28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Kina Membe kusuka au kunyoa CCM

Nora Damian -Dar Es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinatarajia kueleza hatma ya makatibu wakuu wastaafu, Abdulrahman Kinana, Yusuph Makamba na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.

Hatua hiyo inakuja baada ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu ya chama hicho kukamilisha ripoti yake ambayo leo itawasilishwa kwenye Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli.

Viongozi hao wanakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa maadili kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na kanuni ya maadili na uongozi.

Kinana, Makamba na Membe waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii zikimsema vibaya Rais Magufuli.

Membe alihojiwa Februari 6, mwaka huu Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma na kusema kuwa alipata furaha kwa sababu alipata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama chake kilitaka kuyajua.

Aidha Februari 10,  Kinana na Makamba nao waliitikia wito wa kufika mbele ya Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili katika ofisi ndogo zilizopo Lumumba, Dar es Salaam.

Wengine waliohusishwa na sauti hizo ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

Hata hivyo kwa nyakati tofauti mwaka jana January, Ngeleja na Nape walimuomba radhi Rais Magufuli ambaye alisema kwa kutambua kuwa hao ni vijana, walimgusa na kuamua kuwasamehe.

“Kuna watu fulani walinitukana wee na ‘nika-prove’ kwamba sauti zile ni zao ‘more than one hundred percent’ (zaidi ya asilimia 100), nikawa nakaa nafikiria, nikasema hawa wakipelekwa kwenye Kamati ya Siasa ya Central Committee adhabu itakuwa kubwa,” alisema Rais Magufuli.

Chanzo cha sauti za viongozi hao ulikuwa ni waraka wa makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Makamba na Kinana, kwenda kwa Baraza la Wazee wa chama hicho wakilalamikia hali ya mambo yanayoendelea nchini.

Kinana na Makamba waliandika barua kwenda Baraza la Ushauri la Viongozi Wastaafu wa CCM wakitaka lichukue hatua dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwao kwa madai kuwa zimewachafua.

Juzi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema alisema siku saba zilizotolewa na Kamati Kuu CCM, zimeshamalizika na taarifa hiyo itapitiwa leo na Kamati Ndogo ya Nidhamu ili iweze kuwasilishwa mbele ya Kamati Kuu inayotarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki hii.

“Kamati Kuu itakaa mwishoni mwa wiki hii ili kupokea taarifa ya Mangula (Philip), hivyo wiki hii wakati vikao vikianza kamati hizo mbili kuu na ndogo ya nidhamu na maadili zitakaa,” alisema Dk. Bashiru.

Alisema uamuzi wa chama ni kuwa taarifa ya Mangula ipo tayari kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye vikao vya chama ambapo baada ya vikao Katibu Mwenezi wa chama, Humphrey Polepole atatangaza kama wamebainika kuwa na makosa na hatua gani zitachukuliwa na kwa adhabu gani.

“Yapo makosa mengine ukithibitika adhabu yake haitangazwi na badala yake anaambiwa mhusika na kwamba saa nyingine inaweza ikatolewa adhabu ya onyo kali hiyo itatangazwa hadharani. Pia inaweza kukosa aina fulani ya haki zako za uanachama .

“Ukithibitika umefanya makosa ya kukiuka kanuni, mtu mwingine anakosa haki za uanachama na kuwa chini ya uangalizi, lakini wakati mwingine mtu anapewa karipio kuliko onyo kali kama utaratibu wa kulitumikia ana muda wa uangalizi ili ajirekebishe.

“Wakati mwingine hupelekea mhusika kuachishwa uanachama na kuwa raia huru lakini anaweza kujiunga tena na kujiunga kwa mujibu wa taratibu za kikanuni na kama ni kiongozi anaweza kusimamishwa uongozi kwa muda au kuachishwa,” alisema Dk. Bashiru

Alisema adhabu hizo hutolewa baada ya watuhumiwa kusikilizwa, kujitetetea na Kamati Kuu kuchambua na kujiridhisha ili kutoa uamuzi.

“Kwa hiyo kuhusu hatua zitakazochukuliwa ni baada ya vikao vya kamati kukaa na kupokea taarifa ndiyo uamuzi utatolewa, hivyo taarifa ya Mzee Mangula itawasilishwa ndani ya Kamati Kuu mwisho wa wiki hii,” alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles