31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

BASILA ANA MLIMA MREFU WA KUPANDA MISS TANZANIA

NA CHRISTOPHER MSEKENA


HASHIM Lundenga maarufu kama  Anko Lundenga ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino International Agency iliyokuwa na dhamana ya kuratibu na kusimamia mashindano ya Miss Tanzania tangu mwaka 1994, ameachia ngazi katikati ya wiki hii.

Mikoba yake imechukuliwa na Basila Mwanukuzi Mkurugenzi wa Kampuni ya The Look Limited, ambayo sasa ina jukumu la kuratibu na kusimamia mashindano hayo makubwa ya urembo nchini.

Swali ambalo mashabiki na wadau wa fani ya ulimwende nchini wanajiuliza mpaka sasa ni kama Miss Tanzania iliyoanguka mikononi mwa Lundenga inaweza kuinuliwa na Basila Mwanukuzi ambaye ni mrembo namba moja katika shindano hilo mwaka 1998.

INAFAHAMIKA

Katika miaka ya hivi karibuni mashindano ya Miss Tanzania yamekuwa yakipitia changamoto nyingi zinazoacha picha mbaya mbele ya jamii.

Itakumbukwa mwaka 2014 mashindano hayo yalifungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa baada ya kushindwa kufuata taratibu na kanuni za shindano kiasi cha kumpa ushindi Sitti Mtemvu, mrembo ambaye aliandamwa na skendo ya umri mkubwa kisha kupokwa taji na kukabidhiwa kwa aliyekuwa mshindi namba 2, Lilian Kamazima.

Hali kadharika shindano hilo liliendelea kupoteza heshima kwenye jamii kufuatia matukio mengi yenye viashiria vya ukosefu wa maadili kiasi kwamba ilionekana tasnia ya ulimbwende ni uhuni na si jukwaa la kuibua watu muhimu kwenye jamii.

Lakini pia kashfa za kupanga matokeo, malalamiko kutoka kwa washiriki ni miongoni mwa changamoto ambazo zilimuumiza Basila Mwanukuzi na kumsukuma kujitosa kuyaendesha mashindano hayo.

CHANGAMOTO NYINGINE

Anko Lundega anasema kitu chochote kikifungiwa ni ngumu kurudi tena ndiyo maana baada ya kufungiwa mwaka 2014, walishindwa kurudi kwa kishindo.

Walishindwa kutoa zawadi kwa wakati kwa Miss Tanzania 2016/17, Diana Edward aliyetwaa taji hilo Octoba 29 mwaka 2017 kisha zawadi yake ambayo siyo ile iliyoonyesha jukwaani siku aliposhinda akaja kupewa gari aina ya Suzuki Swift, Mei 11 mwaka jana.

Kitendo hicho kilimfanya Waziri mwenye dhamana  na sekta ya sanaa, Dk. Harrison Mwakyembe kuwataka waandaaji wa shindano hilo kujipanga na kuacha ubabaishaji wa kuwacheleweshea zaidi washindi.

Endapo watataka kuendesha hayo mashindano nitahitaji zawadi ya mshindi wa kwanza kama ni gari iletwe ofisini kwangu niione na waniachie funguo yake pia zawadi ya mshindi wa pili hivyo hivyo ndipo nikaporuhusu.

“Maana kila mwaka zawadi ya mshindi wa kwanza imekuwa ikisumbua kutolewa kwa muhusika. Sasa huo mchezo hapana, hatuwezi kuona ukiendelea, ubabaishaji siyo kwa Tanzania ya leo,” alisema Mwakyembe.

Changamoto zilipozidi shindano la Miss Tanzania lilifikia hatua mbaya ya kuteua badala ya kushindanisha warembo wa kuwania taji la Miss World huko Sanya, China.

Mrembo Julitha Kabete ambaye alikuwa kwenye tano bora ya Miss Tanzania mwaka 2016 aliteuliwa mwaka jana na kamati ya Miss Tanzania kutuwakilisha kwenye mashindano ya Miss World kitendo kilichoendelea kuonyesha udhaifu mkubwa wa waandaaji wa mashindano hayo ya urembo.

MAFANIKO MAKUBWA

Licha ya Anko Lundenga kuachia ngazi kwa sababu kadhaa ikiwamo ya umri wake kumtupa mkono pamoja na kukosa mawazo mapya yenye tija kwenye sekta ya urembo, katika uongozi wake amefanikiwa kutoa warembo wenye ‘impact’ chanya kwenye jamii.

Mrembo kama Nancy Sumari ambaye alikuwa mshindi mwaka 2005, ndiyo mshiriki pekee toka mashindano hayo yaanzishwe kuingia kwenye 6 bora ya warembo wa Dunia.

Warembo Hoyce Temu, Happiness Magese, Angela Damas, Faraja Kotta (Nyalandu), Nancy Sumari, Wema Sepetu, Flaviana Matata, Lisa Jensen, Happiness Watimanywa  wamekuwa na mchango mkubwa kwenye jamii kupitia shughuli zao mbalimbali.

MISS TANZANIA AONGEA

Swaggaz lilimtafuta mshindi wa shindano hilo msimu wa mwaka 2016/17, Diana Edward ambapo naye ametoa maoni yake baada yaametoa maoni yake

“Kwangu mimi ni watu ambapo walinisapoti, watu walionifikisha nilipo kwa hiyo kwa upande wangu nimeumia sababu walikuwa ni watu wazuri hata kama walikuwa na mapungufu yao kwa upande mwingine ni vizuri kwa sababu wamempa mtu ambaye ana uzoefu na mambo ya urembo na amekuja na nguvu mpya,” alisema Diana.

MLIMA MREFU WA KUPANDA

Basila ambaye sasa ni mratibu na mwendeshaji wa mashindano hayo kuanzia Februari 23 mwaka huu hana skendo wala kashfa yoyote toka alipotangazwa mshindi hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kuirudisha taswira njema ya  Miss Tanzania.

Japo kuwa ana kibarua kizito cha kuhakikisha masuala ya zawadi, nidhamu kwa washiriki na mengine mengi yaliyodhoofisha shindano hilo yanafanyiwa kazi chini ya uongozi wake yasijirudie.

Si jambo baya kuwatumia warembo waliowahi kushinda taji la Miss Tanzania miaka ya nyuma kama Nancy Sumari, Flaviana Matata, Jacqueline Mengi, Faraja Kotta, Happiness Magese na wengine kama hao katika michango ya mawazo ili kuboresha shindano.

Ikumbukwe kuwa kilichompa mafanikio Lundenga enzi zake alikuwa na timu na kamati  yenye nguvu kiasi cha kuwavutia wawekezaji wengi mpaka viongozi wakuu wa nchi walilipenda shindano hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles