalipia kupitia moja kati ya makampuni ambayo walitambulishwa na TRA kuwa ndio wauzaji, lakini hadi kufikia siku ya mwisho hawajafungiwa mashine hizo.

Kutokana na hilo, wameiomba TRA kuzibana kwanza kampuni hizo au kuzichukulia hatua kwa  kuchelewesha  kuwafungia mashine hizo kama ambavyo  wameagizwa na Serikali.

“Suala la matumizi ya mashine za EFD’s sisi tumekuwa tukizitumia siku nyingi toka mwaka 2014 Serikali ilivyoagiza  matumizi ya mashine  hizo, ila tulikuwa hatujafunga kwenye  pampu na baada ya kuagizwa kufanya hivyo,  tulilazimika kununua mashine hizo kutoka kwa makampuni tuliyoelekezwa na TRA kuwa ndiyo yanauza, ambao yenyewe ndiyo yamechelewesha,” alisema Meneja wa Kituo  cha TFA, Ramadhan  Botto.

Alisema walilipia mashine hizo toka Julai 17, mwaka huu baada ya  TRA Mkoa wa Iringa  kufunga kituo chake kwa  kukosa mashine hizo.

Alisema baada ya kufungiwa walitozwa  faini na walilipa pamoja na kutakiwa kununua mashine hizo na  walifanya hivyo ila kampuni inayofanya kazi ya kuzifunga imechelewesha.

Mwandishi wa habari hizi alipowapigia simu Kampuni ya Boston Solution Limited kupitia mtandao wa Vodacom,  inayoishia na namba 690, ilipolewa na baada ya kutaka  kujua kuhusu hatima ya waliolipia mashine hizo lakini bado hawajafungiwa, mpokeaji aligoma kujibu lolote na kukata simu.

Mbali ya  wafanyabiashara wa vituo vya mafuta  kulalamikia ucheleweshaji wa mashine hizo, pia  wafanyabiashara ambao  walifungiwa maduka yao na TRA Mkoa wa Iringa kwa kutokuwa na mashine hizo wamelalamikia Kampuni ya Bolsto Solutions Limited kwa kuchelewesha mashine hizo licha ya kuzilipia kama walivyotakiwa.

Hivyo wameitaka TRA  kuwajibika kuwapa mashine hizo kwani  kampuni hiyo ilitambulishwa kwao na mamlaka hiyo, hivyo  kitendo cha wao  kufungiwa maduka ni kuwaonea.

Mfanyabiashara Victoria  Masawe, alisema kuwa walinunua kwa kiasi cha Sh 400,00 kama fedha ya utangulizi kwa mashine hizo toka Machi 14, mwaka 2014.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Lamson Tulyanje, alisema msako wa utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli kwa vituo vya mafuta visivyo na mashine za EFD’s umeanza tangu jana.

“Tunachokifanya katika msako huu ni kukagua  pia mashine zilizofungwa kama zinafanya kazi,  tukikuta mashine zipo ila hazifanyi kazi, vituo  hivyo vinafungwa,” alisema Tulyanje.

 

TANGA

Kwa Mkoa wa Tanga vituo vingi vya mafuta vilikuwa vikiendelea kutoa huduma hiyo, huku wakiendelea kutoa stakabadhi kupitia EFD’s.

MTANZANIA ilitembelea katika baadhi ya vituo na kubaini hali ni shwari katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Star Service Station kilichopo Barabara ya Saba jijini Tanga, Salmini Juma, alisema wamepokea vizuri mfumo huo kwa sababu unachangia kulipa kodi ipasavyo kutokana na baadhi yao awali kushindwa kufanya hivyo.

Alisema kabla ya kufungwa kwa mfumo huo, vituo vingi vilikuwa havilipi kodi na hivyo kuikosesha Serikali kukusanya mapato halali kutokana na mauzo ambayo walikuwa wakiuza kila siku katika vituo vyao.

Naye Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Lake Oil cha Chumbageni, Mohamed Twalib, alisema utaratibu huo ni mzuri kwani unarahisisha kutoa stakabadhi kwa wateja na kuondoa usumbufu mkubwa kwao, ikiwamo kuepukana na hasara ambazo walikuwa wakiingia kutokana na mauzo yao ya kila siku.

 

WIZARA YA FEDHA

Alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kuzungumzia suala hilo, Ben Mwaipaja, alisema suala hilo lipo kwa TRA.

Alisema leo Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango itaanza kufanya tathmini kuhusu agizo hilo na kisha kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari.

“Serikali itatoa maelekezo, wasiwe na wasiwasi, sisi tunaangalia utekelezaji wao na kisha baada ya kumaliza tathmini hiyo, tunakabidhi ripoti yao kwa rais kama alivyoagiza.

“Na sasa tunachofanya tunaangalia waliolipa, waliolipa ambao hawajapewa mashine, wasiolipa ambao wamegoma kutekeleza na tutawaita na kutoa taarifa hiyo pia,’’ alisema Mwaipaja.

Kuhusu mawakala wa mashine hizo kuwa wachache, alisema hawezi kulizungumzia kwa kina kwa sasa ila ni kwamba waliolipia watajulikana na ambao bado hawajapata mashine hizo na wasiolipia watajulikana mara baada ya kukabidhi tathmini hiyo.

 

TRA

Na alipotafutwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema kwa baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo ambao hawajafunga mashine hiyo, hawana nafasi ya kulalamika kwani walipewa muda tangu Julai Mosi mwaka 2016 na mawakala hao.

“Hao hao mawakala wameweza kuwafungia Puma, Oryx, Engine na Gapco je, wao walikuwa wapi mpaka wasubiri amri? Waulizeni,” alisema Kayombo.

 

Habari hii imeandaliwa na Francis Godwin (Iringa), Asha Bani (Dar es Salaam), Eliya Mbonea (Arusha) na Oscar Assenga (Tanga)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles