28.3 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

27 wakamatwa mauji ya watoto Njombe

Elizabeth Kilindi-Njombe

SIKU chache baada ya Kikosi Maalumu cha Operesheni kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini kutua mkoani Njombe chini ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Marijamani, kwa ajili ya kuchunguza matukio ya mauaji ya watoto, hatimaye jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watu 27.

Mauaji hayo ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya watoto saba wakiwamo wa familia moja huku mauaji hayo yakihusishwa na imani za kishirikina.

Akizungumza na MTANZANIA jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe,  Renatha Mzinga, alisema hadi sasa jeshi hilo linawashikilia watu 27 kutokana na mauji hayo.

“Mpaka sasa tunawashikilia watu 27 kwa mahojiano na uchunguzi wa matukio haya na bado tunaendelea kuwakamata na kuwahoji zaidi. Kubwa tunawaomba wananchi watupe ushirikiano Jeshi la Polisi ili tuweze kukomesha mauaji haya ya kinyama pamoja na mtandao mzima wa kihalifu katika mkoa wetu wa Njombe,” alisema Kamanda Mzinga.

Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Njombe, wamesema kwa sasa bado hali ya usalama si shwari huku hofu ikitanda katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

“Bado hatuna amani kila siku tunapeleka na kuwarudisha watoto shule kwa kweli jambo hili limekuwa likitufanya hata tushindwe kuendelea na shughuli za uzalishaji. Ila bado tuna imani na vyombo vyetu vya usalama kwamba vitapambana na wahalifu hao ambao wamekuwa wakisababisha tuishi kwa hofu,” alisema Agatha Mlowe.

MBUNGE ALAANI MAUJI

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Njombe, Neema Mgaya (CCM), amelaani vikali mauaji ya watoto wadogo yanayoendelea mkoani Njombe.

Amesema matukio hayo, yamechafua taswira ya mkoa huo ambao tangu kuanzishwa kwake haukuwahi kuwa na mauaji ya ajabu kama hayo.

Akizungumza juzi wakati akitoa pole kwenye msiba wa mwanafunzi wa darasa la pili wa Shule ya Msingi Matembwe, Rachel Malekela (7) aliyefariki dunia kwa kuchinjwa na kutupwa kichakani, Mgaya alisema matukio hayo yanasikitisha kwa sababu yanakatisha uhai kwa watoto wasiokuwa na hatia.

 ‘’Napiga vita vikali huu mwenendo unaoendelea wa kuokoteza watoto siku hadi siku, inasikitisha mno.

‘’Mimi ni mama, ninazungumza haya kwa uchungu wanauawa  watoto kikatili, wamekosa nini…Njombe mambo haya hatuna yametoka wapi,”alihoji.

Aliwataka wananchi kushirikina na vyombo vya usalama kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za awali ili ziweze kufuatilia kwa karibu  na kuwakamata wahalifu.

 Mauaji hayo yamefikisha idadi ya watoto saba ambao wamekutwa vichakani na kwenye mabwawa wakiwa wamefariki dunia kwa kuchinjwa.

WATATU WAUAWA

Wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu mauaji hayo yanayoendelea mwishoni mwa wiki iliyopita watu wawili waliuawa wilayani Ludewa kwa kushambuliwa na wananchi wa Kijiji cha Luvuyo, Kata ya Madope.

Watu hao waliuawa baada ya wananchi kuwahisi kuwa ni miongoni mwa wanaodhaniwa kuhusika na matukio ya utekaji na mauaji ya watoto.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere, alithibitisha tukio hilo.

Alisema kabla mauti hayajawakuta watu hao walionekana wakitaka kujificha eneo la kisima ambacho watoto wanapenda kuchota maji ndipo wananchi hao walipochukua uamuzi huo wakidhani kuwa ni wauaji.

“Basi wananchi wakaitana wakawateka, walipowateka viongozi wa kijiji wakapata taarifa hiyo walipoanza kuwapiga viongozi wakaamua kuwaingiza lokapu ya kijiji.

“Lakini wananchi wakaendelea kuitana kwa umoja wao wakavunja hiyo lokapu ya Serikali, wakawatoa nje wakaanza kuwapiga mpaka wakawaua,” alisema DC Tsere.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Ludewa alisema kati ya watu hao wawili waliouawa, mmoja ametambulika kuwa ni mkazi wa Kijiji cha Luvuyo ambaye bado jina lake halijafahamika, lakini anajulikana kwenye kijiji hicho.

WANGING’OMBE

Tukio jingine ni lile lililotokea wilayani Wanging’ombe ambako mtu mmoja aliyetambulika kwa majina ya Ibrahim Sanga, aliuawa juzi saa moja jioni na wananchi wenye hasira.

Tukio hilo lilitokea katika Kata ya Usuka, Ibrahim na mwenzake ambaye amejeruhiwa walidhaniwa kuwa ni watekaji na wauaji wa watoto.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Igwachanya Wilaya ya Wanging’ombe, Adamu Dononda, alisema marehemu alikuwa mkazi wa Kijiji na Kata ya Igwachanya, lakini tukio hilo limetokea katika Kata ya Usuka maeneo ya sekondari ambako marehemu akiwa na rafiki yake walikutwa wamesimama na mwanafunzi wa kike wa shule ya sekondari ndipo wananchi wakapiga yowe na kukusanyika kufanya mauaji hayo.

Ofisa mtendaji huyo alimtaja majeruhi kuwa ni Given Nyachi ambaye amejeruhiwa vibaya na kwa sasa amelazwa katika Hospital ya Ikelu kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwili wa marehemu Ibrahimu umesafirishwa kwenda nyumbani kwao jijini Mbeya kwa ajili ya mazishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles