22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

KAMA HUNA UKITAKA UNA NAFASI YA KUPATA

Na ATHUMANI MOHAMED


WENGI wetu hatujui jambo moja muhimu sana kwenye maisha; ukiwa kwenye wakati mgumu zaidi, ndipo unakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kuliko ukiwa kwenye hali nzuri.

Ogopa sana mtu mwenye changamoto. Ubongo wake haulali, anawaza na kuwazua. Hebu vuta picha; siku ambayo uliamka asubuhi ukiwa huna hata mia mfukoni, una familia na hujui cha kufanya. Je, familia yako ililala njaa?

Tafakari kwa makini. Fikiria siku ambayo ulikwenda mjini, ukajikuta umeibiwa au umepoteza fedha zako zote, huna nauli na muda umekwenda na unatakiwa kurudi nyumbani. Je, ulirudi kwa miguu?

Bila shaka nikiruhusu watu watoe ushuhuda wao kuhusiana na hili, kila mtu atasema lake lakini wengi watakueleza mambo ya kushangaza, kuhusu namna walivyopata fedha za chakula nyumbani au nauli ya kurudi nyumbani baada ya kukwama.

Kuna watu ni mabingwa wa kulalamika maisha magumu… haitakusaidia kitu. Unalalamika nini? Maisha magumu sawa, sasa? Upewe hela za bure? Hakuna vya bure. Wapo wanaolalamikia wazazi wao kwamba hawajawasomesha, ndiyo maana maisha kwao yamekuwa magumu, siyo sahihi.

Utajikuta unalalamika karibu robo tatu ya maisha yako na siku ukija kushtuka, tayari umeshakuwa mzee na huna cha kufanya tena ili kujikwamua kiuchumi. Wakati ukiwa kijana, akili yako ikiwa na uwezo mkubwa wa kuchaji, ndiyo wakati unaotakiwa kuumiza ubongo sana ili utoke kwenye umasikini.

UMASIKINI KIPIMO CHA AKILI

Kama umezaliwa kwenye familia tajiri, huna mambo ya kufikiria ya kukuumiza kichwa. Huu ni ukweli utakaowaumiza wanaotoka familia bora, lakini wengi wao hawaumizi vichwa vyao. Uani kwao magari kibao, chakula cha uhakika, baba ana biashara kibao, zaidi anasubiria urithi tu.

Hii ndiyo sababu familia nyingi zenye uwezo, baba anapoondoka na kuacha miradi yake, mara nyingi huwa haina maisha marefu. Hiyo ni kwa sababu walioachwa hawakufundishwa namna ya kuendesha miradi hiyo.

MATAJIRI WENGI WALIANZIA UMASIKINI

Ni vile wengi hatufahamu, lakini ukweli ni kwamba matajiri wengi wametokea kwenye ufukara wa kutisha. Fuatilia historia za matajiri wengi, wafanyabiashara, utagundua wengi walianzia chini kabisa.

Hasira za maisha magumu, kulala chini, kudharauliwa shuleni, kukosa mavazi, kuishi nyumba za kupanga nk, ndiyo vitu vilivyowatesa maishani mwao kiasi cha kutamani mafanikio maishani.

Kumbe basi, huna sababu ya kulalamikia maisha magumu badala yake unapaswa kuchukulia ugumu huo kama changamoto kwako ya kusaka njia za namna ya kutoka kimafanikio.

SHIDA ZIKUFUNZE

Ikiwa unaishi nyumba ya kupanga mpaka sasa, iwe ni hasira kwako ya kuhifadhi fedha kidogokidogo ili uweze kununua kiwanja na baadaye ujenge. Acha maneno ya wakatisha tamaa. Viwanja bado vinapatikana kwa bei nafuu kwa maeneo ya nje kidogo ya mji.

Mfano kwa maeneo ya Dar es Salaam, viwanja bado vinapatikana hadi kwa Tsh. Milioni tatu au zaidi kidogo kwa maeneo ya Kibamba, Bunju, Kiluvya, Banana, Kigamboni, Charambe na sehemu nyinginezo, tena kwa kulipa kwa awamu.

Ukiwa na milioni moja na nusu leo hii, una uwezo wa kumiliki kiwanja chako hata kama ni kidogo, kisha ukaendelea kumalizia deni kidogokidogo. Huko mikoani ni rahisi zaidi, ukiwa na milioni unapata kiwanja nje kidogo ya mji.

Baada ya muda mfupi utamaliza na utaingia kwenye hatua ya pili ya kujenga. Kujenga napo ni hatua, utaanza na matofali kisha vifaa vingine na baada ya muda fulani, utaanza ujenzi hata kama ni kwa awamu. Usifikirie kujenga ni gharama kubwa sana kiasi cha kukutisha na kukukatisha tamaa.

Ikiwa huna gari, basi weka hasira zako hapo. Mimi namfahamu mtu ambaye aliweka malengo ya kununua gari kwa miaka mitatu na kweli baada ya muda huo akanunua gari lake – hakukopa!

Kila kitu ni mipango, itoshe kukupa somo kwamba, changamoto zako ndiyo petroli ya kukuwashia moto kuelekea kwenye mafanikio kwa kuweka malengo yako.

Kwa leo somo letu linaishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!

Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,283FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles