NA THERESIA GASPER, DAR ES SALAAM
KOCHA wa JKT Ruvu, Abdallah Kibadeni, amesema hafikirii kuingia mkataba na klabu hiyo kabla ya kuwaandaa wachezaji na kupata kikosi bora cha kwanza kitakacholeta ushindani katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kibadeni ambaye amewahi kuifundisha Simba na mshauri wa benchi la ufundi la timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa sasa, aliitwa kuinusuru timu hiyo na matokeo mabaya baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa kocha mkuu, Felix Minziro.
Akizungumza jana kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Kibadeni alisema bado ana kazi kubwa ya kuwasoma wachezaji akisaidiana na msaidizi wake ili kuandaa ‘first eleven’ itakayoleta ushindani Ligi Kuu.
Alisema ni vigumu kufikiria suala la mkataba kwa kuwa sasa hana mpango huo na anachoangalia zaidi ni kuhakikisha timu hiyo inaondokana na matokeo mabaya na kupata pointi ambazo zitarejesha matumaini ya kubaki Ligi Kuu.
“Suala la mkataba sijalipa kipaumbele wala kulifiria kwa sasa hadi nitakaporidhika na maendeleo mazuri ya timu kwa kupata pointi zaidi ya sita,” alisema.
Alisema kwa kuanza kampeni zake za ushindi watahakikisha wanaondoka na pointi tatu muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar kesho watakapowakaribisha Uwanja wa Karume, Dar es Salaam ili kuondokana na majanga ya kubaki mkiani mwa ligi hiyo wakiwa na pointi moja.
“Kwa muda mfupi ambao nimeifundisha JKT Ruvu nimegundua kuna wachezaji wazuri ambao nitaweza kuwapa nafasi katika kikosi cha kwanza na kuanza safari ya ushindi kwenye mechi zinazofuata,” alisema.
Tangu kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu, JKT Ruvu inakabiliwa na hali mbaya kutokana na kupata matokeo yasiyoridhisha ya kufungwa mechi sita na kupata sare moja baada ya kushuka dimbani mara saba.