23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

KIDATO CHA KWANZA KUPIMWA KWA MITIHANI

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza kuwafanyia upimaji maalumu wa stadi na maarifa wanafunzi waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za serikali.

Barua iliyosainiwa na Edigar Kasuga kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo kwenda kwa Makatibu Tawala Tanzania Bara, imeeleza mtihani huo maalumu utafanyika Februari 28, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kasuga, wanafunzi ambao watashindwa kuonyesha uwezo wao katika udahili huo wataondolewa shuleni.

“Katika taarifa ya matokeo ya mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi 2016 (PSLE) iliyotolewa na Katibu Mtendaji Oktoba 27, mwaka huu, pamoja na mambo mengine, Baraza lilielekeza kuwa  wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2017, watapimwa  kubainisha usahihi wa uwezo waliouonyesha katika mtihani huo.

“Wanafunzi wote watakaobainika kutokuwa na uwezo stahiki na  walifaulu mtihani kwa udanganyifu wataondolewa shuleni,” alisema.

Aliongeza:  “Baraza linawajulisha kuwa litafanya upimaji maalumu wa stadi na maarifa kwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za umma ifikapo Februari 28, mwaka huu”.

Aliwataka makatibu tawala kuwasilisha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule za umma kwa mfumo maalumu waliopewa.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba MT/ E/16/191/VOLXXIV/103  iliyotolewa Februari 6, mwaka huu, mfumo huo unamtaka katibu tawala kujaza jina la mkoa, halmashauri, jina la shule na idadi ya wanafunzi.

“Takwimu zimfikie Katibu Mtendaji kabla ya au ifikapo Februari 10, mwaka huu. Tafadhali maofisa elimu sekondari na wakuu wote wa shule za umma wajulishwe ipasavyo. Nawatakia kazi njema,” alisema Kasuga.

Ili kupata ufafanuzi zaidi kuhusu jambo hili, MTANZANIA lilimtafuta Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Chalres Msonde.

Awali simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa hali iliyomlazimu mwandishi kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi.

Hata hivyo ujumbe huo haikujibiwa na baadaye simu yake haikupatikana hewani hadi tunakwenda mitamboni.

Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA lilimtafuta Ofisa Uhusiano wa Baraza hilo, John Nchimbi hata hivyo naye simu yake haikupatikana.

Akitangaza matokeo, Oktoba, mwaka jana, Dk. Msonde alisema yalionyesha Mkoa wa Geita ndiyo ambao uling’ara kwa kushika nafasi ya kwanza katika taifa.

Ufaulu wa jumla ulipanda kwa asilimia 2.52 ikilinganishwa na mwaka juzi ambao ulikuwa asilimia 67.84.  Mwaka huu ni asilimia 73.50, wavulana wakifanya vizuri kwa kushika nafasi tisa katika 10 za kwanza (kumi bora), huku msichana akishika nafasi ya nne katika orodha hiyo.

Watahiniwa 795,739 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wasichana wakiwa 422,864 sawa na asilimia 53.14 na wavulana 372,875 sawa na asilimia 46.86. kati yao 811 walikuwa na uono hafifu na 95 walikuwa ni wasioona.

Matokeo hayo yalionyesha   watahiniwa 555,291 kati ya 795,739 ambao walisajiliwa walifaulu mtihani huo.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde, idadi ya watahiniwa waliofaulu ilikuwa ni   asilimia 70.36, kati yao wasichana ni 283,751 ambao ni   asilimia 67.59 na wavulana ni 271,540,   asilimia 73.50. Mwaka jana watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 67.84,hivyo kuna ongezeko la asilimia 2.52.

Dk. Msonde, kwa mara ya kwanza liwataja hadharani baadhi ya wamiliki wa shule, walimu wakuu na wasimamizi waliohusika na vitendo vya udanganyifu wakati wa mtihani huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles