IPTL yasema ipo tayari kulipa bilioni 426.6/-

0
605

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imekubali kulipa Dola za Marekani 185,449,440 ambazo ni sawa na Sh 426,533,712,000 kwa Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited (SCBHK) ikiwa itabainika ni deni halali.

IPTL imeomba ilipwe malimbikizo ya fedha zake zote inazoidai Tanesco kwani kutoilipa ni kuidhoofisha na kuinyima uwezo na uweledi wa kukabiliana na changamoto zake.

Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa IPTL, Wakili Joseph Makandege katika tamko alilotoa kwa vyombo vya habari baada ya Benki Standard Chartered kupata tuzo ya kulipwa kiasi hicho cha fedha.

“Tumekubaliana na msimamo wa Serikali, tunatambua kwamba kama mdhamini wa IPTL, Serikali haiwajibiki kuilipia IPTL madeni yake, jukumu hilo ni la IPTL.

“Serikali inawajibika tu kusimamia na kuhakikisha kwamba IPTL inalipa madeni yake yote halali inayodaiwa na wadai wake, deni hilo la SCBHK likiwemo, kama kweli ni deni halali la IPTL,” alisema.

Kampuni hiyo ilieleza kustaajabishwa na taarifa zilizochapishwa kwenye vyombo vya habari nchini,  kwamba SCBHK imepata tuzo ya Sh 426,533,712,000 dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kesi ya usuluhishi Na. ARB/05/04 ya mwaka 2015 katika Baraza la Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) huko London nchini Uingereza.

Makandege alisema IPTL imepokea tamko la Serikali kupitia vyombo vya habari, lililotoa msimamo kwamba Serikali  na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), haziwajibiki kuilipa SCBHK fedha hizo na kwamba Serikali siyo mdaiwa bali ni  mdhamini tu katika masuala ya IPTL.

Alisema kwamba mdaiwa anayewajibika kulipa fedha hizo ni IPTL ambayo ilitoa kinga inayoikinga Serikali na taasisi zake dhidi ya madai yoyote yatokanayo na kupewa fedha zilizokuwa katika iliyokuwa akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Hata hivyo, kwa sasa IPTL haijawatambua SCBHK kama wadai wake na inahoji mahakamani uhalali wa madai yao hayo.

“IPTL imewafungulia SCBHK mashauri mbalimbali (Shauri la Madai Na. 60 la mwaka 2014, shauri la maombi Na. 801 na 802 ya mwaka 2016, na mashauri ya biashara Na. 67 na 75 ya mwaka 2017) yanayoendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

“Katika mashauri hayo, pamoja na nafuu nyinginezo, IPTL inaiomba Mahakama Kuu itamke rasmi kwamba SCBHK siyo wadai wake na ibatilishe tuzo mbalimbali, ambazo SCBHK ilipewa huko Ulaya bila kuwepo IPTL (ambayo ndiyo mhusika mkuu katika migogoro husika).

“IPTL pia inaidai SCBHK fidia ya jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 3.240  ambazo ni sawa na Sh trilioni 6.5,” alisema Makandege katika tamko hilo. 

Alisema madai na tuzo hiyo ya SCBHK ni miongoni mwa masuala ambayo bado yanabishaniwa na ambayo IPTL bado ina haki ya kuyahoji na fursa ya kuyabatilisha mahakamani.

Makandege alisema SCBHK pia bado inapaswa kuthibitisha uhalali wa tuzo hiyo katika mahakama za Tanzania.

 Maamuzi ya Mahakama za Tanzania (Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, kama yeyote atarufani) ndiyo yatahitimisha mzozo kama kweli SCBHK ni mdai halali wa IPTL au vinginevyo.

“Endapo IPTL hatimaye itashinda katika mashauri yake hayo, SCBHK yaweza kupoteza kabisa uhalali wa kuendelea kuibughudhi IPTL na Serikali kwa madai yake au yaweza kukata deni lake hilo la Sh bilioni 426.53 katika Sh trilioni 6.5 inazodaiwa na IPTL na kuilipa IPTL kiasi kitakachobakia.

“Hata kama itashindwa katika mashauri yake hayo, IPTL haitashindwa kulipa deni hilo la SCBHK kwani kiwanda na rasilimali zake nyingine zinatosha kuuzwa na kulipia madeni yake sambamba na hilo la SCBHK.

“Kama mazungumzo yatahitajika, IPTL siyo Serikali itazungumza na kukubaliana na SCBHK, kwani IPTL na SCBHK ndiyo wadaawa katika mashauri husika, wenye haki na wajibu huo,” alisema.

Alisema ingawa IPTL inakubaliana na msimamo wa Serikali, ni rai yao kwamba kwa sasa haijashindwa kulipa deni hilo bali bado inatumia haki yake ya msingi na ya kikatiba kuhoji madai ya SCBHK mahakamani.

Makandege alisema IPTL itawajibika tu kulipa deni hilo na Serikali italazimika tu kuiwajibisha kufanya hivyo, pindi itakaposhindwa katika mashauri yake yanayoendelea mahakamani hapa nchini.

Alisema hakuna haja Watanzania na wadau wote wa IPTL kutaharuki, ingawa hadi sasa haijarudishiwa leseni yake ya kufua na kusambaza umeme.

“IPTL bado ni kampuni binafsi iliyo hai na yenye rasilimali lukuki, miundombinu iliyokamilika na uongozi thabiti unaotosha kusimamia haki na maslahi ya kila mdau wa IPTL.

“Pia IPTL inaomba ilipwe malimbikizo ya fedha zake inazoidai Tanesco. Kutoilipa IPTL fedha hizo ni kuidhoofisha na kuinyima uwezo na uweledi wa kukabiliana na changamoto zake yenyewe,” alisema Makandege.

Katika muktadha huo, IPTL inakubaliana na inaunga mkono kwa dhati msimamo wa Serikali na inaahidi kufanya kila liwezalo kulipa madeni yake, lakini inaomba iwezeshwe kufanya hivyo kwa kulipwa madeni yake na kurudishiwa leseni yake ya kufua na kusambaza umeme wa bei nafuu na wa uhakika kwa maendeleo ya Watanzania na taifa zima katika uchumi wa viwanda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here