23.9 C
Dar es Salaam
Thursday, September 29, 2022

Kichaa cha mbwa hakiambukizwi kwa kula nyama yake – Daktari

Na AVELINE KITOMARY

UGONJWA wa kichaa cha mbwa  husababishwa na virusi vinavyoshambulia  mfumo wa fahamu na huambukizwa kwa kung’atwa au kulambwa jeraha  na mnyama mwenye virusi.

Virusi hivyo vinavyoshambulia kwa kitaalamu huitwa Lyssavirus.

Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya mnyama mwenye kichaa cha mbwa kumng’ata binadamu au wanyama wengine.

Kichaa cha mbwa kinaambukizwa kwa binadamu, wanyama wafugwao kama mbwa, paka, mbuzi, kondoo na ng’ombe.

Vilevile hata wanyama wa porini kama fisi, nguchiro wanakuwa na virusi hivyo  ila hawaonyesho dalili za wazi kama mbwa.

Hivyo, kila tukio la kung’atwa na mbwa lazima litolewe taarifa kwa wataalamu wa afya au mifugo kwani ugonjwa huu hauna tiba  kwa binadamu au mnyama pindi dalili zinapojitokeza.

HALI YA UGONJWA ILIVYO NCHINI

Siku ya kichaa cha mbwa  huadhimishwa kila Septemba 28 duniani, ambapo Jumuiya ya kitaifa inatoa elimu juu ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 70,000 hufariki kila mwaka duniani kutokana na ugonjwa huo.

Bara la Asia hasa  nchi ya India inaongoza kuwa na ugonjwa ikifuata Bara la Afrika.

Watu 59,000 hupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa  asilimia  96 ni Asia  huku asilimia 36 ni Afrika na kwa Tanzania kunatakwimu za wanaokwenda hospitali mwaka 2019 ambapo  watu walioripoti kung’atwa na wanyama 12,680  nchi nzima, kati yao ni watu sita walifariki.

Kwa mwaka huu, wamepatikana watu 18,766 mfumo haujaripoti vifo lakini pia  taarifa za tafiti mbalimbali za mwaka 2002 zinaonesha kuwa takribani watu 1,500 hufariki kila mwaka  kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini.

Watoto chini ya  umri wa miaka 15 wanatajwa kuwa waathirika  huku wengine hawaripoti  katika vituo vya afya mpaka baadae dalili zinapoanza kuonekana.

KWANINI WATU HUPENDA KUFUGA MBWA

Michael Ngoma Mkazi wa Kimara ambaye anafuga mbwa, anasema yeye humpenda mnyama huyo kutokana na ulinzi katika nyumba yake hali inayomfanya kuwa makini katika kuhudumia.

Anasema kwa takribani miaka 10 amekuwa akifuga mbwa na anaona hawezi tena kuishi katika nyumba yake bila kuwa na mnyama huyo.

“Niliamua kufuga mbwa baada ya nyumba yangu kuvunjwa na kuibiwa vitu.

Anaongeza: “Mbwa anaweza kusababisha madhara lakini pia nampenda ni mlinzi wa nyumba yangu huwa namfungulia usiku kwahiyo wezi hawathubutu kusogea hapa na kuimba na hata wanapokuwa karibu na nyumba yangu mbwa anabweka hadi naamka.

“Huwa namhudumia mbwa na ninakibali cha kufuga, nampatia chanjo ya kichaa cha mbwa kila mwaka na asubuhi namfungia ndani hadi usiku ndio namfungua saa nne au tano kwani wakati huo hakuna watu wanaopita hapa,” anasema Ngoma.

Hata hivyo, anasema ufugaji mbwa unahitaji umakini hasa wa kulisha na chanjo ili aendelee kuwa na afya bora.

“Sijawahi kupata malalamiko ya mbwa wangu kumg’ata mtu lakini hii hainifanyi kutokuzingatia chanjo kila mwaka  kwani ni muhimu,” anabainisha. 

UELEWA WA JAMII KUHUSU KICHAA CHA MBWA

Jubileta Bernard, ni mtaalamu wa elimu ya afya kwa jamii kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, anasema zipo jamii ambazo zinaimani potofu kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa  kutokana na kuhusishwa na kulongwa.

Anasema si vyema jamii kuzingatia suala hilo badala yake ni muhimu kupata kuelewa jinsi kupata chanjo haraka na kujua dalili za ugonjwa huo.

“Lakini wengine  wanahusisha ugonjwa huo  na ushirikina kutokana na dalili zake ambazo zinaonekana kwa mgonjwa  kwahiyo wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji na kufariki.

“Muhimu mtu anapong’atwa awahi kituo cha afya kupata huduma na wafugaji wawafungie wanyama ndani wawafungulie usiku, lakini pia kuna watu wanazoea kukaa na mbwa ndani hadi anamlamba mtu kama anakidonda hivyo virusi vinaweza kuingia  na jeraha ikikutana na mate ya mbwa anaweza kupata madhara,” anasema.

ULAJI NYAMA ZA MBWA

Kwa mujibu wa Jubilate, ulaji wa nyama za mbwa mwenye kichaa hauwezi kusababisha mtu kupata ugonjwa huo isipokuwa labda kama alikufa na kumshika.

“Kama mbwa kafa halafu mtu kaenda kumshika na kama kashika sehemu ya uti wa mgongo au ubongo na labda yeye ana kidonda na kikakutana na sehemu hizo virusi wanaweza kupenya kupitia hicho kidonda.

“Hapo anaweza kupata lakini virusi hivi vinaweza kufa kwa joto inamaana ukipika nyama haiwezi kuwa na virusi hivyo mtu hawezi kupata,” anaeleza Jubilate.

KUTOKA KWA BINADAMU KWENDA KWA MNYAMA

Jubilate anasema uenezaji wa virusi kutoka kwa binadamu kwenda kwa mnyama  haujawahi kuripotiwa lakini kisayansi hilo linawezekana.

“Hutokea hadi mtu huyo athibitishwe kuwa na virusi vya kichaa mbwa na huyo mbwa hana na kuwe na ukaribu kati ya mnyama na huyo mtu.

Anasema kwa kawaida virusi vinakaa kwa wanyamapori ambao ni jamii ya mbwa kama fisi, mbweha, mbwa mwitu na nguchiro.

“Mbwa hupata maambukizi endapo kama akakutana na fisi au mbwa mwitu  akimg’ata anapata virusi kwahiyo mbwa na yeye anaambukizwa na wanyama wa porini. Hata hivyo, mbwa kupata chanjo inaondoa uwezo wa binadamu kupata  maambukizi,” anafafanua.

DALILI KWA WANYAMA

Jubilate anasema dalili ya kichaa cha mbwa hujitokeza kati ya siku mbili hadi 45 au zaidi tangu kung’atwa na mbwa au mnyama mwenye ugonjwa.

Anasema dalili hizo ni kama mbwa kubadilika tabia na kuwa mpole au mkali zaidi, kushambulia na kuuma vitu mbalimbali kama vyuma, vijiti, kuhangaika  hangaika na kukimbia ovyo.

“Zingine ni kushindwa kula na kunywa maji, kutokwa mate mengi, kudhoofu, kupooza na hata kifo. Lakini dalili kama hizi zinaweza kuonekana kwa wanyama kama mbuzi, ng’ombe, paka na nguruwe.

“Si hao tu, wanyama pori kama mbweha, mbwa mwitu, fisi na nguchiro wanaweza kuonesha dalili hizo,” anasema.

DALILI KWA BINADAMU

Anasema dalili za kichaa cha mbwa kwa binadamu hujitokeza  kati ya wiki moja  hadi mwaka tangu kung’atwa na mbwa au mnyama mwenye kichaa cha mbwa.

“Dalili zinazoonekana ni maumivu ya mwili, kuwashwa sehemu ya jeraha, kuona vitu ambavyo havipo, maruweruwe hivyo kufanya mgonjwa ajifiche au kukimbia.

“Dalili zingine ni kuogopa maji (hydrophobia), kupata nguvu za nyingi hadi kufungwa kamba, mwili kupooza, kushtushwa na mwanga na kelele mwishowe kupoteza fahamu na kufa,” anaeleza.

HUDUMA YA KWANZA KWA  MTU ALIYENG’ATWA

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mtu aliyeng’atwa na mbwa anatakiwa kupewa huduma ya kwanza haraka zaidi ili kupunguza kiwango cha madhara.

Jubileta anasema mara mtu anapong’atwa na mbwa anatakiwa kusafisha jeraha kwa maji yanayotiririka na sabuni au spirit kwa muda wa dakika 15.

“Kidonda cha mtu aliyeng’atwa na mbwa au mnyama hakitakiwi kufungwa kwa sababu hali hiyo huruhusu wale virusi kuzaliana na kuongezeka, virusi hivyo huishiwa nguvu kwenye mwanga hasa wa jua.

“Hatua inayofuata ni mhanga kuwahishwa kituo cha afya kilichopo karibu ili kupatiwa chanjo na matibabu zaidi vilevile taarifa itolewe kwa mtaalamu wa mifugo wa eneo husika,” anaeleza Jubileta.

KUMALIZA DOZI

Jubilate anasema kwa kawaida dozi ya chanjo ya kichaa na mbwa kwa mtu aliyeng’atwa ziko za aina mbili, ambayo kuna dozi nne na nyingine dozi tano.

Anasema  chanjo ya dozi tano (IM) huanza siku ya kwanza 0, yapili siku saba, ya tatu siku 14, ya nne siku 21 na ya tano siku ya 28 na nyingine yenye dozi nne (ID) huanza siku ya kwanza, siku ya saba, siku ya 14 na siku ya 28.

 “Mtu asipomaliza dozi anakosa kinga kamili  kama inavyotakiwa uwezekano wa  ugonjwa kukua upo kwahiyo inaweza kuwa inampa kinga halafu hapati anachotakiwa na vimelea haviishi mwili.

“Tunashauri mtu kumaliza chanjo ili apate kinga ya kutosha ili ugonjwa usiindelee,” anasisitiza.

SHERIA ZA UFUGAJI WANYAMA  
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya huduma za  Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Audifas Sarimbo, anasema chanjo ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa inatolewa  mara moja kwa mwaka na inatolewa kwa mujibu wa sheria ya chanjo ya mwaka 2012 zikiwa kwenye sheria ya magonjwa ya mifugo 2013.

“Katika kuchanja inawalazimu kila mfugaji wa mbwa kuchanja mifugo yake na kisheria inatakiwa unapofuga mifugo lazima uwe na kibali  ili kufuga katika hali inayotakiwa kama kupata chakula, maji, mahali pa kukaa pamoja na chanjo.

“Gharama za chanjo kwa mifugo ni nafuu  na lazima kwani asipochanjwa ugonjwa unaweza kuhamia kwa binadamu kwahiyo, kipindi  cha utoaji chanjo kwa mifugo wananchi wanatakiwa kuwa makini,” anaeleza Sarimbo.

Anasema sheria haziruhusu mifugo kuzurura hovyo badala yake inatakiwa kulindwa au kufungiwa.

“Na sheria hiyo ipo ya mwaka  2020 ambayo imeshapita mnyama anatakiwa kufungwa asizurure na mtu anapofuga anatakiwa kupata kibali na  kumpa masharti ya kuchanja mifugo, kuilisha na anakae naye vizuri na  akitoka  anamfunga mnyororo anatembea naye lakini sio kuzurura.

“Kwa mujibu za sheria za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya mwaka 1989 inazungumzia utunzaji wa mifugo ndani ya jiji ambapo mfugaji anatakiwa kuwa na kibali, cheti za kuchanja mifugo na anatakiwa amfunge hadi saa nne usiku ndio amfungulie na kufungwa asubuhi saa 12.

“Pia tunashirikisha serikali za mitaa katika kuzuia mifugo kuzurura hovyo na wataalamu wa mifugo, wito wangu wafugaji wafate sheria na taratibu zilizopo kwa maana kwamba kila jambo unalofanya ufuge kwa  jinsi ambavyo hutaleta madhara kwa wenzako na kuzingata taratibu zilizopo,” anashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,298FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles