27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

UKWELI KUHUSU SINDANO ZA UZAZI WA MPANGO

 

 

Na JOACHIM MABULA,

WATU wengi leo hii hupenda kufanikiwa maishani. Wengi wakiwa na utajiri na wenzi bora wa maisha kitu kikubwa wanachokitamani ni kuzaa na kuwa na familia yenye furaha. Ili uwe na familia bora ni vyema pia kuzingatia mpango wa uzazi na si kufululiza kuzaa. Baadhi ya wanawake wamechagua sindano za uzazi wa mpango kama njia yao ya kupanga uzazi. Sindano za uzazi wa mpango ni sindano za homoni zinazochomwa ili kuzuia mimba.

Sindano za uzazi wa mpango zina homoni aina moja tu ya projesteroni. Kuna aina tofauti tofauti za sindano za uzazi wa mpango mfano Noristeral inayozuia mimba kwa wiki nane, Depo Provera inayozuia mimba kwa wiki 12 na Sayana Press inayozuia mimba kwa wiki 13. Aina kuu inayotumika nchini Tanzania ni Depo-Provera. Sindano hizi huwa na homoni za projestini aina ya Depot Medroxyprogesterone Acetate (DMPA au Depo Provera) inayofanana na homoni asilia ya projesteroni inayopatikana kwenye mwili wa mwanamke.

Sindano hizi hazina homoni ya Istrojeni hivyo inaweza kutumika kipindi chote ambacho mama ananyonyesha ikiwa hawezi kutumia njia ya uzazi wa mpango yenye homoni ya Istrojeni. Hufanya kazi kwa miezi mitatu, hivyo mwanamke atachoma sindano hii kila baada ya miezi mitatu baada ya kila sindano atakayochoma. Sindano huanza kufanya kazi saa 24 baada ya kuchomwa.

Zinavyofanya kazi

Sindano za uzazi wa mpango zinafanya kazi kwa kuzuia mayai kutoka kwenye ovari (kokwa), hufanya ute/utando mzito kwenye seviksi (shingo ya kizazi) unaozuia mbegu za kiume kuingia kwenye uterasi, pia hufanya mirija icheleweshe kupitisha mayai.
 
Ufanisi wake

Sindano za Depo Provera zinazuia mimba kwa asilimia 97 kwa wale wasiozingatia matumizi sahihi, kuna uwezekano wa mimba tatu katika wanawake 100 wanaotumia sindano hizi. Zikitumiwa vizuri yaani kwa kawaida na kwa muda muafaka zinaweza kuzuia mimba kwa asilimia 99.

Watumiaji

Mwanamke yeyote aliyethibitika kutokuwa na ujauzito anaweza kuanza kutumia sindano wakati wowote, wenye umri wowote, vijana na wenye umri zaidi ya miaka 40. Ingawa kwa wanawake chini ya miaka 18 wanapaswa kuchunguzwa vizuri kabla ya kutumia sindano za uzazi wa mpango kwa kuwa wako katika ukuaji na wakati mwingine sindano hizi huathiri mifupa. Zinatumika kwa wanawake waliozaa na ambao hawajazaa, waliolewa na wasiolewa, walioharibu mimba, wanaovuta sigara na wasiovuta, walio na VVU na wasio na VVU, wanawake wenye shinikizo kubwa la damu (High blood pressure) na wasio na shinikizo kubwa la damu na walio na wasio na ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell Disease). 

Maudhi yake

Kwa miezi michache ya mwanzo mwanamke atapata mzunguko wa hedhi usio wa kawaida. Baada ya mwaka wa matumizi ya sindano inakadiriwa kuwa asilimia 40-50 hukosa hedhi, asilimia 80 hukosa baada ya miaka mitano ya matumizi. Kuongezeka uzito kilo moja hadi mbili kila mwaka, kuumwa kichwa, kushuka moyo (depression).

Fikra potofu za watumiaji

Sindano zinasababisha hedhi ya kila mwezi kuacha na kusababisha matatizo makubwa, ukweli ni kwamba kukosa hedhi wakati unatumia sindano za uzazi wa mpango hakuna madhara ni kama tu kutopata hedhi wakati ukiwa mjamzito. Ikiwa huoni siku zako wakati unatumia sindano, hivyo watu hudhani kuwa hujikusanya ndani ya mwili wa mwanamke, ukweli ni kwamba damu haijikusanyi mahali popote. 

Wanadhani kuwa sindano ya uzazi wa mpango inaweza kutumika kutolea mimba, ukweli ni kwamba sindano za uzazi wa mpango haziwezi kutoa wala kuharibu mimba iliyoingia tayari. Dhana ya kwamba sindano hizi humfanya mwanamke kuwa mgumba, si kweli na wala huwa haiharibu kizazi.

Muda wa kutunga mimba baada ya kuacha

Mzunguko wa hedhi unaweza kubadilika ndani ya mwaka mmoja wa matumizi ya sindano hizo. Mara nyingi siku za hedhi huwa bila mpangilio na damu hutoka kwa wingi au siku za hedhi huwa chache zaidi na damu kutoka kidogo au kuacha kabisa kupata hedhi. Matatizo haya yanaweza kutulia baada ya mwaka wa kwanza, lakini yanaweza yakaendelea ikiwa homoni iliyochomwa bado iko ndani ya mwili wako. 

Inaweza kuchukua muda mrefu kwa siku zako na kizazi chako asilia kurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kuacha kutumia sindano za uzazi wa mpango. Huchukua kati ya wiki nane hadi 12 kwa homoni ya projesteroni iliyochomwa kuondoka mwilini, lakini unaweza ukalazimika kusubiri zaidi kwa mzunguko wako wa hedhi kurudi katika hali yake ya kawaida ikiwa unajaribu kupata mimba. Kwa baadhi ya wanawake huwachukua miezi mitatu hadi mwaka kwa hedhi yao kuwa katika hali yake ya kawaida. Itakuwa vigumu sana kupata mimba hadi pale utakapokuwa unapata hedhi yako iliyo katika mpangilio mzuri kila mwezi.
 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Habari,sorry naomba kupata majibu mm nimechoma hiyo sindano moja tu mwezi wa 5 mwaka huu na miezi mitatu imepita lkn nashangaa sasa sioni siku zangu,hapo nyuma zilitoka sana na kwa muda mrefu ila kwa sasa hazitoki tena naomba ushauri

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles