26.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

‘MINZIRO’ Kocha anayesakamwa na mkosi wa kutimuliwa katikati ya mafanikio

ZAINAB IDDY

NI shabiki gani wa soka hapa ambaye hajapata kulisikia jina la Fredy Felix Minziro? Kama yupo basi huyo hana muda mrefu tangu ameanza kuufuatilia mchezo huo.

Minziro ni supastaa wa zamani wa timu ya Yanga, lakini hata baada ya kutundika daluga ameendelea kuwa masikioni mwa wapenzi wa mchezo wa soka kutokana na kufanya kazi ya ukocha.

Kwa miaka mingi sasa amekuwa akifanya kazi ya kuzinoa timu mbalimbali na nyingi zimepata mafanikio zikiwa chini yake.

Miongoni wa klabu za Ligi Kuu alizopata fursa ya kuzifundisha ni pamoja na Yanga yenyewe, Tanzania Prisons, JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania), Singida United, KMC kabla ya kuinoa timu ya  Arusha United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Pamoja na umaarufu wake katika medani ya soka la Tanzania, Minziro amekuwa ni mtu mwenye bahati mbaya unaweza kusema hivyo.

Unajua ni kwanini?

Kocha huyo mwenye mizuka ya ajabu anapokuwa katika benchi, ana historia ya kuziwezesha kuzipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara timu za madaraja ya chini, lakini shukrani anayopewa na waajiri wake baada ya hapo ni kufungashiwa virago.

Mabalaa hayo alikutana nayo wakati akizinoa Singida United na KMC kabla ya hivi karibuni kukusanyiwa kila kilicho chake pale Arusha United ambayo tayari  imeonyesha uelekeo mzuri wa kufuzu Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Kutua Arusha United

Minziro alijiunga na Arusha United kwa mkataba wa mwaka mmoja, akiwa mkuu wa benchi la ufundi, ikiwa ni muda mfupi baada ya kutimuliwa KMC.

Huko Arusha United alikuwa akisaidiana na Fikiri Elias ambaye ni kocha msaidizi.

Baada ya kutua jijini Arusha, Minziro alifanya usajili wa wachezaji wengi wazawa ndani ya kikosi chake akiwachanganya wakongwe na vijana.

Alifanya hivyo akiamini uzoefu wa wachezaji wakongwe utamsaidia kuipandisha Arusha United daraja.

Miongoni mwa wachezaji wakongwe aliowaingiza katika kikosi cha timu hiyo ni kiungo Abdulhalim Humud na washambuliaji  Zahoro Pazi na Yusuph Mgwao, ambao wamepata kutamba na klabu mbalimbali na timu ya  Taifa, Taifa Stars.

Alipoiacha Arusha United

Hadi anaondolewa Arusha United, Minziro, ameiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi B wa Ligi Daraja La Kwanza, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi 11.

Katika michezo hiyo, Arusha United imeshinda mara tano, sare tatu na kupoteza michezo mitatu pekee.

Mwenyewe afunguka

Minziro ameliambia MTANZANIA kuwa aliziona dalili za yeye kuondoka Arusha United, lakini aliamua kukaa kimya bila kufungua mdomo wake, akisubiri kuona nini kitakachotokea.

“Unasemaje timu inafanya vibaya wakati inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 18, huku anayeongoza akiwa na pointi 23, niwazi walipanga kuniondoa kwa sababu wanazozijua wao.

“Kabla ya kunipa taarifa ya kuvunja mkataba wangu, nilianza kuwasikia baadhi ya viongozi wakisema pointi 18 tulizovuna katika michezo 11 zilikuwa ndogo, hivyo wanamleta Moroco (Hemed) tusaidiane na sikuona tatizo.

“Hapo ndio kwanza mzunguko wa kwanza hata ule wa pili bado, lakini wanakata tamaa, nilishaelewa natafutiwa sababu, wamenipa stahiki zangu naangalia maisha mengine,” anasema Minziro kwa masikitiko na kuongeza:

“Kwa sasa nasubiri kuona Arusha United ikipanda daraja, lakini pia silaumu sana kuondoka pale, pengine ningeipandisha timu alafu baada ya hapo nikafukuzwa kama  ilivyotokea huko nyuma.”

Wadau wamkingia kifua

Mshambuliaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King’ anasema: “ Viongozi wa timu za Tanzania akili zao zinafanana sana, wanaweza kuwa na kocha anayesaidia kupata matokeo mazuri lakini wakamfukuza pale tu wanapoona ameenda kinyume na mahitaji yao.

“Nina uhakika Minziro ni kocha mzuri na rekodi zake zinambeba, lakini huenda kuna vitu amekosana na mabosi wake wakaamua kumfukuza, lakini kuhusu timu kutopata matokeo mazuri si kweli kwani ipo nafasi ya tatu sasa,” anasema King.

“Sitaki kumhukumu moja kwa moja Minziro wala uongozi wa Arusha United kwani wao ndio wanajua ukweli ni upi, lakini siku zote kocha anaajiriwa ili kufukuzwa, nina hakika Arusha United isipopanda daraja viongozi watakimbiana.

“Namwomba Minziro awe na uvumilivu, timu nyingi zinahitaji huduma yake na kwa kuwa ni kocha mwenye daraja A siku si nyingi tutasikia mazuri kutoka kwake,” anasema Kenny Mwaisabula, ambaye ni kocha na mchambuzi mahiri wa soka nchini.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,451FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles