Katibu Mkuu CCM ataja sababu wanachama kususia uchaguzi kura za maoni

0
1176

Anna Potinus

Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally ameweka wazi changamoto mbalimbali ambazo chama hicho kimekumbana nazo katika mchakato wa upatikanaji wa wagombea kwenye mitaa na vijiji ambazo zimesababisha baadhi ya wapiga kura kususa.

Dk. Bashiru amesema hayo leo Jumatatu Oktoba 21, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo pamoja na mnambo mengine ametoa maelekezo kwa kamati za siasa za ngazi husika kuchukua hatua juu ya changamoto hizo.

“Yako maeneo ambayo hayakuzingatia kanuni kwani tunayo kanuni ya uteuzi ndani ya chama chetu inayoelekeza utaratibu wa kuwapata wagombea, kuwachuja, kuchukua fomu, kupiga kura za maoni na kuteua hivyo baadhi ya maeneo hayakuzingatia hili.

“Yako maeneo ambayo hapakuwepo na maelewano na wakati mwingine kumekuwepo na mabishano na kutoridhishwa na mchujo na kura za maoni kule ambako zimefanyika, yapo baadhi ya maeneo migongano hiyo imezuia mchakato wa kupiga kura kuendelea au baadhi ya wapiga kura kususa na kuamua kukaa kando.

“Kuna maeneo hasa Dar es Salaam na zaidi Wilaya ya Kinondoni ambapo wasimamizi walichelewa kuanza, maeneo mengine walianza saa tisa alasiri wakati tulikubaliana waanze saa nne asubuhi baada ya ibada na wanachama wengi sana walijitokeza kwa wingi lakini wasimamizi wakachelewa,” amesema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru amesema ili kutoa nafasi ya kutosha kwa marekebisho hayo mchakato wa ndani umeongezwa kwa siku mbili zaidi ambapo awali ilikuwa umalizike Oktoba 29 sasa utamalizika Oktoba 31 ili waweze kwenda kuchukua fomu za wagombea wa CCM ambao watashindana na vyama vingine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here