Bethsheba Wambura
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani amewakaribisha wawekezajji kutoka ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza wilayani Chato kutokana na mji huo kuwa na maendeleo ya kasi yatayochangia uwekezaji katika sekta nyingi hususani madini.
Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Chato (CCM), amesema mji huo unakua kwa kasi kwasababu ina vitu vinavyochagiza maendeleo hayo ikiwamo miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege na katika sekta ya utalii ambapo Julai 9 mwaka huu Rais Dk. Magufuli atazindua Hifadhi ya Taifa ya Burigi ambayo itaongeza pato la taifa kutoka kwa watalii wakaoitembelea.
Dk. Kalemani ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 5, wakati akizungumza katika mapokezi ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika Uwanja wa Ndege wa Chato, ambapo amesema pia kuna uwekezaji katika sekta ya uvuvi sababu ya uwepo wa Ziwa Victoria.
“Mheshimiwa Rais mimi ulinipa dhamana baada ya wananchi na ‘wanazengo’ wa Chato kuniamini kubeba nguzo na kuwapelekea Watanzania nataka nikwambie tu kuwa upele huu umepata mkunaji na kama ulivyoniagiza nipeleke umeme sehemu zote bila kujali aina ya nyumba hata kama ya tembe na makuti nami nafanya hivyo.
“Mwaka jana ulianzisha mradi wa umeme unaotokana na maporomoko ya Mto Rufiji wa megawati 2,115, kwa hatua hii Mheshimiwa Rais Watanzania hawatakusahau kwani umeiweka Tanzania katika ramani kwa kujenga bwawa kubwa ambalo litakuwa kati ya mabwawa 70 makubwa duniani hakika hii ni historia,” amesema Kalemani.