30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

NEC yatoa ufafanuzi utaratibu wa kupiga kura

Damian-LubuvaJONAS MUSHI NA ALLEN MSAPI (GHITBS), DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi zaidi juu ya masuala mbalimbali yanayowakanganya wananchi na kuibua taharuki kuhusu upigaji kura katika uchaguzi mkuu Jumapili ijayo.

Juzi, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kufafanua masuala yaliyokuwa yakihojiwa na wananchi kuhusu upigaji kura, taarifa ambayo nayo iliibua maswali mengine.

Moja ya suala lililoleta utata ni taarifa kuwa mtu mwenye kadi ya kupigia kura ambaye jina lake halipo katika Daftari la Kudumu la Wapigakura atoruhusiwa kupiga kura.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Mpigakura na Habari wa NEC, Clarence Nanyaro, alifafanua kuwa kauli hiyo ilimaanisha endapo itatokea mtu akawa na kadi feki ya kupigia kura, hatakuwamo katika daftari hilo na hivyo hataweza kupiga kura.

Alisema kwa wale ambao wana kadi halali iliyotolewa na NEC na hawamo katika mfumo wa daftari, ndio ambao taarifa ya juzi ilieleza kuwa fomu zao za kujiandikishia zitapelekwa tume na majina yao yatawekwa katika orodha isiyo na picha na kupelekwa kituoni ili mtu huyo aweze kupiga kura.

“Tuliposema kwamba mtu ambaye ana kitambulisho, lakini hayupo kwenye daftari la mpigakura hataweza kupiga kura, tulimaanisha wale wenye vitambulisho feki,” alisema Nanyaro na kuongeza:

“Kama tunavyojua teknolojia imekua, hivyo mtu anaweza akatengeneza kitambulisho chake, hii inamaanisha mtu huyo hatakuwapo kwenye daftari na wala ile fomu ya kujiandikisha haitakuwapo tume, hivyo kitambulisho chake kitatambulika kuwa si halali, na ndio hao tuliosema hawataweza kupiga kura.”

Kuhusu watu wenye vitambulisho vyenye namba tofauti na iliyopo katika daftari kuruhusiwa kupiga kura, alisema hiyo haina tatizo kwa sababu si namba ya kitambulisho pekee inayomtambulisha mpigakura.

“Kile kitambulisho kina taarifa nyingi zinazomtambulisha mpigakura, ambazo zitalinganishwa na za kwenye daftari, ikiwamo majina, jinsi, tarehe ya kuzaliwa na mahali ulipojiandikishia, hivyo kama mtu ana kitambulisho na yumo kwenye daftari hatuwezi kumkataza kupiga kura kwa sababu tu namba zimetofautiana,” alisema Nanyaro.

Kuhusu kuwapo kwa wapigakura wenye majina mawili kwenye kituo kimoja cha kupigia kura ambapo tatizo hilo limetokana na mpango wa majaribio, alisema watatoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo wapitie orodha hiyo ili majina hayo yajulikane, na jina moja liondolewe kuzuia mtu kupiga kura mara mbili.

Alisema hawatarajii mtu yeyote kupiga kura mara mbili kwa sababu baada ya kupiga kura atachovya kidole kwenye wino maalumu usiofutika haraka, kutikiwa baada ya kupiga kura, na kwamba hawezi mtu kupigia kura kwenye kituo kingine ambacho jina lake halipo.

“Sheria inasema ili mtu apige kura lazima kwanza aonyeshe kitambulisho cha kupigia kura, na msimamizi atalinganisha taarifa zilizopo kwenye daftari na zile za kitambulisho kisha atapewa karatasi za kupigia kura, akimaliza kupiga kura jina lake litatikiwa na atachovya kidole katika wino maalumu usiofutika haraka, hivyo hataweza kupiga kura mara mbili,” alisema Nanyaro.

Vilevile kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya watu ambao majina yao yametokea kwenye vituo ambavyo hawakujiandikisha, alisema NEC ilikwishatoa ufafanuzi wa suala hilo kuwa lilisababishwa na kuhamisha mashine kutoka eneo moja kwenda jingine, ambapo kutokana na makosa ya kibinadamu waendeshaji wa mashine hizo walisahau kuhifadhi na kubadili majina ya maeneo pale walipokuwa wakihama.

Awali, NEC ilifafanua kuwa ililiona tatizo hilo baada ya kutolewa kwa daftari la awali, na walichofanya ni kuorodhesha majina hayo ili yapelekwe katika vituo walivyojiandikisha waweze kupiga kura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles