28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

MFANYABIASHARA AMKATA MAPANGA MTALAKA WAKE

CHRISTINA GAULUHANGA NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA wa matunda aliyefahamika kwa jina moja la Jumanne, anatuhumiwa kumkatakata kwa mapanga mtalaka wake, mama Athuman, kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.

Tukio hilo lilitokea jana saa 5.00 asubuhi katika kituo cha mabasi Mkwajuni Kinondoni, Dar es Salaam,  baada ya Jumanne kufika eneo hilo akiwa na panga  na  kumkatamata aliyewahi kuwa mke wake ambaye alikuwa akiuza matunda pembezoni mwa kituo hicho.

Hali hiyo ilisababisha wananchi   jirani na kituo hicho wakiwamo madereva wa bodaboda,  kukimbia huku na kule kuhofia usalama wa maisha yao.

Hata hivyo, kondakta mmpja wa daladala  namba   T 138 DGL, Shaban Juma akiwa ndani ya gari hilo, aliamua kujitosa kwa kumrukia Jumanne na kumkaba shingo ili kunusuru uhai wa mwanamke huyo.

Akizungumza na MTANZANIA, Juma alisema aliingiwa na ujasiri huo baada ya kushuhudia mwanamke akikatwa mapanga hivyo  aliingiwa na uchungu na kuamua kujitosa kupambana  kunusuru maisha yake.

Alisema   mtuhumiwa alikuwa amegeuka mbogo  kwa sababu  alikuwa haonyeshi ubinadamu hata kidogo.

“Nilihisi huruma sana baada ya kuona mwanamke akishambuliwa kwa panga. Nilijisemea moyoni, hata kama simfahamu najitosa  mradi niokoe maisha yake, tena kibaya alikuwa mjamzito,”alisema Juma.

Alisema baada ya kumrukia na kumkaba mwamamume huyo ndipo watu waliokuwapo jirani walipomnyang’anya panga na  kumshambulia   hadi akazirai.

“Hadi sasa hatujafahamu hali yake kwa sababu wengine wanadai yule jamaa kafariki dunia na mtalaka wake amekimbizwa hospitali.

“Kikubwa tunawaombea wote wapate nafuu ila roho ilinuma kuona panga likiwa linatembea mwilini kwa mwanamke,”alisema Juma.

Alisema mwanamke huyo alikuwa tayari akivuja damu kwa wingi mikononi, kichwani na sehemu za shingo.

Shuhuda,  Lowasa Moleli, ambaye alikuwa akifanya biashara jirani na mama huyo alidai ugomvi kati ya watalaka hao ulianza jana.

Alidai  Jumanne  alifika na kumtuhumu mtalaka wake kuwa ana uhusiano na mfanyabiashara mwenzake.

 “Mwanaume huyo ambaye inadaiwa amezaa naye watoto wanne, alimwambia kwa sauti kuwa ‘utanitambua’,”alisema Mollel.

Alisema kitendo cha shambulio hilo kilidumu zaidi ya robo saa na kusababisha eneo hilo kuwa dimbwi la damu.

  Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkunguni ‘A’ Hananasif, Reubern Luhongole alisema  hajapokea taarifa sahihi kuhusu tukio hilo kwa kuwa lilipotokea alikuwa kanisani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda, aliahidi kutoa ufafanuzi baada ya kupokea taarifa sahihi kuhusu tukio hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles