30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

… GWAJIMA: NITAPAMBANA NA MAKONDA

PATRICIA KIMELEMETA NA ASHA BANI, DAR ES SALAAM

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ametangaza vita kati yake na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Amedai ni kwa vile Makonda  amemdhalilisha baada ya kumtangaza kuwa miongoni mwa watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Vilevile amemuomba Rais Dk. John Magufuli kumuondoa kwenye  ukuu wa mkoa.

Gwajima amedai ni kwa sababu  RC Makonda ameshindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo na kuanza kujenga chuki na watu asiowapenda.

Alikuwa akizungumza jana na waumini wake waliohudhuria ibada ya Jumapoli katika Makao Makuu ya Kanisa la Uzima na Ufufuo,   Ubungo   Dar es Salaama.

 Gwajima alilaani kitendo cha kuhusishwa na dawa za kulevya akisema  kitendo hicho kimemdhalilisha yeye, familia na kanisa lake.

“Nimeamua kujitokeza hadharani   kutangaza vita kati yangu na Makonda kwa sababu amenidhalilisha sana kwa kunitangaza hadharani kuwa mimi ni miongoni mwa washukiwa wa dawa za kulevya.

“Sitakubali katika hili…narudia tena, sitakubali… nitakachokifanya ni kumuomba Rais John Magufuli kwa sababu ni mteule wake, kumpangia kazi nyingine,  hii alionayo haimfai,”alisema Askofu Gwajima.

Hata hivyo alimuomba  Rais Dk. Magufuli asikate tamaa kwa uamuzi wake wa kuwachagua vijana kushika nafasi mbalimbali za uongozi kwa sababu si vijana wote wenye akili kama za Makonda.

 “Rais hajamtuma huyu dogo kufanya anayoyafanya…bali ni akili zake yeye mwenyewe ambazo zimempeleka kufanya hivyo.

“Nina imani Rais Magufuli anahitaji msaada wangu katika hili ili aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo na mimi nipo tayari kumsaidia huku nikihakikisha kuwa Makonda anaondoka kwenye nafasi hiyo,” alisema.

Alisisitiza  kuwa hataki Rais Dk. Magufuli amfukuze kazi, bali anapaswa kumtafutia kazi nyingine ikiwezekana apewe nafasi nyingine katika Jeshi la Polisi au akasome katika Chuo cha Polisi (CCP)   Moshi mkoani Kilimanjaro.

Askofu Gwajima pia alisimulia tangu aliposhikiliwa na jeshi la polisi  baada ya kuwasili kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita, kuitikia wito uliotangazwa na Makonda wa kuwatak kuripoti   Ijumaa,

 Alisema   Jumatano iliyopita akiwa katika helikopta yake akienda  Dodoma   kukagua makanisa yake, alipata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba alikuwa anahitajika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akidaiwa anajihusisha na mtandao wa dawa za kulevya.

Alisema alishtuka na kuwaambia wasaidizi wake  waliokuwamo kwenye helkopta hiyo kwamba hilo ni zege halilali na Ijumaa ni mbali hali.

Gwajima alisema aliamua  kuahirisha ziara yake Dodoma na kurejea Dar es Salaam kwa mahojiano na polisi.

“Ilipofika asubuhi nilikwenda kituo cha polisi kama ilivyoelekezwa, sikungoja Ijumaa na nilimkuta mwarabu, sijui mhindi mmoja hivi ambaye aliniuliza wewe ndiyo Askofu nikamwambia ndiyo…. na mimi nikamuuliza wewe ndiyo mfanyabiashara Manji akanijibu ndiyo na ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kukutana hapo,’’ alisema na kuongeza:

 

‘’Nilitoka na kuingia ndani.  Usiku tulichukuliwa mimi na Yusuph Manji, mfanyabiashara huyo,  na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupimwa damu”.

Alisema baada ya hapo wakaandika ripoti pamoja na kukabidhiwa cheti cha uthibitisho wa kuwa hakuna walichokikuta.

  Gwajima alisema polisi pia walikagua akaunti ya kanisa na ya kwake binafsi, huku wakimuuliza   kwa nini ana fedha nyingi.

Alisema  aliwajibu kuwa fedha hizo ni sadaka na kazi yake ya kutunga vitabu na usambazaji wa vitabu vyake vya neno la Mungu nchi nzima.

“Stock yangu kwa sasa ina vitabu milioni 20 na ninaviuza nikichapa kwa waumini wangu… vyote ni shilingi ngapi?  Mimi ni mwalimu pia akae akijua,’’alisema Gwajima.

Alisema    kanisa lake kwa upande wa Dar es Salaam  lina   waumini 70,000 , kila mmoja akiamua kutoa Sh 1,000 kama sadaka   anaweza kuingiza Sh milioni saba na kama waumini hao wakitoa zaidi zitapatikana zaidi.

ATOA SHUKRANI

Askofu Gwajima alisema   kanisa lake ni miongoni mwa makanisa yanayopiga vita   dawa za kulevya.

Alisema atashirikiana na Serikali   kuhakikisha   vita hiyo inakwisha salama   pamoja na kuishauri serikali kutumia njia halali za kuwashtaki washukiwa wa dawa hizo ikiwa watabainika.

“Sikatai kwamba watu hawauzi dawa za kulevya, bali napinga njia zinazotumika kuwakamata siyo halali.

“Kwa sababu kama mtu ameficha dawa za kulevya halafu ukamtangaza kwenye televisheni si atachukua dawa zake na kuzificha.

“Makonda alipaswa kuwaita washukiwa   waweze kufika polisi na kufuata utaratibu mwingine wa sheria,” alisema.

DK. SLAA AIBUKA

Askofu Gwajima  aliwaambia waumini kuwa ametumiwa ujumbe mfupi kwa njia ya mtandao na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa.

Aliusoma ujumbe huo ukisema:  “Baba pole sana. Pamoja na mengine yote kwenye tukio hilo la dawa za kulevya wamekuonea na kukudhalilisha tu.

“Mungu yupo. Kwenye ukweli nilisema nitasimamia ukweli ninaouamini na siko tayari kuyumbishwa, wamekosea approach hata kama ni kwa kutaka uwataje wanaotumia. Mimi Dk. Slaa”.

  Gwajima aalisema alimjibu:  “Ninashukuru kwa ujumbe wako, nimepata meseji yako leo baada ya kuachiwa, asante”.

Dk Slaa alimjibu:  “Asante baba. Kwenye ukweli nitapiga kelele  hata mahakamani nipo tayari kuja kutoa ushahidi”.

KANISANI KWA GWAJIMA

Gwajima aliwasili kanisani kwake   saa 5.00 asubuhi huku akisindikizwa na walinzi wa kanisa hilo,   ulinzi ukiwa umeimarishwa.

Alipofika kanisani, waumini waliinuka na  kushangilia huku wakiwa na hamasa ya kutaka kujua kilichotokea   baada ya kutoka polisi.

Baada ya hapo, aliinuka katibu wa kanisa hilo na kutangaza kuwa  Askofu Gwajima yupo tayari kuzungumza na waumini wake kutokana na hali ya sintofahamu iliyojitokeza  wiki iliyopita baada ya kutangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa ni miongoni mwa washukiwa wa dawa za kulevya.

Alipomaliza kusema hayo, Gwajima aliinuka na kuwaambia waumini kuwa  majeshi ya bwana yamefika na wakae tayari kusikiliza yajiyojiri polisi.

Gwajima alitumia   saa moja kutoa ufafanuzi wa suala hilo na   baada ya kumaliza aliwaambia waumini wainuke na kumuombea Rais Magufuli na viongozi wenzake  huku wakiomba dua ya kumlaani Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles