25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

SCHAMICA STEVENSON: MAMA SHUJAA ANAYENYONYESHA AKIWA NA MAJERAHA YA MOTO

 

 

Na MWANDISHI WETU,

KUNA msemo usemao mama ndiyo kila kitu katika maisha. Mtoto anapokosa mama huwa mpweke hivyo kujikuta akiishi maisha asiyoyapenda.

Upendo wa mama hauwezi kufananishwa na kitu chochote kile, ndiyo maana wazee wanakwambia radhi ya baba inapoteza mawazo wakati ya mama inaua. Ukimdharau mama maisha yako ni lazima yatakuwa ya kubabaisha hapa ulimwenguni.

Schamica Stevenson maarufu kwa jina la Mimi (34) ni mwanamke aliyeungua moto mwili mzima lakini anadiriki kumnyonyesha mtoto wake wa pili licha ya uchungu anaoupitia.

Mimi anasema anafanya hivyo ili kuwahamasisha wanawake wengine ambao hawaoni umuhimu wa kunyonyesha watoto wao.

Mimi aliungua vibaya na moto akiwa na umri wa miaka miwili, nyumbani kwao katika Jimbo la Michigan, nchini Marekani.

Alipopata mtoto wa kwanza hakumnyonyesha akihofia majeraha aliyokuwa nao, lakini baada ya kujifungua mtoto wake wa pili aliamua kumpa haki yake ya kunyonya ziwa la mama.

''Nafanya hivi ili wanawake wenzangu wasikate tama iwapo wana matatizo, kama nilivyofanya mimi nikiwa na miaka 20,'' anasema Schamica na kuongeza:

''Kama matiti yanafanya kazi, basi yanastahili kutumika kwa kuwanyonyesha watoto.''

Katika ajali hiyo ya moto uliosababishwa na sufuria ya maji yaliyokuwa yakichemshwa jikoni, Mimi alimpoteza kaka yake ambaye alikuwa na miaka minane.

Mimi anasema kuwa mama yao alishindwa kuwaokoa kutokana na chuma zilizokuwa madirishani.

Anasema amekuwa akifanyiwa upasuaji wa ngozi mara kwa mara katika maisha yake, hali iliyomfanya awe na wasiwasi wa  kubeba ujauzito, pindi alipofikisha umri wa miaka 20 kutokana na alama alizokuwa nazo tumboni.

Mimi, ambaye kwa sasa anafanya kazi ya ukaguzi msimamizi wa afya, anasema mara ya kwanza hakunyonyesha licha ya kwamba alitamani kufanya hivyo.

“Nilikuwa mdogo na sikuwa na uvumilivu wa kustahimili maumivu kwa wakati huo. Ila huyu mtoto wangu wa pili niliamua kujaribu kumnyonyesha baada ya kumuona wifi na binamu yangu wakifanya hivyo kwa watoto wao,” anasema Mimi.

Anasema alikuwa na maziwa kidogo hivyo ilimlazimu kutumia pampu na sirinji kabla ya kumpa mtoto titi.

''Muuguzi wa unyonyeshaji alinisaidia mno pindi nilipokuwa hospitalini,” anasema.

“Nakumbuka muuguzi aliniambia hali hii itakuwa ngumu huku akijaribu kulitoa na kulifinya titi langu.

“Nilikamua maziwa baada ya saa tatu na baada ya kula nikiwa bado hospitali, lakini sikuwa napata maziwa mengi,” anasema.

Mimi anasema alikuwa akifanyiwa upasuaji wa ngozi kila mwaka huko Cincinnati hadi alipofikisha miaka 17.

Licha ya kuwa na alama mwilini, Mimi anatumia picha zake anazonyonyesha kuhamasisha wanawake wengine kujivunia miili yao.

“Inanivunja moyo nikisikia mtu anajitoa uhai kutokana na sura zao zilizoathirika na majanga mbalimbali,” anasema na kusisitiza kuwa yeye hajali lolote na kwamba anatembea kila mahali akijilinganisha na mwanamuziki Beyonce au Tamar Braxton.

Anaongeza: “Sikupata ujasiri kwa siku moja, lakini najivunia kuwa mjasiri kwa sasa. Kuna wakati nilijihisi mnyonge kwa sababu mimi ni binadamu, lakini narudi na kumshukuru Mungu kwa maisha yangu na watoto wangu ambao niliweza kujifungua na kuwalea.”

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles