22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Siri namna ya kujitafutia furaha maishaniSiri namna ya kujitafutia furaha maishani

Na MWANDISHI WETU

FURAHA ni hitaji la kila mtu. Hatupendi kukosa furaha. Tunapoikosa, mioyo yetu huwa inahangaika. Hata katika nyakati tunapoonekana kutamani kinyume cha furaha, kimsingi tunafanya hivyo kwa sababu tunahitaji furaha. 

Furaha, kwa ujumla, ni ile hali ya kuridhika inayomfanya mtu awe na moyo uliochangamka, unaoyatazama mambo kwa mtazamo chanya. Mtu anayejisikia kuridhika anakuwa na mtazamo chanya kwa nafsi yake mwenyewe, watu wanaomzunguka na hata maisha kwa ujumla. 

Furaha inaonekana kuwa moja wapo ya malengo makubwa ya mwanadamu. Wapo wanaofikiri kuwa maisha kimsingi ni harakati za kuitafuta furaha. Kwamba, kila tunachokifanya kinalenga kutuhakikishia furaha. 

Kwa watu wengi, kwa mfano, kutafuta fedha na mali kunasukumwa na shauku ya kuwa na furaha. Hofu ya maisha yenye dhiki inatusukuma kutafuta fedha. Hali za maisha zinapotuondolea uhakika wa kipato, furaha inatuacha. Tunaamini bila vitu, ni vigumu kuwa na furaha. 

Si fedha pekee inayofikiriwa kuwa chanzo cha furaha. Karibu kila kitu tunachokifanya katika maisha yetu kinaonekana kulenga kutupa furaha. Elimu na maarifa; mamlaka na madaraka; umaarufu na uwezo; uhusiano na urafiki; imani na dini; kazi na ajira; vyote hivyo vinaishia kwenye furaha.

Hata hivyo, si mara zote tunapokuwa na hivyo vyote, tunaweza kudai kuwa na furaha. Unaweza kuwa na maarifa, madaraka, umaarufu, uhusiano imara, kazi nzuri na vyote unavyovitamani katika maisha lakini bado ukaikosa furaha. 

Ilivyo ni kwamba, wakati wewe mwenye vyote hivyo kwa pamoja ukifikiria namna ya kuwa na vingine zaidi kwa matumaini ya kuwa na furaha usiyo nayo, wengi kwa maelfu nao wana ndoto za kuwa kama wewe ili waweze kufurahia maisha.

Aidha, wakati mwingine kutokuwa na chochote kunaweza kusiathiri furaha. Katika sehemu nyingi vijijini, kwa mfano, ambako kwa vigezo vya mjini watu wanaishi katika lindi la ufukara mkubwa wa kipato, unaweza kushangaa namna watu wanavyoishi maisha yaliyojaa utoshelevu na furaha. 

Ukitembelea maeneo hayo unakutana na watoto waliojaa vumbi lakini wenye vyuso zilizofunikwa na tabasamu lisilo na chembe ya unafiki. Unakutana na kina mama wanaotembea peku peku, wenye kuvalia mavazi chakavu lakini wenye nyuso zilizopambwa na furaha. 

Katika mazingira kama haya, unakutana na akina baba wasio na hata senti mfukoni, lakini wenye mioyo iliyojaa matumaini. Ni kama vile kutokuwa na kitu chochote kinachohesabika kuwa cha thamani hakuondoi furaha yao.

Ingawa ni kweli watu hawa wanaweza kuwa katika mazingira duni, ambayo wakati mwingine yanahatarisha afya zao wenyewe, nyuso zao zimekunjuliwa na matumaini. 

Sisi tunaoishi mijini, kwa kutumia vigezo vyetu vya maendeleo tunaweza kuwahurumia. Tunaweza hata kuthubutu kuwashauri namna ya kuachana na maisha yao hayo ya kijima. Lakini wao wenyewe hawana wasiwasi huo tulio nao sisi.

Katika mazingira ambayo wale wanaofikiriwa kuwa na karibu kila kigezo cha kuwafanya wawe na furaha, wanakuwa hawana furaha, ni muhimu kujiuliza, furaha hasa inatoka wapi? Kwanini, kwa mfano, masikini asiye na senti za kupanda daladala awe na furaha, wakati mwenzake aliyeendesha gari la kifahari asiwe na furaha?

Umewahi kujiuliza kwanini wakati mwingine unakuwa na furaha lakini wakati mwingine unakosa sababu ya kukufanya uwe na furaha?  

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles