27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Kashfa nzito wizi wa mabilioni

Christina Gauluhanga na Godfrey Shauri -Dar Es Salaam

KASHFA nzito polisi wizi wa mabilioni ya fedha. Ndilo neno pekee unaloweza kusema baada ya Jeshi la Polisi Kanda  Maalumu ya Dar es Salaam kuwashikilia askari wake 8 na wafanyakazi watatu wa Kampuni ya Ulinzi ya G4S kwa tuhumza za kushiriki wizi.

Askari hao na watuhumiwa wengine, wanadaiwa kuiba Sh bilioni 1.2, Dola Marekani 402,000 (Sh milioni 926.6)  na Euro 27,700 (Sh milioni 69.2) ambazo ni mali ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alisema askari hao wanashikiliwa kwa sabbau ya kukiuka maadili ya kazi yao.

“Askari hawa tunawashikilia kwa sababu ya kukiuka maadili ya kazi yao katika tukio hili wote waliohusika lazima tutawashughulikia wawe wa ndani au nje.

“Askari wetu baada ya kufika eneo la tukio kwenye upekuzi walikiuka maadili na kuacha maagizo waliyopewa na viongozi wao katika ukamataji wa mtuhumiwa wa kwanza kuna ukiukwaji wa maadili waliofanya…hawakuzingati maelekezo waliopewa na mkuu wa oparesheni ya ukamati wa wezi hawa.

“Lakini pia walielekezwa wasubiri kiongozi wa oparesheni atakapofika atatoa maelekezo namna ya kufanya upekuzi, lakini walianza kufanya upekuzi ambao si kwa mujibu wa utaratibu.

“Baadae hicho kilichowapelekea kukisubiri kikaungwa mkono na mshtakiwa wa kwanza ambaye aliwalalamikia kwamba wamechukua baadhi ya fedha.

“Sisi kwa kuwa kazi yetu ni kulinda maisha ya watu na mali, hatutajali ni nani anayefanya nini awe ni mtuhumiwa wa ndani awe ofisa wa polisi atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria, awe ni raia pia atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria  tumewakamata na tutawashughulikia,” alisema Mambosasa.

Kuhusu kutaja majina ya askari waliokamatwa, Kamanda Mambosasa alisema hawezi kuwataja kwa sababu za uchunguzi.

“Siwezi kuwataja majina askari hawa, lakini yupo mkaguzi msaidizi ambaye alikuwa kiongozi,”alisema.

Alisema tukio hilo lilitokea Februari 7, mwaka huu,  Dar es Salaam ambapo rafiki yao,  Salum Shamte (43) ndiye aliyefanikisha kusafirisha fedha hizo kwa gari lake.

Aliwataja watuhumiwa hao, kuwa ni Christopher Rugemalila (34) ambaye ni dereva wa kampuni  ya ulinzi, mkazi wa Chanika, Mohamed Athuman (40), mlinzi wa G4S , mkazi wa Mtoni Kijichi, Ibrahim Maunga (49), mkazi wa Kiluvya na Shamte (43), mkazi wa Mbagala Kizuiani.

Alisema watuhumiwa Rugemalila, Athuman na Maunga, wakiwa na gari lenye namba za usajili T 728 BAN , aina ya Hard Body mali ya G4S walipewa fedha hizo ili kuzisindikiza makao makuu ya benki hiyo,lakini walikiuka na kutokomea nazo.

Alisema walinzi hao, walichukua fedha hizo kutoka matawi ya NBC Kariakoo na Samora ili wazipeleke makao makuu ya benki  hiyo yaliyopo Posta ya zamani Sokoine Drive, lakini  hawakufanya na matokeo yake walielekea Temeke Maduka Mawili karibu na kituo cha mafuta cha Camel.

Watuhumiwa hao, walichukua fedha zote na kuzipakia kwenye gari ndogo T 134 DHY Toyota IST  iliyokuwa ikiendeshwa na Shamte.

Alisema baada ya kufanikisha uhalifu huo walitelekeza gari la Kampuni ya G4S , silaha mbili mali ya kampuni hiyo aina ya ‘pump action’ , bastola moja, mashine ya kuhesabia fedha na muhuri wa Benki ya CBA kisha kuondoka kusikojulikana.

Alisema baada ya polisi kupata taarifa hizo waliunda kikosi kazi na kuanza ufuatiliaji ambapo Februari 17, mwaka huu, mchana, Mongolandege mtuhumiwa wa kwanza Rugemalila alikamatwa na kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na Sh milioni 110,  Dola za Marekani 19,000, zikiwa ndani ya gari lake lenye namba za usajili T 691 DSU BMW na magari matano yenye namba  tofauti.

Alizitaja namba hizo na thamani yake kwenye mabano kuwa ni T 691 DSU BMW yenye ( Sh milioni 15), T 909 TOYOTA Runx  (Sh milioni 13), T 627 DSU Toyota IST (Sh milioni 11), T 653 DSU Toyota IST (Sh milioni 11) na  T 857 DSU Toyota IST (Sh milioni 11).

Alisema pia alikiri kununua nyumba mbili, kiwanja kimoja vyenye thamani ya Sh.milioni 107, samani za ndani  vyenye thamani ya Sh milioni 5 na kufanya thamani ya mali na fedha taslim kuwa zaidi ya Sh milioni 297.1 na Dola 21,000.

Mambosasa alisema  pia Februari 21, mwaka huu, watuhumiwa Mohamed Ramadhan na Salim Shamte  walikamatiwa Mbagala,Dar es Salaam.

Alisema baada ya kupekuliwa walikutwa na Sh milioni 332, Dola za Marekani 50,000, Euro 5010 na gari lenye namba za usajili T 134 DHY aina ya Toyota IST, iliyotumika kubeba fedha siku ya tukio, baada ya kulitekeleza gari la Kampuni ya G4S.

Watuhumiwa wawili walikiri kununua viwanja viwili maeneo ya Kisemvule na Kivule vyenye thamani ya Sh milioni 25 ambapo thamani ya mali ni Sh milioni 357, dola 50,000 na euro 5010.

Alisema upelelezi uliendelea na usiku wa kuamkia Februari 24, mwaka huu mtuhumiwa Maunga alikamatwa, alipopekuliwa alikuwa na Sh 192,213, 450, Dola za Marekani 70,600 na nyumba aliyonunua Kibaha Sh milioni 30, samani za ndani zenye thamani ya Sh milioni 10 thamani ya mali ni Sh milioni 253.

Alisema jeshi hilo, linaendelea kuwashikilia watuhumiwa  hao watatu wa kampuni hiyo akiwamo mtu mmoja ambaye aliwasaidia kufanikisha wizi huo.

POLISI KUKAMATWA

Alisema wakati oparesheni ya kuwasaka na kuwakamata watu hao, ikiendelea jeshi lake lililazimika kuunda kikosi kazi ili kubaini ukweli.Alisema kikosi hicho kilisaidia kupata taarifa zilizosaidia kuwatia mbaroni askari hao.

Onyo

Alitoa onyo kwa kampuni zinazosafirisha fedha kuwa makini wakati wa usafirishaji kwakuwa mazingira ya tukio hilo inaonyesha yaliandaliwa tangu fedha hizo zinapakiwa.

“ Hatutakubali uzembe huu uendelee fedha za Watanzania ziendele kupotea tuna amini katika hili kuna ‘inside job’ tutashughulika na wote waliohusika,”alisema Mambosasa.

Katika tukio jingine, mtuhumiwa wa ujambazi  Ramadhan Rashid (20), ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya jaribio lake la kutaka kuwakimbia polisi kushindikana.

Alisema mtuhumiwa alikamatwa  na Kikosi cha Kupambana na Ujambazi, Februari 24, mwaka huu, saa 7 :30 usiku, Sabasaba Mbagala Kizuiani.

Alisema mtuhumiwa  alikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi Tuangoma , Mbagala na Mkuranga ndipo alipokiri kukubali kwenda kuonyesha askari alipoficha  silaha na watuhumiwa anaoshirikiana nao walipofika eneo hilo alianza kukimbia huku akipiga kelele.

Alisema kuona hivyo, askari walifyatua risasi tatu hewani kuamuru asimame lakini alikaidi na risasi moja ilimpata.

Mtuhumiwa alifariki dunia wakati akipelekwa hospitalini kwa matibabu.

MATUKIO YALIYOPITA

AGOSTI 3, mwaka 2001 saa 2 usiku, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana alitangaza unyan’ganyi wa Dola za Marekani milioni 2  uliokuwa umetokea nje kidogo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalim Julius Nyerere (JKIA).

Katika tukio hilo,dereva wa Kampuni ya Ulinzi ya Knight Support, Justine Kasusura alitokomea na mabilioni ya fedha.

Kasusura hakupatikana kwa miezi mitano na baada ya hapo alikamatwa Desemba 24, mwaka 2001 katika hoteli  ya Three In One’ maeneo ya Soweto, Mbeya.

 Kasusura alifikishwa mahakama ya Kisutu Januari 7, mwaka 2002 na Land Rover Defender Namba PT 0881 akiwa pamoja na washtakiwa wengine sita

Katika tukio hilo, Januari 16, 2002 maofisa nane wa polisi walifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka mawili ya kula njama ya kumtorosha Kasusura

 ASKARI WA DHAHABU

Askari nane  walishtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi jijini Mwanza kwa tuhumza za kushirikia kusindikiza shehena ya dhahabu.

Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa na taratibu za kuwarejesha kazini zilianza.

Askari hao pamoja na wafanyabiashara wanne, walikuwa wakikabiliwa na makosa matano ya kutakatisha fedha, uhujumu uchumi na kula njama za kupanga uhalifu, makosa waliyodaiwa kuyatenda kati ya Januari 4 na 5, mwaka jana. Rais Dk. John Magufuli aliagiza askari hao warejeshwe kazini.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,554FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles