26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

KIGEZO MUHIMU UNAPOMTAFUTA MWENZI WA MAISHA – 2

 

 

Na Christian Bwaya,

KISAIKOLOJIA, dalili ya kwanza kuwa unampenda mtu ni kiwango chako cha kumwamini. Kumwamini maana yake ni kutokuwa na wasiwasi na mtu kiasi cha kuthubutu kumwambia mambo yako ya faragha bila hofu ya kutokueleweka. Kuwaamini watu, hata hivyo, si jambo rahisi. Binadamu hatuna kawaida ya kumwamini kila mtu.

Kinachotuzuia kuwaamini watu kiholela ni ile hofu tunayokuwa nayo ndani yetu kwamba watu wakitufahamu undani wetu inawezekana ama washindwe kutuelewa  kama tunavyotamani au basi tunaweza kujikuta katika mazingira ya kugeukwa. Kwa sababu hiyo, ili kujilinda, binadamu tuna desturi ya kuchagua kwa makini watu tunaofikiri tunaweza kuwaamini. Ingawa tunaweza kuwa watu wengi tunaofahamiana nao lakini tunaowaamini wakawa wachache.

Kuaminiana katika ndoa

Kuaminiana ndio msingi wa kwanza wa uhusiano ya karibu kama ndoa. Huwezi kusema unampenda mtu ambaye moyo wako una shaka naye. Lazima mapenzi yaanze na kumwamini kisha mengine yafuate. Ni hivyo kwa sababu ukifanikiwa kumwamini mtu unakuwa na ujasiri wa kutosha kumwambia mambo uliyonayo moyoni.

Mwenzi wa ndoa ndiye mtu wa karibu zaidi anayepaswa kujua undani wako wote. Ndiye anayepaswa kuwa mtu wa kwanza kufahamu matumaini yako; wasiwasi wako; udhaifu wako; mipango yako na mambo yote yanayokuhusu. Kuaminiana ndiyo sababu ya kwanza inayowafanya watu wawili kuamua kuishi pamoja kama mke na mume. Ndoa ndio uhusiano unayoweza kumwondolea mtu hofu ya kutokueleweka; hofu ya kusalitiwa; hofu ya kudanganywa na mambo kama hayo.

Unapokuwa na mume/mke ambaye ndani yako huna kabisa ujasiri wa kumwambia mambo yako ya faragha, maana yake ukaribu wenu una shaka. Furaha na usalama wenu kama wapenzi hautegemei namna gani kila mmoja anajilinda na mwenzake. Utoshelevu wenu hautegemei namna kila mmoja anavyoweza kuficha mambo yake binafsi bali vile mnavyokuwa na uhuru wa kushirikishana mambo ambayo ambayo hamwezi kumshirikisha mtu mwingine. Hicho ndicho kiwango cha juu kabisa cha ukaribu katika ndoa.

Gharama ya kuaminika

Hata hivyo, kuaminiana si tukio la siku moja. Imani kati ya watu wawili wanaopendana inajengwa hatua kwa hatua. Kupitia mambo unayomfanyia mwenzako ndivyo anavyoweza kuendelea kujenga imani na wewe. Kwa mfano, unapokuwa na tabia ya kuwadanganya wenzako mbele ya mwenzako, hiyo inakupunguzia alama za kuaminika. Kwamba umeweza kuwadanganya wengine, maana yake unaweza kumdanganya na yeye.

Kadhalika, unapokuwa mtu mwenye tabia ya kutapanya fedha kadri anavyozipata unafanya iwe vigumu kwa mwenzako kukuamini. Kuelewa thamani ya fedha, kuwa na nidhamu ya fedha ni sifa muhimu ukitaka uaminiwe. Huwezi kuomba kuaminiwa kama bado hujaweza kuaminika.

Namna ya kumjua anayeaminika

Unapofikiria mtu anayeweza kuwa mwenzi wako wa maisha, jiridhishe na kiwango chake cha kuaminika. Kipimo rahisi cha kuaminika kwa mtu ni ukomavu wa kutunza mambo. Mtu asiye na siri, anayeweza kusema lolote kwa yeyote ni vigumu kuaminika.

Pili ni namna mtu huyo anavyoweza kuheshimu makubaliano anayoweka na watu bila kutafuta visingizio. Mtu anayeaminika, kwa kawaida, anapoahidi kufanya kitu anasimamia maneno yake. Jambo la kuzingatia ni kwamba mtu anayekupenda anaweza kuwa tayari kuheshimu ahadi zake kwako lakini asifanye hivyo kwa watu wengine. Jiridhishe ikiwa mtu unayemfikiria kuwa mwenzi wako ana uwezo wa kuheshimu makabaliano madogo anayoweka na watu wengine.

Kadhalika, aina ya misimamo aliyonayo mtu katika mambo ya msingi inaweza kuwa kipimo cha kuaminika kwake. Mtu asiye na misimamo imara inaoongoza maisha yake hawezi kuaminika. Lakini pia ili watu wawili waweze kuaminiana lazima misimamo yao katika mambo ya msingi ioane.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles