22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kiiza aibuka mchezaji bora Septemba

c9661bfc79f76cb048f249f19a2680f2NA THERESIA GAPER, DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa Simba, Hamis Kiiza ‘Diego’, ameibuka mchezaji bora wa Septemba katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kujinyakulia zawadi ya shilingi milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo.

Mechi za raundi tano zilizochezwa mwezi Septemba tangu kuanza kwa ligi hiyo ndiyo zimehusishwa kwenye mchakato wa kumpata mshindi wa kwanza.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema Kiiza ameisaidia Simba kufanya vizuri ndani ya mwezi huo ikiwemo kufunga ‘hat-trick’ katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kiiza aliyefunga mabao matano hadi sasa ameibuka mshindi na kuwapiga bao wachezaji wengine waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho, Amissi Tambwe wa Yanga na Elius Maguli wa Stand United.

Nyota ya mshambuliaji huyo aliyetua Simba akitokea kwa mahasimu wao Yanga, imezidi kung’ara baada ya mwezi uliopita kuchaguliwa na klabu yake kuwa mchezaji wa mwezi.

Kiiza ni miongoni mwa wachezaji wanaowania kiatu cha dhahabu Ligi Kuu akiwa amefunga mabao matano sawa na Donald Ngoma wa Yanga huku Maguli akiongoza kwa kufunga sita wakifuatiwa na Tambwe na Kipre Tchetche waliopachika nyavuni mabao manne kila mmoja.

Wakati huo huo, TFF imezisogeza mbele mechi za Ligi Kuu ambazo zilipangwa kuchezwa katika raundi ya 11 Novemba 7 na 8, mwaka huu hadi Desemba 12 na 13, mwaka huu ili kupisha maandalizi ya timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ dhidi ya Algeria.

Stars inatarajiwa kukutana na Algeria Novemba 14, mwaka huu katika mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kizuguto alisema Stars itaingia kambini mapema mwezi ujao ili kujiandaa na mchezo huo wa awali kabla ya kurudiana ugenini Novemba 17, mwaka huu.

Alisema mechi tatu za raundi ya sita ambazo hazikuchezwa Oktoba 4, mwaka huu ili kupisha mechi ya Stars dhidi ya Malawi zimepangwa kufanyika Desemba 16, mwaka huu.

Mechi zilizoahirishwa zinaihusisha Yanga dhidi ya African Sports katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam FC ikiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex huku Simba ikisubiri kupangiwa tarehe ya kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles