29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya Mfalme Zumaridi na wenzake 82 yaahirishwa hadi Aprili 14

Na Clara Matimo, Mwanza

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza Machi 31, 2022 imeahirisha kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa 83 akiwemo Diana Bundala, maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi kutokana na hakimu anayeendesha shauri hilo kutokuwepo mahakamani hapo.

WAFUASI ZUMARIDI: Baadhi ya wafuasi wa Mfalme Zumaridi wakisubiri kuingia mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili mfalme zumaridi na wenzake.Picha na Clara Matimo.

Mfalme Zumaridi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, shambulio la kudhuru mwili na kuzuia maofisa wa serikali kutimiza wajibu wao.

Kutokana na kutokuwepo mahakamani hapo kwa hakimu anayeendesha shauri hilo, Hakimu Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekubora, mashauri hayo yamesikilizwa na Hakimu Mkazi  Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga, aliiambia mahakama hiyo kwamba upelelezi wa kesi namba 11 na 12 inayomkabili mfalme Zumaridi na wanzake 82 umekamilika lakini kutokana na hakimu anayeendesha kesi hiyo  pamoja na baadhi ya washtakiwa kutokuwepo mahakamani hapo  ameiomba  mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya maelezo ya awali kusomwa.

Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Stella Kiama, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14, mwaka huu ambapo mfalme zumaridi na wenzake  saba ambao hawajapata dhamana wataendelea kusota rumande.

 Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wakili wa washtakiwa hao Erick Mutta, amewaambia waandishi wa habari kwamba jumla ya washtakiwa nane wamedhaminiwa leo hivyo kufanya idadi ya ambao hawajadhaminiwa lakini dhamana yao iko wazi kufikia  saba ukimuondoa mfalme Zumaridi ambaye kesi yake namba 10 ya usafirishaji haramu wa binadamu kutokuwa na dhamana.

Amesema mshtakiwa mwingine ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kuugua, amelazwa  Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC) akiuguza majeraha aliyoyapata wakati wa kukamatwa na maafisa wa jeshi la polisi mkoani humo katika mtaa wa buguku jijini hapa.

“Kesi zote tatu leo ziliitwa, kesi namba 10  ya usafirishaji haramu wa binadamu ambayo inamuhusu Mfalme Zumaridi peke yake  iliitwa kwa ajili ya kutajwa  na kesi mbili zinazomkabili  pamoja na wafuasi wake zilikuja kwa ajili ya usomaji wa hoja za awali.

 “Lakini kwa bahati mbaya kesi hizo zote  hazijaendelea kwa sababu mshtakiwa namba 38  wa kesi namba 12 hakuweza kufika mahakamani hapa yuko hospitali kwa ajili ya matibabu na kesi nyingine ambayo inamkabili mfalme Zumaridi  pamoja na wenzake imeshindwa kuendelea kwa kuwa hakimu anayeendesha shauri hilo hayupo mahakamani hapa leo,”amefafanua Mutta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles