22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

‘Kina baba wanapaswa kujihusisha na hedhi salama kwa watoto’

Na AVELINE  KITOMARY

HEDHI  ni hali ya mwanamke  kutoka damu ukeni  baada ya kuta za ndani za mji wa mimba kujiengua, au ni muunganiko wa yai ambalo halikurutubishwa pamoja na damu inayotokana na kumomonyoka kwa tishu laini za ukuta wa mfuko wa mimba (uterus).

Hali hii kwa kawaida hutokea kila mwezi kwa mwanamke na huratibiwa na mzunguko wa homoni.

Kuvunja ungo au hedhi ya kwanza kwa wastani  huanza kati ya umri wa miaka 12 hadi 15.

Hata hivyo, katika hali zingine huenda ianze baadaye kwa kuchelewa kati ya umri wa miaka 17 hadi 20 au mapema kati ya umri wa miaka nane hadi tisa.

Baadhi ya mambo yanayoathiri umri wa kuvunja ungo ni ya kibayolojia na mengine ni ya kitamaduni.

Kuvunja ungo  au hedhi ya kwanza  huanza kwenye  sehemu ndogo katika ubongo (hypothalamus)   ambapo inapochochewa kuanza kutoa homoni iitwayo gonadotropin katika umri wa takribani miaka 12 hadi 15.

Imethibitishwa kuwa homoni inayoongeza uzalishaji wa mbegu za kiume au mayai ya kike (ganadotropins)  inaweza kuanza kutolewa kuanzia umri chini ya miaka 12  kwa wasichana ambao wana afya njema na kujihusisha kufuatilia mambo ya ngono.

Mambo hayo ni  kama vile kutazama filamu za ngono na kuzungumzia masuala ya ngono.

Wakati mwingine, hedhi ya kwanza (kuvunja ungo) inaweza kuchelewa  hadi umri wa miaka 17 hadi  20 kwa wasichana  wasio  na  afya njema na wasiotangamana na mambo yanayozidisha hamu ya ngono.

Magonjwa yanayoathiri sehemu ndogo ya ubongo iitwayo Hypothalamus na tezi ya pituitari au ovari na uterasi yanaweza pia kuathiri umri wa hedhi ya kwanza.

Katika umri wa kuvunja ungo, homoni za uzazi wa kike, oestrogen huleta mabadiliko katika mwili wa mwanamke kama vile matiti kukua, kupamuka kwa nyonga, kuongezeka kwa shughuli za tezi za jasho na za mafuta na uotaji wa nywele  sehemu za siri hata kwapani.

Hedhi huendelea kutoka kila mwezi isipokuwa wakati wa ujauzito hadi mwanamke huyo atakapofikia kikomo cha hedhi kati ya takribani umri wa miaka 48 hadi 50 ambapo hedhi hukoma.

Mtoto mchanga wa kike anapozaliwa tayari huwa na takribani ova 60,000 zisizopevu na hawezi kutoa zingine zaidi maishani mwake.

Anapofikia ukomo wa hedhi, uwezo wake wa kupevusha ova hufika mwisho.

IMANI YA JAMII IKOJE?

Hedhi  sio jambo jipya  kabisa  kwenye jamii yetu ya Kiafrika na Kitanzania kwani lilikuwapo tangu binadamu alipoumbwa.

Katika maeneo mengi na tamaduni  za Afrika, bado suala la mjadala wa hedhi limekuwa la siri kati ya wanawake pekee wakati mwingine kufanywa kuwa suala la miiko  kutokana  na kutokujadiliwa waziwazi.

Hali hiyo inachangia kuwapo kwa changamoto nyingi miongoni mwa wanawake na  wasichana wadogo, ambazo wakati mwingine zinaweza kuwafanya wakakosa kufikia fursa sawa na wanaume au watoto wa kiume.

Zipo jamii ambazo zina imani potofu kuhusu damu ya hedhi ya mwanamke, wakidhani kuwa ni sumu na inaweza kusababisha mimea kukauka, chakula kuchacha au pombe kuwa chungu.

Hivyo, macho ya watu yanaposhudia damu ya hedhi ya mwanamke imesambaa kwenye nguo zake, ni wazi kuwa watamtenga na kumbagua na wengine kumsema vibaya.

Ubaguzi huo unaweza kujitokeza shuleni na hata katika shughuli mbalimbali za kijamii endapo mwanamke atakumbwa na hali hiyo.

Si kwa jamii tu hata kwa wanawake endapo ataonekana na damu hiyo atahisi kupoteza thamani yake mbele za watu waliomuona.

Ifahamike kuwa suala la kukosekana kwa hedhi salama halijawa kikwazo  cha mtoto wa kike kupata haki zake za msingi  bali jambo hili linazorotesha juhudi za utimizaji wa malengo ya maendeleo.

Ni kwa vipi mtoto kike atahakikisha anapata elimu bora yenye usawa na fursa ikiwa mahudhurio yake yatashuka kisa tu amekosa nyenzo muhimu za kumfanya apata hedhi salama na kubaki shuleni? Ni dhahiri kuwa suala hili litaathiri masomo yake. 

Hedhi salama ni ile ambayo inahusisha mtoto wa kike kupata mahitaji yake yote muhimu akiwa kwenye siku zake za hedhi.

Mahitaji hayo huhusisha taulo za kike ama pedi kama ijulikanavyo na wengi, maji safi na salama na sehemu ya kubadilishia.

Wataalamu  wa  afya wanasema kuwa mtoto wa kike akipata hedhi salama basi ataweza kuondokana na matatizo mengi ya kiafya kama vile miwasho, fangasi, maumivu pamoja na hedhi bila kutokwa damu nyingi na hivyo huwa hedhi yenye amani na furaha.

ASIMULIA SIKU ALIYOVUNJA UNGO 

Fatuma  Jumanne (sio jina lake halisi)  ambaye kwasasa ana umri wa miaka 17 anasimulia jinsi elimu ya hedhi ilivyomsaidia alipovunja ungo mwaka 2015.

Anasema wakati hali hiyo ilipomkuta kwa bahati nzuri alikuwa nyumbani hivyo ilimpa wepesi wa kutoa taarifa kwa mlezi wake.

Anaeleza kuwa bibi yake ambaye ndiye alikuwa akimlea, alimsaidia kwa kumpa maelekezo ya namna ya kujisitiri.

“Nakumbuka nilivunja ungo Desemba, mwaka 2015 nikiwa nyumbani. Kutokana na elimu niliyopewa, sikupata hofu yoyote maana hata wenzangu shuleni waliniambia hivyo nilikuwa nasubiria siku tu.

“Lakini, wakati tukio hilo linatokea ilikuwa usiku hivyo nilivyoamka nikakuta nimelowa katika nguo zangu nikawaza kuwa kuenda ilikuwa ni haja ndogo, nikaenda kwa bibi yangu kumwambia akanielekeza namna ya kufanya,” anaeleza.

Anasema hali hiyo pia imemfanya kuwa imara zaidi hata aliporudi shuleni  kwani alikuwa anasoma shule ya kulala (boarding).

“Sikuwahi kushindwa kuingia darasani kwa sababu vifaa vya kutumia tunapata na walimu walezi walikuwa wanatusaidia katika masuala ya hedhi mara kwa mara.

 “Hata nikiwa nyumbani mama ananikatia vitambaa vya kujisitiri lakini shuleni situmii vitambaa kwa sababu siwezi kufua kwani kutokana na ulemavu wa macho nilionao nikiwa nyumbani mama huwa ananiangalizia kama imetakata au la,” anabainisha.

Hata hivyo, sio wasichana wote wanaweza kuwa kama Fatuma, ambaye anasaidiwa kupata pedi au vitambaa vya kujisitiri kwani wengine huweza hata kukosa masomo kutokana na kushindwa kujisitiri wakati  wa hedhi.

Kutokana na hilo, kuna haja ya wanafunzi wa kike kusaidiwa kuweza kujisitiri wakati wa hedhi.

WALIMU WANAWEZA KUSAIDIA HEDHI SALAMA

Nafasi ya walimu hasa wa kike au walezi shuleni, ni kubwa katika kuhakikisha kuwa suala la hedhi salama kwa wanafunzi wa kike linafanikiwa .

Ikiwa nafasi hiyo wataitumia ipasavyo wanafuzi wa kike wataweza kuhudhuria darasani siku za hedhi bila tatizo lolote.

Clementina Njelima, ni mlezi wa wanafunzi katika  Shule ya Msingi Buigiri, wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, anasema yeye amekuwa akiwasaidia wanafunzi wa kike waliovunja ungo kuweza kutambua namna ya kujisitiri.

“Nimeanza kufanya  kazi hii tangu  mwaka 2002 na sasa  kuna watoto 129 hapa shuleni ambapo kati ya hao wasichana waliovunja ungo ni 15.  

“Kuna Changamoto kadhaa ukizingatia shule hii ni maalum kwa watoto wasioona, ni tofauti na shule zingine unatakiwa uwalee kwa upendo hivyo hata maelekezo ni vigumu kushika kuliko wanaoona, lakini tunamshukuru Mungu kwa sababu tunawalewesha. 

“Tunawaelekeza namna ya kuhifadhi pedi na zikishajaa tunamwaga mahali tunazichoma japo hatuna shimo, ni wachache huwa wanaweka popote lakini wale wazoefu wanaweka sehemu husika,” anabainisha mlezi huyo.

Anasema kuwa endapo mwanafunzi wa kike atakapofikia hatua ya kuvunja ungo akiwa shuleni, taarifa hutolewa kwa mlezi na wanafunzi wenzake hivyo anafanya haraka kumuelekeza namna atakavyoweza kujisitiri.

“Tunamwelekeza namna ya kuwa msafi nikimaanisha kujisafisha kama kuoga mara kwa mara, pia tunamwelekeza kuwa asijihusishe na masuala ya wanaume tukimsisitiza kwamba akifanya hivyo atapata ujauzito.

“Pia huwa tunawapigia simu wazazi wake na kuwaeleza kuwa mtoto wao amekua,” anasema.

Anachokitamani Clementina ni kupata washauri  watakaoweza kuzungumza na wanafunzi hao hasa katika suala la kujua mipaka yao.

“Kuna wakati mwingine unaweza kumweleza kitu akakuona mkali au anaonewa kwahiyo akiwa na mtu mwingine ataelewa zaidi,” anashauri Clementina.

KINA BABA WATAKIWA KUJIHUSISHA

Imebainika kuwa kina baba huwa hawana utaratibu wa kujihusisha na mambo ya hedhi kwa watoto wao wa kike.

Baadhi yao wanasema kuwa hawajawahi kujihusisha kutokana na mambo hayo kuwahusu wanawake pekee.

Pia wapo wanaosema kuwa ni mwiko katika jamii kujihusisha na hayo mambo huku wengine wakitaja aibu kuwa sababu.

Miongoni mwa kina baba 20 waliohojiwa na gazeti hili, tisa walikiri kubadilika kwa kujihusisha na mambo ya hedhi huku waliobaki wakisema hawatathubutu kufanya hivyo. 

Mmoja wa baba aliyehojiwa kuhusu suala hilo, ambaye pia ni ni mwandishi wa habari, Michael Maurus, anasema uwazi ni sehemu muhimu hasa kwa wasichana wadogo.

Maurus anataka jamii isione kuwa suala hilo ni aibu hivyo kuzingatia kuwaelimisha watoto wao wa kike  kuhusu hedhi na hata masuala ya uzazi kwa ujumla.

 “Suala la hedhi halitakiwi kuwa la siri katika familia, elimu itolewe kwa watoto, kuna siku nilikuta mtoto wa kike ametokwa damu ila hajui jinsi ya  kujisitiri ili aweze kuwa katika hali ya usafi nikachukua jukumu la kumsaidia.

“Natamani wafundishwe namna bora ya kujisitiri, wapewe uwezo wa kujiamini na kujitambua, mtoto aweze kuomba hela ya pedi hata kwa baba, isiwe jambo la ajabu kwao,”anabainisha.

ASHAURI BAJETI ZA PEDI KATIKA FAMILIA

Maurus anashauri licha  ya familia kuweka uwazi kuhusu mambo ya hedhi, pia bajeti za manunuzi ya pedi za kujisitiri ziwekwe katika ngazi ya familia kama ilivyo mahitaji mengine.

“Binafsi huwa nina kawaida  ya kununua pedi na kuwapelekea watoto wangu na nawaambia kuwa pedi hizi hapa wanafurahi  wazitumia badala ya vitambaa, pia huwa nawashauri kutopewa kazi nzito wakiwa katika kipindi cha hedhi,” anasema.

Anaongeza “Natamani wazazi kuweka bajeti za pedi kama ilivyo kwenye chakula na mahitaji ya shule. Wazazi wa kiume wasione haya kuwasaidia watoto wao wa kike, wasikwepe majukumu kwa hilo sio suala la mama tu, ni kitu ambacho lipo na sio cha dharura.

Kwa upande wake mmoja wazazi aliyejitambulisha kwa jina la mama Kalebi anasema: “Wenzetu wa  nje wazazi  wote wanawajibika ila kwa mila za Afrika mama ndio anahusika zaidi  hivyo, wanaume kushiriki ni utamaduni wa kigeni.

JUKWAA LA HEDHI SALAMA

Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania, limekuwa na kawaida ya kutoa mafunzo ya namna ya kujisitiri wakati wa hedhi. 

Pia limekuwa likifanya tathmini ya mafunzo hayo wanayotoa katika shule mbalimbali. 

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, ambaye pia ni Ofisa Afya Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Salvatha Silayo, anasema lengo la tathmini hiyo ni kuona jinsi walimu na wanafunzi walivyotekeleza kwa vitendo mafunzo wanayopatiwa.

Silayo anasema mwaka 2019 jukwaa hilo ambalo linawajumlisha wadau mbalimbali wa hedhi salama, lilitoa mafunzo kwa wanafunzi hivyo katika kipindi cha mwaka mmoja sasa wameamua  kuwa pamoja na kuweka mikakati ambapo yale ambayo hayajaweza kutekelezwa yatekelezwe.

“Mwaka jana tulifika Shule ya Msingi Buigiri na kuwaeleza wanafunzi wote na walimu wao namna ya kujisitiri wanapokuwa kwenye hedhi, sasa tumekuja kuangalia je, yale tuliyowafundisha wametekeleza?

“Tumeona mambo mengi yametekelezeka na yale machache tumeyawekea muda yatekelezwe,” anasema  Silayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles