24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

RC Mgumba awagomea madiwani juu ya waliofukuzwa msituni kurudia mkaa

Na Denis Sinkonde, Songwe

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amekataa ombi la madiwani wa Wilaya ya Songwe mkoani humo waliotaka wafanyabiashara ya mkaa waruhusiwe kuchukua mkaa wao uliokwama katika maeneo ya Hifadhi ya misitu ya asili na wale waliokiuka vibali vya kusafisha mashamba baada ya Serikali kupiga marufuku uchomaji holela wa mkaa.

Mgumba amekataa ombi hilo wakati wa kikao cha kujadili mbinu za kuzuia uharibifu wa mazingira na hali ya amani wilyani Songwe ambacho kimefanyika Februari 28, 2022.

Awali, akizungumza katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Shabath Kapingu aliiomba serikali iwaruhusu wananchi kutoa mkaa au iuchukue mkaa na kugawa kwenye taasisi za umma.

Moja ya sehemu iliyoharibiwa kwa uchomaji huo wa mkaa.

Upande wake diwani wa Kata ya Kanga, Erick Kihinda amesema utaratibu ulikosewa tangu mwanzo na serikali ilipotoa vibali halali ambavyo wananchi walienda kuchukua mikopo benki kwa ajili ya uchomaji wa mkaa.

Nae diwani wa Viti Maalumu Songwe, Paskalia Shitundu aliiomba serikali kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa watu ambao waliomba kusafisha mashamba kwa ajili ya kilimo cha korosho kama kweli walifanya hivyo basi waruhusiwe kuchukua mkaa wao.

Huku diwani wa Kata ya Magamba, Kapala Makelele akiiomba serikali itoe muda walau wa siku 14 baada ya hapo isimamie kweli kweli usimamizi wa mazingira.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba, akitoa majibu ya maombi hayo, amesema, serikali itasimamia sheria kwa kuwa wananchi wengi wamekiuka vibali walivyopata kwa kwenda kuchoma mkaa kwenye misitu ya hifadhi.

“Ndio maana serikali imeweka adhabu hata kama mtu alikopa benki lazima apate adhabu ili siku nyingine asirudie kutenda kosa.

“Kwenye utunzaji wa mazingira serikali haina utani, lazima ihakikishe mazingira yanakuwa salama,” amesema Mgumba.

Aidha, Mgumba amemuagiza mkuu wa wilaya ya Songwe kwenda kukusanya mkaa wote uliopo kwenye mapori kwa ajili ya kuandaa utaratibu mzuri wa kuigawa kwenye taasisi za serikali kama inavyofanya pale inapokuwa imekamata sukari za magendo.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameagiza ianze oparesheni maalumu kwa ajili ya kuwaondoa watu wote ambao waliovamia hifadhi za misitu, vyanzo vya maji na wale wanaoharibu mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles