26.1 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

KATIBU MKUU CCM AWASHUKIA MAWAZIRI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema kuna baadhi ya viongozi ndani ya Serikali wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi akiwamo  Waziri mmoja ambaye  anamiliki ekari 1000 mkoani Morogoro.

Akizungumza jana Jijini hapa  katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Dk. Bashiru alisema ardhi imekuwa muhimu lakini kuna baadhi ya viongozi wamehodhi maeneo makubwa.

Dk.Bashiri alisema hivi karibuni alikuwapo mkoani Morogoro ambako alitajwa Waziri mmoja kwamba anamiliki ekari 1,000 za ardhi.

“Nilikuwa Morogoro akatajwa waziri mmoja ana ekari 1,000, wananchi wananiuliza wanataka kujua amezipataje. Na mimi nitamuita aeleze amezipataje?”

“… Hatuwezi tukawa na viongozi ndani ya chama kinachojitambulisha kama chama cha wanyonge halafu baadhi yetu wanapora ardhi ya wanyonge,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema migogoro ya aina hiyo inajenga chuki kati ya chama, serikali na wananchi.

Alisema ardhi kwa masikini ndiyo nyenzo ya uhakika ya kumkomboa katika lindi la masikini.

Dk. Bashiru alisema atamuita waziri huyo aeleze alipataje eneo hilo kwa sababu CCM haiwezi kuwa na wanachama ambao ni waporaji wa ardhi.

“Achague kimoja kama ni mporaji ama kuwa kiongozi wa CCM,” alisema.

Alisema wakati mwingine mambo yanayozungumzwa katika vyombo vya habari unaweza kudhani ndiyo hali halisi katika Jamii.

“Viongozi msifanye kazi katika vyombo vya habari nendeni katika maeneo mbalimbali mkatatue kero za wananchi.

“Nilikwenda eneo moja wananchi wanajiuliza waziri huyo amepataje ardhi hiyo,” alisema Dk. Bashiru.

RULA YAMUUMIZA KICHWA

Kuhusiana na Uvuvi, Dk. Bashiru alisema katika operesheni ya kukabiliana na uvuvi haramu yameibuka makundi ya watumishi wa Serikali kuwakandamiza wananchi.

“Kuna mama alianika kisiwani samaki wake 66 aina ya sato, wamefikishwa mwaloni na kupokelewa  wapelekwe Arusha. Ghafla anapigiwa simu kuwa samaki wamekamatwa kisa rula, kwa hiyo atume Sh 100,000 kuukomboa mzigo,” alisema.

Alisema alimpigia simu Mkuu wa Wilaya ya Ilemala lakini simu yake haikupokelewa kwa sababu alikuwa kikaoni, hivyo alimuagiza Katibu wa CCM wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo.

Alisema baada ya kufuatilia suala hilo ilibainika ni watendaji wa Serikali waliokuwa wakimnyanyasa mama huyo kwa kutaka kupewa rushwa ambako hatua zilichukuliwa dhidi yao.

Alisema alimuagiza Naibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kuwa chama hakitaki ubabaishaji kwenye kusimamia sheria lakini utu uzingaitiwe.

WATENDAJI KUKWAMISHA JITIHADA ZA SERIKALI Kuhusina na Kilimo, Dk Bashiru alisema  kuna jitihada zinazofanywa na Serikali kuwakomboa wakulima lakini  wapo watu wachache  wanaofanya juhudi za kukwamisha jitihada hizo.

Alitoa mfano juhudi zilizofanyika kwenye zao la kahawa mkoani Kagera kwa kuweka mikakati ya kuwanufaisha wazalishaji kupitia vyama vya ushirika, lakini waliohusika kuviua vyama hivyo wamekuwa mstari wa mbele kuhujumu mkakati wa serikali.

“Nyie mnaotokea Kagera mmesikia hali ya soko la Kahawa, tumejaribu kuzuia uporaji kwa kuwataka wazalishaji kufuata utaratibu kupitia vyama vya ushirika, kilichofanyika na wengine ni viongozi waliohusika kuviua kumeibuka vuta nikuvute.

“Sasa serikali inataka kuinua zao la kahawa sauti zenu ziko wapi?  Mbona hazisikiki kama zilivyosikika kwenye korosho?” alihoji Dk.Bashiru.

ASHANGAA UWT KUKAA KIMYA KATIKA ELIMU

Dk. Bashiru alieleza elimu ndiyo msingi utakaojenga nidhamu na utamaduni wa taifa, lakini bado sekta hiyo inahitaji uangalizi wa kutosha.

Alisema shule za umma ndizo zinapaswa kuwa kiongozi, hata hivyo licha ya udahili kuimarika bado usimamizi wake si mzuri, kuanzia ubora, maslahi na mazingira ya kufundishia.

“Kuna wengine walikuja na mjadala kuhusu mimba za utotoni wakitaka wanafunzi wanaopewa ujauzito kuendelea na masomo, tunakuwa wachovu wa kufikiri kwenda kushughulikia chanzo cha tatizo ikiwamo utoro.

Alisema kuna tatizo la walimu kujihusisha katika mapenzi na wanafunzi na kuwaadhibu wanafunzi mpaka kufikia hatua ya kufariki dunia au kupata ulemavu.

Alihoji, Je wanapata mafunzo sahihi vyuoni?

“Lakini kuna tabia za walimu ya kujihusisha kwenye mapenzi na wanafunzi, ukatili kwa kumuadhibu mwanafunzi hadi kumsababishia ulemavu au kumuua,tujiulize, je? wanapata mafunzo ya kutosha vyuoni?” alihoji Dk.Bashiru.

Alisema jamii haipaswi kukubali vitendo hivyo kuendelea kutokea na kuvizoea kwa sababu  elimu ni kioo cha taifa.

Alisema   changamoto za msingi hazijadiliwi ikiwamo UWT kukishauri chama kuhusu hali ya elimu nchini na hatua za kuiboresha.

ALIA NA MAKUNDI NDANI YA CHAMA

Dk. Bashiru alikiri kuwa ndani ya CCM bado kuna makundi yaliyosababishwa na uchaguzi kutosimamia muungano, utovu wa nidhamu na kukosekana   umoja.

Katibu mkuu alisema CCM hakitamvumilia kiongozi kutumia muda, rasilimali za serikali kusaka na kuendesha makundi ya wasaka vyeo.

“Nasema kuna chama kimoja na Rais mmoja, kusaka urais kabla ya muda huko ni kujishushia sifa.

“Kila mmoja jina lake tunalo, kipi alichosema, wapi walipokutana na muda ukifika tuta – print (kuchapisha) na tutawaonyesha.

“Cheo hicho ni cha watu wote si mtu kujipitisha, urais si wa mapambo ni sifa. Mtu anayefaa kuwa rais anaombwa,” alieleza huku akishangiliwa na wajumbe wa baraza hilo.

Kadhalika, alisema changamoto nyingine iliyopo ni kukosekana kwa umoja baina ya watendaji wa serikali na chama.

“Waziri haelewani na Naibu. Mkuu wa mkoa haelewani na RAS. DC (Mkuu wa wilaya) ana mgombea wake makatibu nao wana wagombea wao. Hakuna kazi inayofanyika hapo ni vyeo tu,” alisema.

KUWALINDA WABUNGE

Kuhusiana na wanaotaka ubunge kabla ya muda Dk.Bashiru alisema atawalinda ambao kwa sasa wapo madarakani.

“Nimewaeleza wabunge watulie, nitawalinda, wawape nafasi ya kufanyakazi, muda ukifika wataarifiwa,”alisema.

MWENYEKITI MKOA WA MARA KUSHTAKIWA

Dk.Bashiru  alisema ataandaa mashtaka ya maadili dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara baada ya kuingilia uchaguzi wa makamu mwenyekiti kwenye halmashauri.

Alisema vikao halali vya chama vilipitisha majina ya wagombea wawili kati ya watatu lakini alimshinikiza aliyekuwa akikaimu nafasi ya ukatibu kuongeza jina la tatu   la mgombea aliyekatwa baada ya kufanya kosa la maadili.

KUNA MITAMBO YA UONGO CCM

Katibu huyo alisema   ndani ya chama kumejaa watu ambao wamekuwa wakitunga uongo kwa lengo la kuwadhoofisha   wenzao katika siasa.

“Mitambo ya uongo imejaa ndani ya chama na kwenye jumuiya kwa lengo la kudhoofisha wenzao katika siasa,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (UWT) Gaudensia Kabaka, alisema  makundi ya uchaguzi bado yanaitafuna Jumuiya hiyo.

Katika hatua nyingine Umoja  ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) unatarajiwa kuwa na kikao cha  Baraza Kuu la Umoja huo   Jijini hapa leo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Umoja huo, Raymond Mwangwala, alisema  Dk.Bashiru   anaratajiwa kuwa mgeni rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles