26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Simba, Yanga zawania usukani

simbaaaNA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

VIGOGO wa soka nchini Simba na Yanga leo watashuka dimbani katika viwanja tofauti kusaka pointi muhimu huku kila mmoja ikiwania kuongoza usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mabingwa watetezi, Yanga ambao ndio vinara wa ligi hiyo, watakuwa wenyeji wa Toto Africans katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Simba ikicheza ugenini na maafande wa Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Baada ya kupunguzwa kasi kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam FC Jumamosi iliyopita, Yanga wanapigana kuhakikisha wanaendelea kubaki kileleni mwa ligi hiyo pamoja na kuweka heshima ya kutofungwa katika mechi saba mfululizo.

Tangu kuanza kwa Ligi Kuu, Yanga ndio  wameshikilia usukani hivyo wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kusaka pointi mbele ya Toto Africans ili kuendeleza rekodi ya kutofungwa na kubaki kileleni.

Kikosi cha Yanga ambacho kimejikusanyia pointi 16 sawa na Azam wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, kitaingia uwanjani kikiwa kimekamilika baada ya kurejea kwa kiungo mchezeshaji, Haruna Niyonzima ambaye hakucheza mechi iliyopita.

Mahasimu wao, Simba ambao tayari wamepoteza mchezo mmoja dhidi ya watani wao wa jadi Yanga, wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamejikusanyia pointi 15 sawa na Mtibwa Sugar wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa Simba wamepania kuendeleza kasi ya ushindi katika Uwanja wa Sokoine ili waweze kutimiza malengo ya kuondoka na pointi sita baada ya Jumamosi iliyopita kuichapa Mbeya City bao 1-0 na kuvunja mwiko wa kutoshinda kwenye uwanja huo.

Upinzani wa mahasimu hao utazidi kuongezeka ikiwa Simba watashinda dhidi ya Prisons na kufikisha pointi 18 huku Yanga ikitegemea kufikisha jumla ya pointi 19 kama watatoa kipigo kwa Toto African ambao wamepanda daraja msimu huu.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, vibonde Coastal Union wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku Stand United wakiikaribisha Majimaji ya Songea Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Mechi ya maafande wa JKT Ruvu dhidi ya Mtibwa Sugar iliyokuwa imepangwa kuchezwa leo katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam umesogezwa mbele kwa siku moja ili kuwapa mapumziko wenyeji hao ambao Jumapili iliyopita walikuwa mkoani Shinyanga kuchuana na Mwadui FC.

JKT Ruvu ambao wanaburuza mkia katika msimamo wa ligi, wamezidi kuwa na hali mbaya kutokana na kupoteza mechi sita na kupata sare moja baada ya kushuka dimbani mara saba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles