22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

KIFO CHA SRIDEVI KAPOOR KINAPOIUMBUA BOLLYWOOD

NA RAS INNO NGANYAGWA


INAWEZEKANA wengi mnaoshabikia muvi za Kihindi za Bollywood mnahisi kwamba ‘Mastaa’ wanaoigiza filamu hizo wana mtelezo wa ganda la ndizi.

Lakini ukweli uko kinyume hususan kwa waigizaji wa kike kutokana na yaliyodhihirika kufuatia kifo cha mwigizaji nyota, Sridevi Kapoor, kilichoitikisa si India tu lakini dunia nzima kwa ujumla.

Kwani njia zinazokifu hutumika kuhakikisha waigizaji wanaendelea kuonekana vijana siku zote lakini pia fursa za kuigiza katika muvi za bajeti kubwa zinazovutia hupatikana kwa mlungula ukiwamo wa ngono.

Inayoambatana na uhalifu ukiwamo wa matumizi ya uraibu usiofaa na unyanyasaji wa kijinsia sanjari na mahusiano tata yanayoibuka na kuvunjika baina ya waigizaji, waongozaji, wazalishaji na wanahusika wengine wa tasnia ya filamu za Bollywood.

Sridevi amekufa kama alivyofariki Whitney Houston miaka sita iliyopita kutokana na kulewa uraibu aliokuwa akiutumia na kushindwa kujimudu kwa kuzama bafuni.

Lakini kwa waigizaji hususan wa kike wa India ambao wanaonekana wenye furaha na mvuto adimu mbele ya kamera kuna mengi nyuma yake ukiwemo msongo wa mawazo kwa yanayowasibu yasiyofahamika kwa mashabiki wao.

Sridevi hakupata nafasi ya kukua kama watoto wengine na kuufurahia umri wake wa utotoni kutokana na presha ya kuanza kuigiza akiwa na makamu madogo, amepitia mengi yanayohusu shinikizo kutokana na kuwa ‘staa’ katika umri mdogo.

Ambayo alijaribu kuyaficha ili alinde taswira anayoiakisi kwenye filamu tofauti na uhalisia halisi.

Kuna kubwa ambalo Sridevi amekuwa akilikana bila tuhuma hizo kuthibitishwa kwamba naye ni miongoni mwa waigizaji aliyefanya operesheni nyingi ili kulinda wajihi wake na kutopoteza mvuto ili aonekane kijana siku zote.

Katikati ya yote hayo ni mapambano ya kuhimili utafutaji fursa dhidi ya waigizaji nyota ambao ni watoto wa waigizaji maarufu wa zamani ambao ni wazaliwa wa mijini wenye viwango vikubwa vya elimu. Ingawa pia watoto wa kimasikini wanaoinukia na kujizolea umaarufu kwenye tasnia hiyo hukubalika kwa uwezo wao lakini hunyanyapaliwa na kutendewa madhila mengi ili wapate nafasi za uigizaji nyota licha ya wengi kufanikiwa na kutambulika kimataifa wakiwemo Shah Rukh Khan, Anushka Sharma, Ranveer Singh na Deepika Padukone ambao mafanikio yao huanzia kwa watengenezaji filamu wanaoamini katika uwezo na siyo kaliba anayotokea mwigizaji anayechipukia.

Mengi yatasemwa baada ya kifo chake kuhusiana na tasnia ya Bollywood lakini ukweli utabakia kuwa Sridevi hayupo tena duniani na mashabiki wake ‘watam-miss’ sana, hata wale ambao hawakuwa wanaamini kwamba amefariki wanalazimika kukubali ukweli huo baada ya maziko yake yaliyofanyika Mumbai siku tatu zilizopita.

Ripoti ya uchunguzi wa matabibu inabainisha kwamba amefariki kwa matatizo ya mshtuko wa moyo akiwa anaoga hivyo kushindwa kujimudu na kuzama bafuni.

Licha ya juhudi za mumewe aliyeambatana naye kwenye harusi ya mpwa wa Sridevi huko Dubai kujaribu kumwokoa akishirikiana na rafiki yake, walipolazimika kuvunja mlango wa bafuni na kumpa huduma ya kwanza ili aweze kupumua baada ya kumkuta amezama kwenye bafu, lakini hawakufanikiwa ndipo walipolazimika kuwataarifu polisi majira ya saa tatu usiku wa Februari 24.

Sridevi (54) ambaye jina lake halisi ni Shree Amma Yanger Ayyapan mzaliwa wa Tamil Nadu jimbo la Kusini mwa India alianza kujitosa kwenye uigizaji akiwa na umri wa miaka minne.

Akafanikiwa kutoboa katika Bollywood miaka kumi na moja baadaye kwa kuigiza filamu ya ‘16 Springs’ kabla ya kuibuka tena kwenye filamu iliyoandaliwa na Balu Mahendra ‘Shock’ na baada ya hapo akaendelea kung’ara katika filamu mbalimbali zikiwemo: “Chaalbaaz’ ‘Lamhe’ ‘Himmatwala’ ‘Chandni’ na ‘Mr India’.

Sridevi aliolewa na mtayarishaji filamu nguli Booney Kapoor (62) mnamo mwaka 1996 na kubahatika kupata mabinti wawili Janvhi (20) na Kushi (17). Katika maisha yake ya uigizaji amewahi kutunukiwa tuzo ya kutukuka ya taifa la India kutokana na mafanikio yake.

Kifo chake kimeigubika India na kupelekea Waziri Mkuu Narendra Modi kutoa kauli: “Nimesikitishwa na kifo cha mwigizaji wetu nguli ambaye ushiriki wake kwenye uigizaji ulitupatia taswira mtambuka kuhusu maisha yetu, rambirambi zangu kwa familia yake na mashabiki wote kutokana na huzuni ya msiba huu mkubwa,”.

Maziko yake yalihudhuriwa na umati mkubwa wa mashabiki waliojipanga barabarani kuupokea mwili wake uliowasili kutoka Dubai na katika hali ya huzuni iliyogubika waombolezaji, polisi walikuwa na kazi ya ziada kudhibiti umati mkubwa uliojitokeza huku Sridevi akipewa heshima ya kitaifa kwa gari lililobeba maiti yake kufunikwa bendera ya taifa na kupigiwa mizinga kabla ya shughuli ya kuuchoma moto mwili huo katika taratibu za maziko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles