23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Bilioni 1.2/- kumaliza tatizo wasiojua kusoma, kuandika

Amina Omari-Muheza

SHIRIKA la Kimataifa lisilokuwa la kiserikali la Room to read, linatarajia kutumia kiasi cha Sh bilioni 1.2 kutekeleza mradi wa kuboresha elimu ya shule za msingi ili kupunguza wimbi la kuwepo kwa wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika nchini.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika  hilo nchini, Peter Mwakabwale wakati akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kuhusu namna shirika hilo linavyoshirikiana na Serikali kuboresha elimu.

Mwakabwale alisema mradi huo unatarajia kunufaisha shule za msingi 30 awamu ya kwanza kwa kujenga miundombinu ya maktaba na uboreshwaji darasa la kwanza na la pili.

Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wànafunzi wanajua kusoma na kuandika wakiwa katika madarasa ya chini na kumaliza tatizo la wànafunzi kumaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika.

“Hivi sasa tunafanya kazi katika nchi 16 duniani ambapo kwa upande wa Afrika ni Tanzania, Afrika Kusini, Zambia, na Rwanda.

“Kwa Tanzania tulianza kazi 2012 wakati kiwango cha elimu kilipokuwa kimeshuka sana, wanafunzi wengi walikuwa wakimaliza darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika, matokeo nayo yalikuwa yapo chini sana, ndipo shirika lilipoona ipo haja ya kusaidia kuboresha sekta ya elimu,’’ alisema Mwakabwale.

Aliongeza kuwa wanajikita zaidi katika kuwafundisha walimu wa darasa la kwanza na pili zaidi sababu ndio msingi wa elimu.

“Kiwango chetu ni mwanafunzi aweze kusoma maneno 45 kwa dakika, hiki ni kiwango cha kidunia. Kwa Tanzania wanatumia maneno 50 ili kuthibitisha kuwa mwanafunzi anaweza kujisomea mwenyewe pasipo kupata usaidizi wowote,” alisema.  

Ofisa Elimu (Msingi), Pilly Maximillian, alisema wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa, ukizingatia wana changamoto ya watoto ambao uwezo wao wa stadi za kusoma na kuhesabu si mzuri, hivyo mradi huo wa maktaba katika shule zao utawasaidia katika kupunguza changamoto hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles