Veronica Romwald na Jonas Mushi, Dar es Salaam
WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa zamani, Lawrence Masha leo anatarajiwa kufikishwa mahakamani mjini Mpanda mkoani Katavi kwa mashitaka mawili likiwamo la kufanya mkutano na kuingia kwenye kambi ya wakimbizi bila kibali.
Masha ambaye ni wakili wa kujitegemea na ambaye hivi karibuni alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) anashikiliwa na wenzake sita mkoani Katavi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari aliiambia Mtanzania kwa simu jana kuwa Masha na wenzake hao wanadaiwa kufanya makosa hayo huko katika maeneo ya Katumba na Kanoge mkoani Katavi
Kidavashari aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Katibu wa Chadema Jimbo la Msimbo, Stanslaus Selemani na Mgombea ubunge wa Msimbo Gerard Kitabu (Chadema). Wengine ni Gaulus Damian, Lameck Kostantine, Fransisco Sylvester na Abraham Mapunda ambao wote ni wafuasi wa Chadema.
“Tuliwakamata jana saa 4.00 asubuhi… tuliwakamata kwa sababu kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hakukuwa na mkutano wowote wa siasa katika eneo la Katumba wala Kanoge.
“Hivyo walitakiwa kuomba kibali kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa jimbo hilo lakini pia hawakufanya hivyo jambo ambalo ni kosa la maadili kulingana na sheria za nchi.
“Pia wamekiuka kanuni ya adhabu namba 73 ya sheria ya nchi ambayo inaeleza kwamba ni lazima waombe kibali lakini wao waliingia na kufanya mkutano na kuingia kwenye makazi hayo bila kibali,” alisema.
Mkoa wa Katavi una makambi mawili ya wakimbizi ambayo ni Katumba iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo na Mishamo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda.
Hivi karibuni serikali iliwapatia vyeti vya uraia wakimbizi zaidi ya 100,000 walioishi zaidi ya miaka 40 nchini wengi wao wakitokea Burundi.
Hatua hiyo ya kuwagawia vyeti ilianza Novemba 26 mwaka jana na kukamilika Aprili 30 mwaka huu kwa makazi ya Katumba na Mishamo mkoani Katavi na Ulyankulu mkoani Tabora.
Hivi karibuni Mkuu wa Makazi ya Katumba wilayani Mlele, Athman Igwe alisema wakimbizi hao wa Mishamo na Katumba ambao wamepewa uraia wa Tanzania, wana haki zote kama Watanzania wa kuzaliwa ya kuwapigia kura madiwani, wabunge na rais katika uchaguzi mkuu wa Jumapili.
Igwe alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani humo, Laurent Magweshi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC)