30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Tume yatakiwa kuhakikisha uchaguzi wa haki, usawa

Nigerian+President+Goodluck+JonathanNa Wandishi Wetu, Dar es Salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama imetakiwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na usawa  kuepuka machafuko  yasitokee nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Madola, Goodluck Jonathan, alisema kufanikiwa kwa uchaguzi huo kunategemea  kuwapo  uwazi, haki na kufuata  misingi ya utawala bora.

Alisema ili kuhakikisha amani inakuwapo watakuwa na mazungumzo  na NEC, vyama vya siasa, wadau wa amani, wanadiplomasia na makundi mengine ya uangalizi wa ndani   kujadili  jinsi watakvyojipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi.

“Kwa kipindi chote ambacho tutakuwapo Tanzania tutajaribu kuangalia mazingira  kabla, wakati na baada ya uchaguzi, kama kutatokea kasoro zozote katika kipindi hicho.

“Baada ya kugundua kasoro zitakazojitokeza tutakabidhi  ripoti kwa Katibu mkuu wa Jumuiya hii na  baadhi ya waangalizi washirika na wadau mbalimbali,”alisema Jonathan.

Alisema waangalizi hao wataanza kazi yao Oktoba 23 ambako watatawanyika kwa  makundi katika kila mkoa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huo.

Jonathan alisema waangalizi hao kazi yao itakuwa ni kuangalia muda wa kufungua na kufunga vituo,   kura zitakavyopigwa na mambo mengine yatakayokuwa yakiendelea hadi   mchakato mzima wa utangazaji  matokeo utakavyofanyika.

“Tunatarajia kufanya uangalizi  wa kutokuegemea  upande wowote pamoja na kuwa wawazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.

“Ninaamini   waangalizi hawa   watashirikiana vizuri na Watanzania  katika kuidumisha amani hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu,” alisema Jonathan.

Nao waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana walizindua uangalizi huo na kusema   watasimamia mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu na kuhakikisha unakuwa wa haki na amani.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Charles Njoroge, aliwataka watanzania kufanya uchaguzi wa amani unaozingatia demokrasia    kuepuka kuingia katika machafuko.

Alisema uchaguzi ni muhimu kutawaliwa na msingi wa demokrasia  na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)kushughulikia kasoro na changamoto zote zilizoonekana   kuweka mambo sawa na kuepuka kuingia katika machafuko.

“Waangalizi watahudhuria kila kituo cha kupigia kura  kushuhudia yanayoendelea na lengo letu ni kuripoti kwamba uchaguzi huu umefuata misingi ya utawala bora, demokrasia na haki,” alisema Njoroge.

Naye Kiongozi wa waangalizi hao ambaye pia ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Kenya, Arthur Awori, alisema katika uchaguzi huo hawatajiingiza  katika suala zima la uvunjifu wa amani bali watafuata utaratibu  na sheria ya jumuiya hiyo.

Alisema lengo lao ni kusimamia  na kuhakikisha  mambo yote ya uchaguzi yanaenda sawa kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.

“Sisi tupo kama wasimamizi tu  na  kufuatilia  kwamba  uchaguzi huo sheria imefuatwa  ili kuendeleza amani na utulivu uliopo katika nchi hii.

“Tupo hapa kwa mujibu wa sheria  iliyokuwapo  EAC ambayo  inatutaka kuhudhuria na kuripoti mwenendo wa uchaguzi utakaofanyika kwa kila nchi,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara  ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Joyce Mapunjo,  alisema watasimamia na kufanya kazi kama sheria ya Tanzania inavyosema  na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.

Pia aliwataka Watanzania wanapowaona watu hao wasishangae  kwa sababu wamekuja kusimamia uchaguzi na wawachukulie kama wenzao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles