28.4 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

KILA LA KHERI WANAFUNZI DARASA LA SABA LEO



LEO watahiniwa 960,000 wanafanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi nchini kote.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 503,972 sawa na asilimia 52.49 na wavulana ni 456,230 sawa na asilimia 47.51.

Alisema watahiniwa wasioona waliosajiliwa ni 90, wasichana 31 na wavulana 59, wenye uoni hafifu ambao wanahitaji maandishi makubwa ni 846, wavulana 475 na wasichana 371.

Idadi hii ni kubwa ambayo tunaamini katika elimu waliyoipata kwa miaka saba, wanaweza kujiandaa sasa na safari ya kupata elimu ya sekondari,

Lakini pamoja na hatua hiyo, tunakubaliana na kauli ya Dk. Msonde kuwa wasimamizi walioteuliwa lazima watimize wajibu wao kwa kusimamia na kutekeleza maelekezo waliyopewa.

Moja ya mambo makubwa ambayo wanapaswa kujiepusha nayo ni vitendo vya rushwa na udanganyifu ambavyo miaka mingi tumeshuhudia vikitokea sehemu mbalimbali nchini.

Pia, wamiliki wa shule wanapaswa kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani, hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huu, maana kumekuwapo na tabia ya walimu husika kutaka kusaidia wanafunzi wao ili wafaulu.

Ni ukweli usipingika kuwa hatua sahihi kwa kituo kitakachobainika kufanya hivi, kifutwe na hatua nyingine za kitaaluma zichukuliwe.

Wakati tunawakemea wasimamizi na walimu, tunatoa rai tena kwa watahiniwa kufanya mitihani yao kwa weledi bila kujihusisha na vitendo vya udanganyifu ambavyo mara nyingi husababisha kufutiwa matokeo yao.

Tunaamini kuna kanuni za mitihani ambazo ndiyo mwongozo mzima, zinapaswa kufuatwa bila kupindishwa.

Katika eneo hili, tunawashauri wahusika kama kutatokea matukio ya aina hiyo, kutoa taarifa kwa vyombo husika na wale wote watakaobainika kuchukuliwa hatua.

Mtihani wa mwaka huu ni tofauti na mwaka jana, kwa sababu uliopita ulikuwa na maswali ya kuchagua, lakini kuanzia sasa kila somo litakuwa na maswali 45, kati ya hayo 40 yatakuwa ya kuchagua na matano yasiyo ya kuchagua.

Kuhusu muundo huo mpya wa mitihani, Dk. Msonde alisema umekuja baada ya baraza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu wakitaka yawepo maswali ya kuchagua na yasiyo ya kuchagua.

Mfumo wa mitihani ya kuchagua ulianza mwaka 2012, huku ukipingwa na wadau mbalimbali wikiwamo wabunge, wakisema utazalisha wahitimu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Bila kificho, mfumo huo ulishuhudia nusu ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013, wakiwa wamepata asilimia 40 ya alama kwenda chini.

Waziri wa Elimu wa wakati huo, Dk. Shukuru Kawambwa, akitangaza matokeo hayo Desemba 2012, alisema wanafunzi 294,833 sawa na asilimia 52.58 waliopata daraja D walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Idadi hiyo iliungana na wenzao 265,873 waliopata madaraja ya A, B na C ambao ni sawa na asilimia 47.41.

Sisi MTANZANIA, tunawasisitiza wanafunzi wote kufanya mitihani yao kwa umakini ambao utawasaidia kufaulu na kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari mwakani.

Kwani hiyo ndiyo hatua ya kwanza ya kuanza njia ya kupata elimu ya juu, hivyo tunapenda kuona matokeo yakayotoka yatakuwa mazuri ambayo yatawapa nafasi ya kuchaguliwa.

Tunamalizia kwa kusema  elimu ndiyo ufunguo wa maisha kwa kila mtu, hatupendi kuona wanafunzi hasa wa kike wanaishia kuolewa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles