22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

ADHA YA MAJI PANGANI YAWATESA WANAWAKE NA MADUMU BAHARINI

 

 

Na Susan Uhinga,

SERA ya Taifa ya maji inaelekeza kila Mtanzania kutembea umbali usiozidi mita 400 kupata maji safi na salama, ikiwa sawa na kutumia muda wa nusu saa kupata huduma hiyo, lakini hali imekuwa tofauti katika baadhi ya maeneo.

Mtanzania imefanikiwa kutembelea Wilaya ya Pangani katika Kijiji cha Buyuni, ambapo wakazi wake wanatembea umbali wa kilometa sita kufuata huduma ya maji safi na salama katika Kijiji cha Uvinza kilichopo Wilaya ya Bagamoyo.

Kijiji cha Buyuni chenye wakazi takribani 206 sawa na kaya 90 kinakabiliwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama ambapo wanakijiji hulazimika kutembea umbali wa kilometa 6 sawa na saa saba kufuata huduma hiyo.

Wakazi wa kijiji hicho wanaeleza kwamba hali hiyo huwafanya washindwe kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa kuwa ndiyo maisha yao ya kila siku.

Mmoja wa wanakijiji hao, Mwanamwamba Ramadhan anasema wanataabika mno kwani kila siku huwa wanaamka saa kumi alfajiri na kutembea kwa muda wa saa saba kufuata maji  katika Wilaya ya Bagaboyo, ambako kuna kijiji kinaitwa Uvinza.

Anasema maji wanayoyafuata kwa umbali huo ni ya kisima, hali ambayo inawaumiza lakini hawana jinsi.

“Kero hii imechangia kwa kiasi kikubwa wanawake wengi kuishi katika mazingira duni kwa kuwa wanashindwa kujishughulisha na kazi nyingine za kujipatia kipato,” anasema mama huyo.

Anasema kuwa kijiji wanachofuata maji kimepakana na Hifadhi ya Taifa Saadan hivyo huwa hatarini kuliwa na wanyama wakali.

Naye Mwanaidi Ramadhan, mkazi wa Buyuni anawalaumu viongozi ambao wakati wa uchaguzi huomba kura huku wakiwaahidi kumaliza tatizo hilo, lakini wanapopata uongozi huwasahau.

“Kila siku ni lazima tubebe ndoo za maji kichwani, hatuna kazi nyingine za kimaendeleo tunazozifanya.

“Watoto wetu pia wanashindwa kufanya vizuri shuleni kwani licha ya kusoma mbali, pia wanaenda shule wakiwa wachafu hali inayowafanya wasijisikie huru mbele ya watoto wenzao.

“Wakati mwingine hutulazimu kuwaambia wasiende shule ili watusaidie kuchota maji,” anasema mama huyo.

Kutokana na adha hiyo wanayokumbana nayo, imewalazimu kubuni mbinu ambayo pia ni hatari lakini inawasaidia kubeba madumu mengi kwa wakati mmoja.

Mbinu hiyo ni ya kubeba madumu mengi ya maji ya lita 20 na kuogelea nayo baharini.

“Tunapofika kisimani tukimaliza kujaza maji kwenye madumu yetu hata yakiwa 10 tunayabeba hadi baharini ambako kuna umbali wa kilometa moja kutoka kisimani.

“Tukifika ufukwe wa Bahari ya Hindi ukanda wa Pwani ya Tanga tunayafunga madumu kamba yote kwa kutumia kamba ndefu, kasha na sisi tunajifunga halafu tunaanza kuogelea nayo hadi pwani ya Kijiji cha Buyuni ambako ndiyo makazi yetu,” anasema mama huyo.

Anasema kuwa mbinu wanayoitumia ni hatari lakini hawana namna kwa kuwa maji ndio kila kitu katika maisha ya mwanadamu.

Asha Jumbe anasema kuwa kwa kawaida huwa wanaogelea baharini kwa muda wa saa saba wakiwa wamejifunga na madumu hadi kufika kijijini.

Anasema kuwa wakati mwingine mawimbi huwa makali hivyo huwa na wakati mgumu.

Hata hivyo, shughuli kubwa za kujiingizia kipato kwa wananchi wa Kijiji cha Buyuni ni kilimo na uvuvi, lakini kutokana na changamoto ya wao kuishi ndani ya hifadhi mazao yao huwa yanaliwa na wanyama.

Akizungumzia adha wanayokumbana nayo wanakijiji hao, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Diwani Akida anakiri kuwapo kwa jambo hilo na kwamba kijiji hicho kilitakiwa kuhamishwa kutokana na kuwa ndani ya hifadhi lakini mpaka sasa jambo hilo halijafanyika.

“Changamoto zilizopo hapa ni nyingi, hivyo jambo la msingi ni kuhama kutoka hapa tulipo licha ya kwamba hifadhi imetukuta.

“Tuliiomba Serikali itutafutie makazi sehemu nyingine, sisi tuko tayari kuhama kwani matatizo tunayokumbana nayo ni mengi, ukiacha suala la maji pia tunakoswa koswa kuliwa na wanyama ambao wakati mwingine hupita hadi kwenye nyumba zetu,” anasema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, anaushukuru uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Saadan kwa kuwapa maji kila mwezi, jambo ambalo kwa kiasi fulani linawapunguzia ukali wa tatizo hilo.

Kwa upande wake Mhifadhi wa Saadan, James Wakibala anasema anatambua uwapo wa kijiji hicho ndani ya hifadhi.

Anasema anawahurumia watu wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo kwani kuishi karibu na wanyama ni jambo la hatari mno.

Anakiri kwamba hifadhi hiyo imekikuta kijiji hicho na kwamba wao wapo tayari kuwahamisha kama watakubali kwa kuwa wao ndio wamewafuata.

“Sisi tulikuwa tayari kugharamia uhamisho wao kutoka hapa, lakini tatizo lilopo ni kwamba wananchi wenyewe walikataa,” anasema Wakibala.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela anasema anatambua uwapo wa kijiji ndani ya hifadhi ya Saadan na kwamba Serikali ilishatoa agizo wahamishwe hasa ukizingatia kuwa hakuna huduma muhimu za kijamii.

Anasema ni wajibu wa Serikali kuwasaidia wananchi wake hasa katika huduma muhimu kama maji, afya na elimu, hivyo anaitaka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kutenga eneo kwa ajili yao.

“Hili jambo nitalifanya kwa haraka, nitazungumza na waziri husika ili mchakato uende kwa haraka zaidi. Hatuwezi kuona wananchi wetu wakitaabika na kuishi hatarini,” anasema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles