25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kigogo OBC yapigwa kalenda

Janeth Mushi -Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imeshindwa kumsomea hoja za awali Mkurugenzi wa Kampuni ya wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu ya Otterlo Business Cooperation (OBC), Isack Mollel (59), baada ya wakili wa Serikali aliyekuwa akiendelea na shauri hilo kutokuwepo mahakamani.

Katika shauri hilo namba 74 la mwaka huu, Mollel anakabiliwa na mashtaka 37 ya kujihusisha na kuajiri raia 37 wa kigeni wasiokuwa na vibali halali vya kufanya kazi nchini wala cheti cha msamaha, kinyume na sheria ya kuratibu ajira na mahusiano ya wageni.

Mollel anaungana katika shauri hilo na raia 10 wa kigeni waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali, ikiwemo ufundi magari, ufundi matairi, wapishi, madereva na wapaka rangi nyumba, ambao wote waliajiriwa na OBC eneo la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani hapa, ikijishughulisha na shughuli za uwindaji wa kitalii.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Niku Mwakatobe, jana shauri hilo lililopangwa kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Janeth Sekule na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Idara ya Kazi, Emanuel Mweta huku Mollel akitetewa na mawakili Daud Haraka na Goodluck Peter.

Wakili Janeth aliiomba mahakama hiyo kuahirisha shauri hilo kutokana na Wakili Mwandamizi wa Serikali Khalili Nuda, aliyetakiwa kuwasomea washtakiwa hao maelezo hayo, kudaiwa kuwa ni mgonjwa, hivyo hawezi kufika mahakamani.

“Mheshimiwa hakimu, shauri hili limekuja leo kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa  maelezo ya awali, lakini kwa bahati mbaya Wakili Nuda ambaye alipaswa kuwasomea maelezo hayo ni mgonjwa, hivyo hajaweza kufika mahakamani leo, tunaomba tarehe nyingine ili waweze kusomewa maelezo ya awali,” alisema.

Baada ya maelezo hayo ya Jamhuri, upande wa utetezi walisema hawana  pingamizi juu ya maombi hayo.

Wakili Haraka aliiomba mahakama tarehe itakayopanga  kesi  hiyo, wateja wao wasomewe maelezo hayo ya awali pamoja na kuanza kusikilizwa siku hiyo hiyo, maana raia hao wa kigeni wamekaa hotelini kwa  muda mrefu, hivyo wanazidi kutumia gharama kubwa wakisubiri kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Baada ya maelezo hayo, hakimu Niku alihairisha kesi hiyo hadi Agosti 7, mwaka huu na kueleza kuwa iwapo upande wa Jamhuri hautawasomea maelezo ya awali watuhumiwa hao, ataifuta kesi hiyo.

Washtakiwa hao ni Darweshi Jumma Riaz, Aziz Khan, Mohammad Tayyab, Ali Bakhsh, Abdul Rehman Muhammad, Martin Crasta, Imtiazd Fiaz, Arshad Muhammad, Hamza Sharif  na Zukfiqar Ali.

Wakati huohuo, mahakama hiyo imeahirisha  kesi inayoikabili Kampuni ya OBC pamoja na Mkurugenzi wake Mollel, wanaokabiliwa na mashtaka 10, ikiwemo ya utakatishaji fedha haramu na kukwepa kodi, kutokana na upelelezi wake kutokukamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles