26.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 7, 2021

Karia aapa kuwabana zaidi wabadhrifu

ELIYA MBONEA-ARUSHA

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema ataendelea kula sahani moja na watu wanaoiba fedha za taasisi hiyo pamoja na wanaowaunga mkono.

Karia alitoa kauli hiyo jana wakati wa Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.

Miongoni mwa ajenda za mkutano huo zilikuwa kuthibitisha muhtasari wa mkutano uliopita wa TFF, yatokanayo na mkutano uliopita, hotuba ya Rais, taarifa kutoka kwa wanachama, kupitisha taarifa ya utendaji wa Kamati  ya Utendaji, kupitisha taarifa ya hesabu za mwaka zilizokaguliwa na  kupitisha taarifa ya ukaguzi na utekelezaji wake.

Nyingine ni kupitisha bajeti ya mwaka 2019, uchaguzi mdogo, kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba, kujadili mapendekezo kutoka kwa wanachama au kamati ya utendaji.

“Hakuna mtu aliyeonewa na tutaendelea kufuata taratibu, ambaye ataungana na mtu aliyeiba hela nitamshughulikia na yeye sitamwacha, sisi tupo kwa ajili ya kutengeneza mpira vizuri, ninachowaomba tushirikiane ofisi yangu iko wazi, mambo ya mpira njoo uzungumze na Karia.”

Karia alisema wale wanaokula fedha za TFF kuanzia wilayani, mkoani hadi taifa atahakikisha wanaangukia kwenye mikono ya sheria.

“Zipo taasisi na wafadhili ndani na nje ya nchi wana nia ya dhati kabisa ya kufadhili michuano mbalimbali chini ya TFF, lakini kutokana na uroho wa fedha kwa baadhi ya watu, taasisi hizi zimeshindwa kuja,” alisema Karia.

Alizungumzia mwenendo wa soka la ufukweni hapa nchini kwa kusema limepanda, Tanzania ikiwa nafasi ya 58 duniani na ya saba Afrika.

“Tupo nafasi ya 7 kwa Afrika na 58 duniani, hivyo tunaamini tunaweza kuingia hata kwenye 10 bora kwa dunia.

Kuhusu Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alisema: “Changamoto ambazo tunaziona zitaathiri Ligi Daraja la Kwanza tutazifanyia kazi, tutaanzisha ligi ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, lakini pia tutaanzisha ligi ya vijana wenye umri chini ya miaka 15,” alisema Karia.

Wakati huo huo Karia aliiagiza Kamati ya Nidhamu na Maadili ya TFF kuwachukulia hatua kali watu wote waliokula fedha za shirikisho hilo.

“Tunataka kuchukua hatua hizi ili kuhakikisha viongozi wa vyama vya soka nchini wanafanya kazi kwa kufuata sheria na maadili ikiwamo uaminifu.

“Sijawahi kuingilia uamuzi uliotolewa na kamati, najua namna utawala bora unavyotakiwa. Utawala bora na wenye uwazi ndiyo siri ya uongozi wangu, nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa, nawaagiza wajumbe, vyama vya soka mkafanye haya,” alisema.

Karia alisema kamwe TFF haiwezi kujitenga na Serikali iliyopo madarakani kwa kuwa imekuwa karibu kuhakikisha Tanzania inapiga hatua.

“Mahusiano yetu ni mazuri, Serikali ipo karibu na sisi ndio maana hata maandalizi ya Afcon kwa vijana wapo karibu yetu, ukijitenga kufanya kazi na Serikali unaweza kukwama mbele ya safari,” alisema Karia.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ambaye alipata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo alimsifu Karia kwa kumwelezea ni mtu mwadilifu.

Akizungumza na wajumbe waliohudhuria mkutano huo, Gambo, alisema anamfahamu Karia tangu akiwa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

“Nikiwa mkuu wa wilaya, wewe ulikuwa mkurugenzi Mvomero, nakufahamu ni mtu mwenye misimamo, mchapakazi na mwadilifu,” alisema Gambo.

Akizungumzia kuhusu mikakati ya kuendeleza soka nchini, Gambo, aliahidi kutoa hekari 15 ili zitumike kujenga viwanja wa michezo mbalimbali ikiwamo soka.

“Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinamiliki viwanja vingi hapa nchini, ni vyema kwa sasa mkahakikisha TFF kila mkoa mnakuwa na viwanja vyenu ili msiingiliane na viwanja hivyo,” alisema RC Gambo na kuongeza:

“TFF kwa sasa imeonyesha wazi kuwa na dira na mwonekano wa kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu na kwa mfano huu mna kila sababu ya kuungwa mkono na ndio maana mimi naanza na kutoa hekari 15.”

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga, aliipongeza TFF akisema inafanya kazi nzuri ya kuendeleza soka.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mliyofanya na naomba muyaendeleze hayo mliyoyapanga, leo tumesikia utekelezaji wa mipango hiyo na tunawapongeza.

“Mheshimiwa Gambo umeutendea haki mpira. Hilo wazo la kujenga uwanja ni zuri. Nawaomba wakuu wa mikoa mingine waige,” alisema Tenga ambaye pia ni Rais wa heshima wa TFF.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,424FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles