Kauli ya Bashiru yagonga vichwa

0
899

Na MWANDISHI WETU

Kauli  iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, akisema kwa mwaka 2010 nchi ilipata Serikali isiyo na uhalali wa kisiasa kutokana na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza na kwamba kwa sasa wananchi wanaona uchaguzi kama kituko na maigizo, imepasua wengi vichwa.

Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo mjini Morogoro, kwenye kongamano la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).

Baada ya kauli hiyo, watu wa kwenye mitandao ya kijamii na katika mikusanyiko mbalimbali, walionekana wakichambua kauli hiyo ya Dk. Bashiru, ambapo baadhi walidai anataka kuonyesha nia yake ya kutenga chama na serikali na wengine walimpinga.

Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa, aliunga mkono hoja ya Dk. Bashiru, akisema ilijikita katika kuupambanua ukweli wa mambo.

Hata hivyo, hakukubaliana na hoja ya kwamba Serikali iliyotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na uhalali wa kisiasa.

Msekwa alisema uhalali wa kisiasa wa Serikali hutokana na kura zilizopigwa na si idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

“Suala la kupiga kura ni hiari ya mtu, hatulazimishwi kupiga kura, sasa hapo nimekuwa tofauti naye kidogo, lakini mambo mengine kaelezea ukweli halisi.

“Kwa kumbukumbu zangu, najua nchi yenye sheria ambayo inamlazimisha mwananchi kupiga kura ni Australia, lakini huku kwingine ni hiari ya mtu.

“Pia nimeona chaguzi mbalimbali tangu uhuru wa nchi yetu, mara nyingi hizi chaguzi za marudio huwa hazina hamasa, labda kwa uchaguzi mkuu watu wanakuwa na shauku ya kuona Serikali mpya,” alisema Msekwa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema kauli ya Dk. Bashiru ni marudio ya hoja ambazo Chadema imewahi kuzisema siku za nyuma.

“Sioni kipya juu ya kauli yake, ni marudio tu, sisi tulishasema huko nyuma, ukiangalia katika chaguzi hata hizi ndogo ni aibu, wao kama wanajikosha maana yake nini sasa, si waondoke?,” alisema Profesa Safari.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo si tu kama Katibu Mkuu wa CCM, bali mchambuzi wa siasa.

Alisema Dk. Bashiru alitumia kauli hiyo kuishawishi CCM kuwa haipaswi kubweteka kwa nyimbo za hiyena hiyena ya ushindi wa kura moja.

Dk. Lwaitama alisema Dk. Bashiru anakikumbusha chama chake ambacho kipo kwenye mapambano na mabeberu wa makinikia kuwa kihakikishe kinajikita kwa wananchi.

“Unahitaji kumuelewa kwa umakini sana Dk. Bashiru, kushinda unaweza kushinda hata kwa kura moja, lakini hata kama umeshinda wakati wapigakura ni wachache ni sawa utakuwa umeshinda kisheria, lakini hujashinda kisiasa.

“Ukijidai umeshinda lakini ndani ya mioyo ya watu hujashinda, hutaaminika na pia hata wewe hutakuwa umeridhika na kama ni hivyo utajikuta umeegemea zaidi mabavu kulisho ushawishi.

“Kwa mtazamo wangu namshauri Dk. Bashiru aendelee na msumari huo huo wa kusema ukweli, lakini itategemea kama mwenyekiti ataendelea kuwa na busara ya kutaka kuendelea kuwa na mtu kama yeye,” alisema Dk. Lwaitama.

Naye  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudens Mpangala, alisema Dk. Bashiru ametumia kauli hiyo kusema ukweli katika mazingira ya ukatibu wake.

Alisema kauli ya Dk. Bashiru inajibu tuhuma ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi ya CCM kuwa ni chama dola na kinatumia Tume ya Uchaguzi (NEC) kuminya haki ya demokrasia.

Alisema kauli hiyo ya Dk. Bashiru inakikosoa chama chake hata kwa mazingra ya sasa ya kisiasa ambapo CCM kinatuhumiwa kununua viongozi wa upinzani na kuwasimamisha tena kugombea nafasi hizo, jambo ambalo si halali kisiasa.

Uchaguzi Mkuu

Mwaka 2000 wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 10,088,484 na waliopiga kura wakiwa 8,517,598, sawa na asilimia 84.4

Katika uchaguzi wa mwaka 2005 waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16,407,318, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11,365,477, sawa na asilimia 69.3.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo walikuwa 8,626,283, sawa na asilimia 42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.

Mwaka 2015, Watanzania wengi mno walijitokeza kupiga kura. Katika watu milioni 23 walioandikishwa kupiga kura, zaidi ya milioni 15.6, sawa na asilimia 67, walipiga kura.

Kauli ya Dk Bashiru

“Tuambizane ukweli, mkishapewa kofia na T-shirt (fulana), (wakati wa uchaguzi) halafu nyimbo zikaanza kupigwa za mbele kwa mbele, huwa mnapata nafasi za kuhoji sifa za mnayetaka kumchagua?

“Je, sifa ya chama mnachotaka kukichagua kinachopiga mbele kwa mbele unaijua, kwa hiyo eneo jingine muhimu kwa nafasi yenu ni kuwa sehemu ya mchakato ya kuwajibisha wote wenye vyeo vyenu. Kwa hiyo msichague kiongozi kwa T-shirt, kwa kofia, kwa ubwabwa, kwa pesa.

“Kwa kufanya hivyo mnatengeneza watu watakaokuja kuwaonea, kwasababu dhuluma zote zinazosemwa na uonevu hazifanywi na wakoloni, zinafanywa na wale mliowachagua nyie wenyewe. Au wale walioteuliwa na wale mliowachagua.

“Sasa watu ambao ni wajanja mimi naweza kusema, wapiga kura wa Tanzania ambao wamefikia hatua ya kudharau uchaguzi, wanakaa nyumbani (siku ya uchaguzi) kwasababu wanaona ni kama kituko, ni mchezo wa kuigiza.

“Na ndiyo maana leo kupata watu kuhudhuria kupiga kura imekuwa shida, kote tunakoshinda ni chini ya asilimia 30, chini ya asilimia 40, hakuna mahali ambako wapiga kura wamejitokeza kwa zaidi ya asilimia 50.

“Na mwaka 2010 ilitia fora, watu wengi walijiandikisha zaidi ya asilimia 100, kumbe walikuwa wanataka kile kipatarata (kitambulisho cha mpiga kura) kwasababu kinatumika kwenda polisi kudhamini, unajitambulisha, walipokipata wakaingia mitini.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, tulipata Serikali ambayo haikuwa na uhalali wa kisiasa kwa sababu wapiga kura wengi zaidi ya asilimia 50 walibaki nyumbani na tatizo hili halijaisha, lakini mwanasiasa akishashinda anasema ushindi ni ushindi tu hata kama ni kwa kura moja.

“Hajali kwamba ushindi ule unatakiwa uwe na uhalali, tulifika mahali ambako ikifika wakati wa uchaguzi wagombea wanauza nyumba, wanakopa, wanaitisha mikutano ya kuchangisha, usipomchangia mkali utafikiri anakwenda hospitali kutibiwa.

“Akishazikusanya zile fedha anakwenda kuwanunua mawakala na mawakala wanawanunua wapiga kura, msimu wa uchaguzi unakuwa msimu wa rushwa ya uchaguzi, ninachowaomba nafasi yenu ni kubomoa na kuharibu soko la kura,” alisema Dk. Bashiru.

CHAGUZI NDOGO

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Ukonga uliofanyika Septemba 16, mwaka huu, waliotarajiwa kupiga kura walikuwa 300,609, lakini waliojitokeza ni watu 88,270, sawa na asilimia 29.4.

Katika Jimbo la Monduli, walioandikishwa kupiga kura walikuwa 80,282, lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 69,521.

Katika uchaguzi wa Jimbo la Buyungu uliofanyika Agosti 12, waliotarajiwa kupiga kura walikuwa 61,980 na  waliojitokeza ni 42,356.

Jimbo la Singida Kaskazini waliojiandikisha kupiga kura ni 91,518, idadi ya watu waliopiga kura ni 22,298, sawa na asilimia 30.

Jimbo la Songea Mjini waliojiandikisha kupiga kura ni 128,841 na idadi ya watu waliopiga kura ni 46,841.

Machi 16, 2014 katika uchaguzi mdogo wa Kalenga mkoani Iringa kati ya watu 71,964 waliojiandikisha kupiga kura, waliojitokeza ni 29,541 (asilimia 41); Vivyo hivyo ikawa katika uchaguzi mdogo wa Chalinze mkoani Pwani, ambako kati ya watu 92,000 walioandikishwa, 24,422 ndio waliopiga kura, sawa na asilimia 26.5.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here