MELBOURNE, AUSTRALIA
MKUU wa shughuli za mahesabu katika Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, Kadinali George Pell jana alikuwa kiongozi wa kwanza wa juu kabisa wa kanisa hilo kufikishwa mahakamani.
Kardinali huyo mkongwe, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikabiliwa na tuhuma kuhusu visa vya ngono vilivyoliandama kanisa hilo, ameapa kupambana vikali mahakamani kupinga mashitaka hayo.
Pell (76), hakuonesha hisia zozote wakati wote alipokuwa akisikiliza mashitaka yanayomkabili katika mahakama ya mjini Melbourne, Australia.
Alifikishwa mbele ya jopo la wazee wa mahakama kwa mashtaka kadhaa, ingawa nusu ya tuhuma zinazomkabili, zikiwemo nyingine kubwa zaidi, zilitupiliwa mbali.
Akiwa Mahakamani Pell alisisitiza kwamba hana makosa yoyote.
Kesi hiyo inasubiriwa kujadiliwa leo na kupanga tarehe kamili kwa kardinali huyo kufikishwa mahakamani.