Bethsheba Wambura
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema nchi yake itaendelea kuimarisha uhusiano na Tanzania bila kujali maneno ya wanasiasa yanayotaka kuuvuruga.
Kenyatta ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 5, wakati akihutubia wananchi na viongozi waliojitokeza kumlaki alipotua katika Uwanja wa Ndege Chato mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili hapa nchini.
“Tuko hapa kuimarisha urafiki na tupo na wananchi wanaojuana na wanaozungumza lugha moja ya kinyumbani na kitaifa, ufike Namanga ni majirani kwa lugha ya nyumbani na kitaifa, upande wa Pwani hadi Taveta ni jamii moja, mtu anawezaje kututenganisha.
“Haiwezekani siasa tuanze nayo kila wakati ukinywa chai siasa, ukienda ‘lunch’ siasa ukienda kwa mpenzi wako ni siasa haiwezekani kila siku ni siasa ina wakati, tujipange kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu mambo hayo ndiyo yatabadilisha maisha,” amesema Rais Kenyatta.
Aidha, Rais Kenyatta amesema hata michezo inaimarisha ujirani kati ya nchi hizo mbili huku akikumbushia mechi kati ya Timu ya Taifa Stars na Harambee Stars zilipomenyana katika fainali za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), zinazochezwa nchini Misri ambapo Harambee ilishinda 3-2.
“Juzi tumechapana kule Cairo kila mtu na timu yake huku Harambee Stars huku Taifa Stars, sidhani kama kuna mtu alilala siku ile ila ndiyo hali ya mpira safari hii Kenya imeifunga Tanzania lakini hata ninyi mlifaidika tulipocheza na Senegal, nyinyi mlifungwa mbili na sisi tulifungwa tatu,” amesema.